MUHTASARI WA MKUTANO WA WADAU WA FILAMU TANZANIA ULIOFANYIKA KATIKA VIWANJA VYA LEADERS – KINONDONI MJINI DAR ES SALAAM
15 AGOSTI 2012.
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Viongozi wa Vyama Wanachama wa Shirikisho la Filamu na Wadau wa Filamu nchini.
Napenda kuchukua fursa hii kwa kuwashukuru wote wale wote waliopata bahati ya kuhudhuria katika mkutano ule ambao kwetu ni mkutano wa kihistoria.
Sababu ya Kuwepo kwa Mkutano.
Mnamo siku ya tarehe 7 Agost 2012 majira ya saa 11 jioni Shirikisho la Filamu Tanzania , TAFF kwa ushirikiano wa pamoja na kampuni ya Usambazaji ya Steps Entertaiment, Watayarishaji wa Filamu wa kampuni za Jerusalem Production, Nice Entertainment , Chen Arts Creation , Nyerere the Power, CYG na Wasanii Waongozaji kwa Ushirikiano wa Jeshi la Polisi na ofisi za TRA Makao makuu. Tulifanikiwa kumkamata mtu ambaye inasadikiwa anadurufu kazi mbalimbali za Wasanii wa Filamu na muziki wa taarabu na injili.
Mfanyabiashara huyo haramu wa kazi Wasanii nchini Bwana Rigobert Masawe alikamatwa kwa kushirikiana na raia mwema ambao hawakuridhikia na faida anayopata kutokana na kufanya biashara haramu inayotokana na jasho la Wasanii.
Baada ya kufanikiwa kumkamata Mtuhumiwa huyo na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Shirikisho la Filamu – TAFF, iliitisha kikao cha dharura kwa Wasambazaji na Watayarishaji wa Filamu wote ili kwa pamoja kutafuta namna ya kulishughulikia jambo hili kwa haraka na kwa nguvu za Pamoja.
Katika kikao hicho kilichofanyika 08/08/2012 ambacho kilikuwa cha Mafanikio Watayarishaji na Wasambazaji wengi walihudhuria, baada ya majadiliano ya kina na yenye busara ambayo yalionesha ushirikiano mkubwa katika kutetea hali hii, Wajumbe walichangia mawazo mbalimbali na maazimio yalikuwa yafuatayo:
- Tufanye Mkutano na Waandishi wa Habari ili kuijulisha jamii na umma wa Watanzania kwamba jambo limezidi kuwa sugu na lisili la kificho na linafanyika wazi Bila ya woga.
- Kufanya matembezi ya kulaani kushamiri kwa wizi wa kazi za Sanaa Dhahiri
- Ili kuonesha kukerwa huko Wasanii na Wadau waliazimia kwamba kila mmoja awe askari kanzu kwa jambo hili kwa makusudi bila ya hivyo filamu zitakosa mauzo kama ilivyo kwa muziki hapa Tanzania kwa sasa.
Wajumbe pia walikubaliana kwamba mambo yote yafanywe chini ya mwavuli wa TAFF kwa sababu ndio muhimili wao.
Baada ya maazimio hayo iliundwa kamati ya kusimamia na kupanga mkakati wa namna ya kutekeleza mkubaliano hayo, kamati hiyo ilikuwa na Wajumbe wafuatao;
- Simoni Mwakifwamba Rais wa TAFF.
- Wilson Makubi Katibu Mtendaji wa TAFF.
- Steven Mengele (Nyerere)
- Simoni Mwapagata (Rado)
- Jackob Steven (J.B)
- Vincent Gibs (Gibs Media)
- Vincent Kigosi ( Ray)
- Issa Mussa (Cloud)
- Mahsein Awadhi (Dr Chen)
- Asha Baraka
Kamati ilikuwa na jukumu la kutafuta namna ya kufanikisha maazimio hayo na Kampuni za Usambazaji na Watayarishaji zilikuwa tayari kusaidia baadhi ya maeneo katika utekelezaji.
