Pages

Showing posts with label Taifa Stars - Timu ya Taifa. Show all posts
Showing posts with label Taifa Stars - Timu ya Taifa. Show all posts

Thursday, August 16, 2012

TAIFA STARS YATOKA SULUHU NA BOTSWANA

Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana, ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana, ‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na Lemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja.
Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37.
Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd.
Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha.
Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza.
Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.

Tuesday, August 14, 2012

Taifa Stars yawasili salama Gaboron Bostwana

Wachezaji wa Timu ya Taifa, Taifa Stars wakiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama Mjini Gaborone, Botswana leo mchana tayari kwa mchezo wa kirafiki na The Zebras ya Botswana kesho Jumatano jioni katika Uwanja wa Taifa wa Molepolole.
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kikiwa na wachezaji 17 kimewasili leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji Botswana 'Zebras' itakayochezwa kesho (Agosti 15 mwaka huu).

Stars ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa 5.45 asubuhi kwa saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania wanaoishi hapa Botswana.

Baadhi ya wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan Singano na Simon Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache baada ya kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).

Wachezaji wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah, Athuman Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto,Ramadhan Chombo, Salum Abubakar, Said Bahanuzi na Shabani Nditi.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia kwenye hoteli ya Oasis ambayo pia ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi hiyo. Mechi itaanza kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika kwenye Uwanja wa Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi sasa uko kwenye matengenezo.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile timu yake bado inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika, na michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) inayotarajia kuanza baadaye mwaka huu.

Popular Posts