TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI KUFAFANUA KUHUSU MIRADI YA UTAFUTAJI NA UVUNAJI WA GESI
ASILIA NCHINI
1.0 UTANGULIZI
Wizara ya Nishati na Madini inapenda
kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi Asilia ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana
na wawekezaji katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa
yatakayopatikana kwa wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara
na Lindi.
Siku ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba
2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi
ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara, wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya
maandamano ya kudai raslimali ya Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na
kupinga mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar
es Salaam. Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa
Wa-Tanzania wote kwa kupitia vyombo vya habari.
Tokea Uhuru, uchumi wa Tanzania
umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile katani (Tanga na Morogoro),
pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa (Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na
Mara), chai (Iringa) na tumbaku (Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha
wakazi wa mikoa yote ya nchi yetu bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka
mikoa hiyo hawajawahi kufanya maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya
Wa-Tanzania wengine) wa aina yo yote ile.
1
Mapato yatokanayo na uchimbaji wa
dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Tabora), almasi (Shinyanga) na
tanzanite (Manyara) yamewanufaisha Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule!
Minofu ya samaki wa Ziwa Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia Taifa
letu fedha nyingi ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wo
wote.
Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha
mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote. Mahindi kutoka
Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu
bila kujali eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi
hayo ni kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na
Kagera inatumiwa na wakazi wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya mikoa
inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu
yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam bila manung’uniko yo yote kutoka kwa
wakazi wa eneo la chanzo cha Mto Ruvu.
Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na
Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro)
unatumiwa na wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya wenyeji wa
sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa. Kwa
hiyo, kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda
maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo yote ile
kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya Upinzani kupanga,
kuhamasisha, kushabikia na kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale
Mtwara Mjini.
2.0
RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA
Gesi Asilia ilianza kugundulika hapa
nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa cha Songo Songo, Mkoani Lindi. Baada ya
hapo Gesi Asilia imegundulika maeneo ya Mtwara Vijijini, yaani Mnazi Bay (1982)
na Ntorya (2012), Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha
Gesi Asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa Futi za
2
Ujazo Trilioni 4.5 – 8. Katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia
uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari. Kiasi cha Gesi Asilia
iliyogundulika katika kina kirefu cha maji inafikia takribani Futi za Ujazo
Trilioni 27. Kiasi cha wingi wa Gesi Asilia yote iliyogunduliwa nchi
kavu na baharini inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 35.
Kufuatana na Sheria za nchi yetu
zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa iliyopo kando kando mwa bahari (isivuke 12
nautical miles au 22.22 km kuingia baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi
sasa katika
Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14
tu ya gesi yote iliyogundulika nchini.
Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa yetu, Lindi
inayo 7% ya gesi yote, Pwani 1% na huku Kina Kirefu cha Bahari (Deep
Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%) kuliko mikoa yote ikiwekwa pamoja! Kwa
hiyo, hakukuwa na haja ya kufanya maandamano kwa sababu Gesi Asilia nyingi
inapatikana kwenye bahari ya kina kirefu ambayo iko ndani ya mipaka ya nchi
yetu bila kujali mipaka ya mikoa yetu. Isitoshe Gesi Asilia imegundiliwa kwenye
miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa Miaka kati ya Milioni 199.6
hadi 23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa yetu
haikuwepo wakati huo!
Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia
pia unaendelea tukiwa wa mategemeo makubwa ya upatikanaji wa raslimali hizi
katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe,
Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora pamoja na kwenye kina kirefu cha maji
baharini kuanzia mpaka wetu na Msumbiji hadi mpaka wetu na Kenya. Hatutarajii
mikoa hii nayo ifanye maandamano ya kutaka kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na
Mafuta zitakapogunduliwa mikoani mwao.
3.0
MATUMIZI
YA GESI ASILIA YA MNAZI BAY (MTWARA) NA SONGO SONGO (LINDI)
Mpaka
hivi sasa Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka Mnazi Bay
(Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi
3
Bay kwa sasa huzalisha umeme kwa
ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu. Mitambo ya kufua umeme kutokana na Gesi
Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao uwezo wa kuzalisha MW 18 lakini
matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na Lindi haijavuka MW 12. Umeme huo
wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni za Wentworth na Maurel & Prom
zikizalisha Gesi Asilia (inayotumiwa na TANESCO) kiasi cha Futi za Ujazo
Milioni 2 kwa siku. Ikumbukwe kwamba ufuaji wa umeme wa hapo Mtwara
Mjini ulikuwa mikononi mwa Kampuni ya Artumas iliyofilisika. Tangu Desemba
2006 hadi leo hii kiasi cha gesi kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya
mikoa hiyo miwili ni chini ya asilimia 1 ya gesi yote iliyogundulika
Mnazi Bay (Mtwara Vijijini). Vilevile ikumbukwe kwamba kuna visima
vinne vya Gesi Asilia pale Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na kinachotumika kwa
sasa na tena kwa kiwango cha chini kabisa ni kimoja tu!