Mkutano na Waandishi
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo tarehe 10/08/2012 saa 5 mchana asubuhi kamati ilifanikisha kutekeleza jukumu la kuongea na waandishi wa habari kama maazimio yalivyopendekezwa. Mkutano ulifanyika katika Hotel ya Demagi Kinondoni ulikuwa na mafanikio makubwa kwa sababu wadau mbalimbali walihudhuria pamoja na Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotions Mh. Alex Msama aliweza kufika na aliipongeza TAFF kwa jitihada za makusudi iliyochukua kuokoa hali ambayo inatishia uhai wa kazi za Wasanii wa Filamu nchini kama ilivyo katika Muziki
Wazungumzaji wakuu katika mktano huo na Waandishi wa habari walikuwa ni Rais wa Shirikisho la Filamu na Mwenyekiti wa kundi la Bongo Movies.
Baada ya Mkutano na Waandshi wa Habari TAFF ilifanya kikao na Wasambazaji wote pamoja na kupitia chama cha Wasambazaji nchini TAFDA na ile kamati ya awali pamoja kutafakari kwa pamoja juu ya matembezi ya kulaani wizi wa kazi za wasanii kikao kilifanyika katika ofisi za TAFF zilizopo Magomeni.
Lakini pamoja na Wajumbe wa kikao cha kwanza kupitisha maazimio ya kufanya matembezi ya kulaani wizi bado Uongozi wa TAFF uliona kwamba hakuna ulazima sana wa kufanya Matembezi hayo kwa kuwa Serikali tayari imeonesha nia ya kusaidia tasnia hii na uzuri ni kwamba utekelezaji wake umeshaanza kupitia mpango wake wa urasimishaji Wajumbe wote walikubaliana na hoja hiyo.
Kutokana na hilo Shirikisho la Filamu ikaamua kusitisha suala la Matembezi badala yake likafanya mkutano wa Kulaani wizi wa kazi sanaa katika viwanja vya Leaders kwa makusudio na malengo yale yale yaliyoamuliwa katika kikao na Wanakamati. Wasambazaji waliohudhuria ni Steps Entertainment, PiliPili Entertainment, Whatever Production, Liro Promotion, Zito Entertainment, SSG Distribution, KAPICO, GMC, Papa Zii, Bajomba Production, Sas O entertainment, KIBIKI, Easy Media, Bornagain Film Production,Mega Video na Wengineo wengi.
Kwa kuona umuhimu wa hilo Wasamabazaji walipitisha azimio la kuchangia ili kufanikisha mkutano huo na jumla ya Tshs 1,300,000/= ziliahidiwa na kufanikisha mkutano huo.
Mkutano wa Kulaani Wizi wa Kazi za Sanaa
Mheshimiwa Waziri,
Napenda kukujulisha kwamba miezi miwili iliyopita kabla ya tukio hili kutokea Wadau mbalimbali wa tasnia ya Filamu na Muziki wameipongeza TAFF kwa muenendo wake mzuri katika kusimamia majukumu yake pamoja na mapungufu makubwa yaliyopo ikiwemo suala la tatizo la kifedha, lakini hawakusita kutushauri juu ya mgogoro wa kifikra uliopo kati ya TAFF na kundi la wasanii wa Bongo Movie, wengi walishauri kwamba ipo haja ya kufikia tamati kwa tatizo lenu sababu nafasi tuliyonayo kwa jamii ni kubwa sana. TAFF iliupokea ushauri huo ilikuwa inaufanyia kazi.
Mkutano wa Wadau Kulaani Wizi huo, ulifanyika tarehe 15 Agost 2012 kuanzia saa 6 mchana na kiukweli ni mkutano wa mafanikio kwa sababu pamoja na muda wa mkutano ulikuwa wa jua kali lakini wadau walijitokeza wengi sana.
Mada zilizozungumzwa katika mkutano huo ukiondoa mada kuu ya Kulaani Wizi wa kazi za Sanaa ni zifuatazo:
a. Nafasi ya Wadau wa Filamu katika Urasimishaji wa sanaa nchini
b. Umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wasanii
c. Umuhimu wa Wasanii katika mchakato mpya wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
d. Umoja na Maadili ya Wasanii na katika kazi zetu.
