KATIBU wa Bunge Dk. Thomas Kashililah ametoa ufafanuzi kuwa mbunge wa Bahi, Omar Badweli anayetuhumiwa kwa rushwa ataendele kuwa mbunge hata kama atahukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita jela.
Dk. Kashililah alisema hayo jana alipozungumza kwa njia ya simu alisema kuwa mbunge huyo bado ni mtuhumiwa na pia kwa mujibu wa katiba atakoma kuwa mbunge kama atahukumiwa kifungo cha kuanzia miezi sita jela.
Amesema hayo baada ya mbunge huyo Badwel kufunguliwa kesi mahakamani ya tuhuma ya kuomba rushwa ya sh. milioni nane toka halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, Pwani.
Dk. Kashililah alitoa mfano wa mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi ambaye hivi karibuni mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno kwa kukusudia na kumuhukumu kwenda jela miezi 10 au kulipa faini ya Sh. 500,000.
Hata hivyo Kilufi alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na mahakama ya Mbeya.
Alisema hata kama Badwel atafungwa kifungo cha chini ya miezi sita kwa mujibu wa katiba ataendelea kuwa mbunge atakapokuwa amemaliza kifungo chake hicho.
"Kwa sasa Badwel ni mbunge halali kwani hayo aliyonayo ni tuhuma tu na hatuwezi sisi kama Bunge kumuondoa mpaka ithibitishwe na vyombo husika. Ubunge wake utakoma tu endapo atafungwa zaidi ya miezi sita na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kila mtu ana haki mbele ya sheria anaweza akajitetea na akawa huru, sasa kama umeshamfukuza utafanyaje ni lazima tusubiri," alifafanua Dk. Kashililah.