Usomi wa ngazi mbalimbali si sifa ya mtu kufaa kuwa kiongozi, dunia katika historia yake ina majina lukuki ya baadhi ya viongozi ambao walikuwa wasomi, lakini hatima ya uongozi wao haikutofautiana na wajinga.
Bila kwenda mbali na tuangalie hata hapo nyumbani Zanzibar kuna baadhi ya viongozi serikalini, kwenye mashirika kwenye Baraza la wanaotuwakilisha na hata kwenye sekta binafsi ambao wakikuonesha vyeti vyao vya unaweza kuogopa, lakini utendaji wao ni kichefuchefu.
Kisaikolijia sifa za kiongozi ziko wazi na ni muhimu, mtu kuwa nazo kabla au baada ya kupewa cheo. Leo tunataka kuziangalia kwa undani sifa hizi, ili kama wananchi au viongozi wenye dhamana ya kuchagua watu wa kuongoza tuwatazame watu kwa sifa zao kabla na baada ya kuwapa nafasi. Sifa za kiongozi ni hizi zifuatazo:
Awaze mafanikio makubwa
Kiongozi bora lazima awe na maono ya juu ya kuhakikisha kuwa nchi yake, kampuni yake sekta yake inapata mafanikio makubwa, hii ndiyo itakuwa dira ya kazi yake itakayompa muongozo wa kusimamia wafanyakazi na watendaji wote walio chini yake kufikia kiwango cha mafanikio anachokiwaza. Kiongozi asiyekuwa na mawazo ya juu ya kuendelea kutoka mahali alipo hafai.
Awe na nia
Haitoshi kwa kiongozi kuwa na mawazo chanya peke yake bila kuwa na nia ya kuyatimiza. Hivyo, kiongozi atafaa kuchaguliwa kuwa kiongozi endapo tu atakuwa na uwezo wa kuratibu vyema na kutekeleza alichowaza. Ajue njia anayopita, awatangulie anaowaongoza kwa vitendo.
Ajitambue mwenyewe
Lazima kiongozi ajitambue mwenyewe ni mtu wa namna gani, ajue uwezo wake na upungufu wake na awe tayari kujiongezea maarifa kila siku, ili aweze kukabili changamoto na mabadiliko ya ulimwengu. Asome, afuatilie mambo yanavyokwenda na ajifunze kwa wenzake kuhusu kufanikisha malengo yake.
Asimamie maamuzi
Kuna wakati malengo hukumbana na vikwazo, hivyo ni wajibu wa kiongozi kusimamia maamuzi sahihi na kuwa mtu wa mwisho. Kiongozi mwenye kubadilika badilika kama kinyonga, hafai kwa vile kukosa msimamo kuna maanisha udhaifu wa mipango na kujiamini.
Adhibiti msongo wa mawazo
Tunamtarajia kiongozi mzuri awe ni mtu mwenye kupunguza msongo wa mawazo, ili kuifanya akili yake ifikie maamuzi sahihi, lakini kama atakuwa mwenye kuwaza mengi, atajikuta anachanganyikiwa na kuwa mtu wa jazba katika maamuzi na hivyo kuipotosha jamii.
Akubali kukosolewa
Viongozi wasiokuwa na sifa za uongozi huwa hawakubali kukosolewa, wakidhani kuwa hiyo ndiyo njia ya kuthibitisha msimamo wao na usahihi wao. Kiongozi makini ni yule ambaye atakuwa tayari kukosolewa na kuwapongeza wanaomkosoa kwa kutazama mwenendo wake na usahihi wake. Asiyekubali kukosolewa hafai kuwa kiongozi.
Awe msikilizaji
Kiongozi mzuri ni yule ambaye atakuwa tayari kuwasilikiza watu walio chini yake, apokee maoni yao na ikiwezekana ayafanyie kazi. Lakini pia anatakiwa kuwafahamu kwa undani, ili aweze kuwaongoza vema kufuatana na hali zao. Akiwa na watu walemavu wenye kasoro kadhaa wa kadhaa anatakiwa kuwatambua kabla na baada ya kuwa kiongozi wao. Kuongoza usichokifahamu ni ujinga.
Afuate haki
Kiongozi imara anatakiwa kufuata haki katika kuongoza kwake, asijione mwenye haki zaidi ya wale anaowaongoza katika sheria. Ni muhimu kwake kuwafanya walio chini yake kujiona wako huru katika mawazo na matendo. Kiongozi anayetumia nguvu na ukali kuongoza watu hafai. Hata yule mwenye kujivunia uongozi wake naye hafai.
Awe egemeo la watu
Sifa nyingine ya kiongozi ni kuwa egemeo la watu wake katika shida na raha. Kiongozi mzuri ni yule ambaye atakuwa tayari kusikitika, kuomboleza, kufurahi pamoja na watu wa chini yake bila kujitenga nao. Ajitolee kuwatumikia watu kwa hali na mali na awe tayari kutumika zaidi kwa maslahi ya wengine.