Wazungumzaji katika Mkutano huo Walikuwa ni
a. Rais wa Shirikisho
b. Mwenyekiti wa kundi la Bongo Movie
Mratibu Mkuu wa Mkutano huo walikuwa ni TAFF chini ya Usimamizi wa Katibu Mtendaji. Mkutano ulifunguliwa saa 6:00 na Mkurugenzi wa kampuni ya Papa Zi kwa kuwashukuru wadu wote wliohudhuria hapo pamoja na hali ya jua kuwa kali. Lakini pia aliwaomba wadau kwamba Jambo linalohusu umoja miongoni mwetu ni la muhimu sana kuliko wanavyofikiria kwa sababu bila ya kuwa na umoja mambo mengi hayatafanikiwa.
Mwenyekiti wa Bongo Movie
Mwenyekiti wa Kundi la Wasanii wa Bongo Movie Jackob Steven (J.B) alisema kwamba sasa ni wakati wa Wasanii kuamka , kujitambua na kuacha tofauti zetu ambazo kimsingi hazitusaidii kupiga hatua bali ni wakati wa kuungana ili kwa pamoja tuweze kumpiga adui yetu kwa nguvu ya pamoja.
Lakini pia aliupongeza uongozi wa TAFF kwa jitihada mbalimbali wanazofanya katika kushughulikia matatizo ya Wasanii, kuwatetea wasanii na mambo muhimu wanayopigania kwa niaba ya Wasanii wote hapa nchini.
J.B aliendelea kusema kuwa Wasanii tusipoonesha ushirikiano na mshikamano wa kweli maharamia wa kazi za filamu wataendelea kunufaika huku wenye haki tukiwa palepale kwa sababu za kuendekeza matatizo yasiyo na tija kwetu. Lakini pia alimuomba Rais wa Shirikisho la Filamu na Uongozi kwa ujumla walitazame suala la mgogoro wetu kwa sababu unachangia kutumaliza wenyewe na aliomba wakati umefika bifu hilo limalizike haraka iwezekanavyo kwa maslahi ya tasnia ya filamu na sanaa kwa ujumla na anamini kwamba hakuna atayeweza kutusuluhisha ikiwa sisi wenyewe hatuko tayari, wao kama Bongo Movie wana tamka wazi kwamba hawana tatizo na Uongozi wa Shirikisho na wanamtambua Rais wa Shirikisho na wako tayari kufanya kazi pamoja .
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kabla ya kuanza kuzungumzia ajenda kuhusu Mkutano huo aliwashukuru wadau wote waliohudhuria kwa sababu anaamini wametambua wajibu na ummuhimu wa Shirikisho la Filamu Tanzania.
Lakini pia alichukua fursa hiyo kujibu maelezo yaliyotolewa na J.B kuhusu mgogoro wa Bongo Movie dhidi ya TAFF, Kabla ya yote alimuomba Mwenyekiti wa Bongo Movie na viongozi wengine na Katibu wa Shirikisho na viongozi wengine wapande juu ya jukwaa.
Alisema kwamba anajisikia furaha na amani bila ya kutarajia kama J.B angetoa taarifa hiyo mbele ya umma wa Wadau wa Filamu Tanzania siku hiyo, lakini kwa niaba ya Kamati Kuu ya Shirikisho, Bodi ya Shirikisho la Filamu na Wanachama wote wa Shirikisho la Filamu Tanzania, alitamka wazi kwamba ikiwa Rais wa Shirikisho au Bodi ya Shirikisho na Wanachama waliwakosea Bongo Movie basi kwa niaba ya wote anaomba tusamehewe lakini pia alisema na ikiwa Bongo Movie waliwakosea TAFF pia kwa niaba ya uongozi mzima wa Shirikisho anatamka wazi kwamba tumewasamehe hivyo anaomba tuzike na kusahau tofauti zetu leo na tuanze upya.