Aidha ni vizuri ndugu zangu
Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii inatafutwa na kuchimbwa na
wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wataalamu na teknolojia ya utafutaji na
uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa kurejesha mitaji yao. Uchorangaji wa
kisima kimoja cha utafutaji wa Gesi Asilia nchi kavu unahitaji Dola za
Marekani Milioni 40, na kwenye kina kirefu cha maji baharini
zinahitajika zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100. Ikumbukwe kwamba,
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Tanzania (TPDC),
inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa shughuli za kuvutia, kuratibu
na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia nchini kote ikiwemo Mikoa
ya Mtwara na Lindi. Walipa kodi Wa-Tanzania bado hawajalalamika wala
hawajafanya maandamano ya kudai fedha zao za kodi zisitumike huko Mtwara!
Ni muhimu pia tukaelewa kwamba Gesi
Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) inazalisha umeme peke yake kwa ajili
ya Mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi Asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) ndiyo
inayotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya Gridi ya Taifa, na pia kwa ajili ya
wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga
4
Fungu (Lindi) na viwandani (Dar Es
Salaam). Tangu Oktoba 2004 ambapo mitambo ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi
leo hii, kiasi cha Gesi Asilia ya Songo Songo kilichotumika ni asilimia 7 tu
ya Gesi Asilia yote iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba
hata uchumi wa Jiji la Dar Es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha Gesi Asilia
(7%) iliyopo Songo Songo (Kilwa, Lindi). Ikumbukwe kwamba waajiriwa
kwenye viwanda vya Dar Es Salaam wamo wanyeji wa kutoka Mtwara Mjini ambako
maandamano yalifanyika na vilevile wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa Vyama
vya Siasa vya Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano ya Mtwara
Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
4.0
MIPANGO
YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5 HADI 10
(a) Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam:
Kuuza
Gesi Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80% ya mapato
ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa ki-uchumi. Tayari
kuna viwanda
34
vinatumia Gesi Asilia ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo gesi zaidi
itapatikana. Soko kubwa la Gesi Asilia lipo tayari Dar es Salaam (na siyo
Mtwara), ambapo ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta. Serikali
inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia
kila siku. Takribani Dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Shilingi
Trilioni 1.6) kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini
ikifua umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei
kubwa sana. Bei ya umeme kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa kutumia
dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya Senti za Marekani 30 hadi 45
na huku bei ya uniti moja hiyo hiyo ni Senti za Marekani 6-8 kwa umeme
utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi.
Vilevile,
takribani Dola za Marekani millioni 202 kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji
la Dar Es Salaam litatumia Gesi Asilia badala ya mafuta katika magari, taasisi
na majumbani. Fedha
5
hizi
zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa manufaa ya
Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale walioratibu maandamo ya
Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na
Gesi Asilia:
Bomba la Gesi Asilia linalojengwa litasafirisha gesi
nyingi zaidi ambayo itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es
Salaam) kufua umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia Somanga Fungu
(Lindi) wa kiasi kisichopungua MW 520.
(c)
Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu:
Dar
es Salaam ndiko kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme
kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi unaotulazimisha
kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka Dar Es
Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa moja viwandani,
majumbani na kwenye magari.
(d) Kwa
kuzingatia mahitaji ya
Gesi Asilia yatakayojitokeza:
Bomba
la kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off)
katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji hii
inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika. Kwa hiyo kuweka
mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye Bomba la Gesi Asilia linalojengwa
kutarahisisha matumizi ya Gesi Asilia viwandani na majumbani katika Mikoa ya
Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine kwa siku za baadae.
(e)Serikali imetenga
maeneo katika pwani ya Mikoa
ya Kusini
(Lindi
na Mtwara) kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda (Industrial
Parks/Estates) vikiwemo viwanda vya mbolea, Liquefied Natural Gas
(LNG) na Petrochemicals.
Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko
katika hatua za mwisho za maandalizi.
(f) Ili kutengeneza mazingira mazuri ya
biashara ya Gesi Asilia na Mafuta kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea
kazi, Serikali imetenga eneo maalumu Mtwara, ambalo litawekewa
6
miundombinu ya msingi ili kutoa
vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda
Huru wa
Bandari (Freeport Zone).
Ni lazima shughuli za kusafisha na
kusafirisha Gesi Asilia zitatoa ajira katika maeneo husika. Kwa mfano kwa
mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo
(Kilwa, Lindi), kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya
Lindi na Mtwara.
Watanzania wanakumbushwa kuwa
raslimali zilizopo nchini ikiwemo gesi asilia, madini, makaa ya mawe, wanyama
pori, misitu, milima ya utalii, mito, maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raslimali hizi
zinapatikana, zinatunzwa na kuzalishwa maeneo mbalimbali nchini mwetu na mapato
yake yanatumika kwa maendeleo ya Wa-Tanzania wote bila kujali maeneo
raslimali hizo zilipo.
Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande
vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali
kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu.
Tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo
kwenye tarafa zetu. Tusikubali kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha
raslimali zilizopo kwenye kata zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa
kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU
Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)
WAZIRI YA NISHATI NA MADINI