Atie moyo watu
Kiongozi mzuri ni yule ambaye atakuwa na uwezo wa kuwatia moyo walio chini yake ili waweze kuendeleza vipaji vyao. Haipendezi kwa kiongozi kuwavunja moyo watu kwa kauli za kudharau kazi na jitihada zao walizojaribu kufanya katika kutekeleza majukumu yao kama wafanyakazi au wananchi.
Afurahie mafanikio
Sifa nyingine muhimu ya kiongozi ni kuwa tayari kufurahia mafanikio aliyopata pamoja na watu wake. Ni wajibu wa kiongozi kutoa tuzo, kuwashukuru wafanyakazi wake na kuwa tayari kuwapa ofa. Hii itasaidia kuwafanya watu waone hawajapoteza nguvu zao katika utendaji wao na kwamba wanakubalika. Si busara wakati mwingine kuwakosoa watu mbele ya hadhara na kueleza kutofurahishwa na kazi zao.
Aungane na wa chini yake
Mtu kuwa kiongozi haimaanishi amekuwa wa tofauti na watu wengine kiasi cha kushindwa kuchangamana nao kama wanavyofanya baadhi ya viongozi. Kiongozi mwema ni yule atakayeungana na watu wake katika maisha ya kawaida. Kuwa kiongozi haimaanishi kwamba watu watakufuata wewe kila siku, wakati mwingine wewe unatakiwa kuwafuata wao na kuwa nyuma yao hata mahali walipokosea au wanapokabiliwa na makosa, watetee na uoneshe kuwajali na kuwapigania, makosa utayahesabu baada ya utetezi wako kukamilika.
Akubali lawama
Kama kiongozi amefanya mambo ambayo jamii haikupendezwa nayo anachotakiwa kufanya ni kukubali kulaumiwa. Ikiwa anaongoza kitego cha umeme kwa mfano na watu hawakupata nishati hiyo kwa wakati hatakiwi kukwepa lawama, vivyo hivyo kwenye wizara na idara au nchi kwa ujumla.
Afahamu kutatua matatizo
Kiongozi mzuri ni yule ambaye atakuwa na uwezo wa kuzuia migogoro na kuitatua kwa haraka. Muongozo mzuri katika eneo hili umesimama katika mawasiliano na watu wa chini, mawasiliano haya ndiyo yatakayomuwezesha kiongozi kujua matatizo waliyonayo wafanyakazi wake au hata jamii anayoiongoza na hivyo kumfanya apate wasaa wa kuyashughulikia mapema.
Ajifunze kwa makosa
Wakati mwingine mawazo na mipango inaweza ikaenda kombo, hivyo ni wajibu wa kiongozi kujifunza kutokana na makosa yake au ya wale anaowaongoza, ili kuepuka kurudia makosa yale yale na kumfanya apoteze sifa za kuwa kiongozi mzuri.
Mwanafalsafa Winston Churchill aliwahi kusema “The price of greatness is responsibility.” Thamani ya ukuu ni uwajibikaji.
Awe mwaminifu
Miongoni mwa maeneo magumu kabisa yaliyowashinda na yanayoendelea kuwashinda viongozi wengi ni uaminifu. Kiongozi bora ni yule ambaye yuko tayari kusimamia muongozo wa katiba ya nchi au marufuku alizowekewa katika madaraka yake. Hii inakwenda sambamba na kutowaonea, kuwanyanyasa wa nchini yake kwa kutumia cheo chake.
Awe mkweli
Viongozi wengi hasa wa kisiasa siku hizi ni waongo hakuna mfano, wamejaa ahadi zisizotekelezeka na hata wanapogundua kuwa hawana uwezo au wamekwama kuzitimiza, hawaoni haja ya kutubu mbele ya wanaowaongoza. Kiongozi makini ni yule atayekuwa tayari kuonesha ubora wa matendo na kauli zake.
Asiwe mwenye majungu
Kuna baadhi ya viongozi kwenye maofisi wanaendekeza sana majungu na pengine kuyapa umuhimu wa hali ya juu. Hii ni sifa mbaya kwa kiongozi yo yote, hivyo anayetumikia ‘umbea’ katika ofisi aliyokabidhiwa kama mkuu anapaswa kuondolewa. Kiongozi makini atatumia uwezo wake kuzuia watu wasimsengenye/wasisengenyane kwa kuwa muwazi na mwenye kufungua milango ya watu kumuona na kumlaumu na kueleza hisia zao.
Awe bora
Kwa kila analofanya kama kiongozi lazima alifanye kwa ubora, asiwe mtu mwenye kulipua kazi na kufanya chini ya kiwango cha uwezo wake. Kila siku katika kazi, maamuzi, usimamizi, utekelezaji lazima atumike zaidi ya uwezo wake.