Baada ya maelezo hayo ambayo yaliungwa mkono kwa wadau kupiga makofi kwa wingi sana Rais wa TAFF, Simoni Mwakifwamba alimkaribisha J.B naye alisema kwamba kwa niaba ya Uongozi wote wa Bongo Movie nao wamekubali msamaha uliotolewa na wao wamewasamehe wale wote walio wakosea katika mchakato wa mgogoro huo na ameomba tuanze upya mahusiano yetu kama ilivyo kuwa zamani wakati tunaanzisha TAFF na wako tayari kushirikiana na TAFF kwa lolote wataloagizwa kufanya na kuanzia leo wanamtambua Rais wa TAFF na uongozi wote kwa ujumla.
a. Nafasi ya Wasanii wa Filamu katika Urasimishaji wa sekta ya Sanaa
Rais wa TAFF alianza kwa kuishukuru serikali kwa kuweza kusikiliza kilio chetu ambacho kimedumu zaidi ya miaka 20 sasa, lakini pia aliishukuru serikali kwa kuifanya sanaa kuwa ni kazi rasmi ambayo itakuwa ni yenye mchango katika pato la Serikali moja kwa moja. Kwa hiyo aliwataka Wasanii wa filamu kuakikisha kuwa wanaitumia fursa ya urasimishaji huo kwa mambo yafuatayo:
i. Kuzalisha kazi bora zenye zitazokidhi viwango vya soko la ndani na soko la kimataifa na zenye maadili ii. Kuhakikisha kwamba kazi zote lazima ziwe zimezingatia sheria zote za utayarishaji wa filamu kwabla ya kupelekwa sokoni.
iii. Wasambazaji na Watayarishaji wahakikishe kwamba wanarekebisha mikataba yao kuwa ni yenye maslahi kwa Wasanii wote wanaofanya nao kazi.
iv. Kufichua Maharamia wa kazi za Wasanii ili kufichua uharamia wao.
b. Umuhimu wa Bima ya Afya
Rais wa TAFF alisema kwamba sasa wakati umefika muda wa Wasanii kujiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa lengo la kujiwekea akiba zitazo wasaidia katika matatizo ya afya zao, mikopo kwa ajili kuendeleza kazi zetu na mengineyo lakini alitumia fursa hiyo kusema kwamba NSSF wametaka TAFF kuingiza wanachama wake kuingia katika mfuko huo, majadiliano yanaendelea yatapo kamilika wadau watajulishwa kupitia vyama na makundi yao.
b. Ushiriki wa Wasanii wa Filamu katika Katiba Mpya na Sensa 2012
Rais aliwataka Wasanii wa Filamu wote kuhakikisha kuwa pale kamati ya Katiba itapowa fikia wahakikishe kuwa watajitokeza kwa wingi kwa ajili kutoa mapendekezo yetu kwa sababu ni jambo muhimu na limekuja kwa wakati muafaka kwa hiyo si jambo la kuzembea.Alisisitiza kwamba itakuwa ni aibu kwa vizazi vijavyo kwamba katika madiliko ya Katiba mpya ya nchi Wasanii wa Filamu hawakushiriki kutoa maoni yao, aliwaomba wajitokeze kwa wingi sana.
c. Umoja na Maadili kwa Wasanii
Umoja
Rais wa TAFF alisema kwamba katika umoja kwa kiasi Fulani tumeanza kufanikiwa kwa sababu ya Wasanii tumekuwa tukishirikiana katika matatizo mbalimbali lakini pia anapongeza tukio la kumaliza mgogoro uliokuwa kati ya Bongo Movie na TAFF kwa siku ya leo hivyo aliwataka wasanii kuwa wakweli na waaminifu miongoni mwetu. Mwisho aliwataka Wasanii kuhudhuria vikao mbalimbali vitavyoitishwa na vyama wanachama au Shirikisho kwa sababu ya kupata taarifa muhimu.
Maadili
Rais wa Shirikisho la Filamu, katika suala la maadili aliweka wazi kwamba Wasanii wa Filamu mbele ya jamii tumechafuka sana. Tusijione tuko sawa tunapokuwa wenyewe kwa wenyewe lakini mbele ya jamii hatusomeki vizuri. Katika hili anaomba wasanii wote tushirikiane kujilinda na tabia zetu kwa lengo la kuleta heshima mbele ya jamii. Lakini pia alisisitiza kwamba katika suala la maadili Shirikisho la Filamu halitamvumilia hata mmoja miongoni mwa wale wataojitokeza kutuchafua na atayejitokeza tutamshughulikia.ipasavyo.
d. Kukamatwa kwa Mharamia wa Kazi za Wasanii
Kama tulivyotangulia kusema hapo awali kwamba Bwana Masawe maarufu kwa jina la Msukuma alikamatwa nyumbani kwake ambapo pia anafanya ofisi kwa ajili ya kudurufu kazi mbalimbali za Wasanii. Kazi zilizokamatwa kwa haramia huyo ni filamu ya Hatia (Tino) , Glory of Ramadhani (Ray), muziki wa Taarabu Mpenzi Chokalte (Mzee Yusuph). Rais wa TAFF aliwataka wasanii wote ili kuonesha mshikamano wa kweli lazima tuhudhurie kwa wingi mahakamani bila ya kukosa pale kesi itapoanza kusikilizwa. Kuonekana mahakamani kutasaidia kudhihirisha machungu kwa wezi wa kazi zetu na endapo tusipojitokeza maana yake tumeridhika na maovu yanayofanywa na maharamia hawa. Lakini pia kampeni itakuwa endelevu ikiwa ni sehemu ya kutekeleza tamko na agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Gharib Billal alilolitoa Musoma katika Uzinduzi wa kanuni za sheria za filamu na michezo ya kuigiza mwaka 2011 mwezi Oktoba.
KUFUNGA MKUTANO
Harambee Maalumu
Baada ya taarifa ya Rais wa Shirikisho Bwana Simoni Mwakifwamba kumaliza kuzungumza Katibu wa Shirikisho la Filamu Bwana Wilson Makubi aliwashukuru wadau kwa kuhudhuria mkutano huo lakini pia wadau waliomba kufanyike harambee ya kuchangia gharama za kuendesha kesi hiyo. Wadau walikubali kuchangia na ilikuwa kama ifuatavyo:
a. Ahadi ya Usafiri kwenda mahakamani zilitolewa na kampuni zifuatazo;
i. Kampuni ya CYG chini ya Issa Mussa (Cloud )
ii. Kampuni ya Cheni Art Creation (Dr Cheni)
iii. Nice Entartainment (Mtunisi)
b. Ahadi ya Kuchangia Tshirt zenye ujumbe maalumu.
i. Tuesday Kihangalla fulana 100
ii. Dr Cheni fulana 50
iii. Chriss Creation Fulana 100
iv. Issa Mussa (Cloud) Fulana 200
v. Christian Promoters fulana 50.
Jumla ya Fulana ziliahidiwa kutolewa na wadau hao ni 500 Wasambazaji na Watayarishaji walipendekeza kwamba fulana hizo mara baada ya kukamilika zitauzwa kwa gharama ya shilingi 2000/= kila moja kuchangia gharama za uendeshaji wa Shirikisho la Filamu Tanzania.
Fedha Taslimu zilizochangwa zilikuwa ni Shilingi 75,000/= lakini pia wadau waliwachangia Mzee Kankaa na Mzee Small jumla ya shilingi 150,000/= ili ziwasaidie katika matibabu yao na matumizi kwa kuwa Wazee wetu hawa ni wagonjwa kwa muda mrefu sasa Mkutano ulifungwa saa 10 alasiri.
Ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh Dk Fenella Mkangara tunaomba achukue hatua za makusudi kuwaita viongozi watatu wa kila upande wa Shirikisho la Filamu Tanzania na Viongozi wa Bongo Movie kwa ajili ya kuhitimisha na kusawazisha zaidi maelewano hayo kuimarisha tasnia.
Muhtasari huu umepitiwa na:
SIMONI J. MWAKIFWAMBA - RAIS
WILSON R. MAKUBI - KATIBU MTENDAJI
TAREHE 18 AGOSTI 2012
Source: http://www.wavuti.com/#ixzz23v3iGISL