Pages

Monday, October 22, 2012

Bandari Dar Mabingwa Inter-Ports Games


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mh. Baraka Konisaga akikabidhi kikombe cha ushindi wa kwanza kwa mwakilishi wa washindi wa kwanza wa mpira wa kikapu, Kisanta kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania mara baada kukamilika kwa michezo ya inter-ports iliyofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mh. Baraka Konisaga akikabidhi kikombe cha ushindi kwanza wa michezo ya inter-ports, kapteni wa timu ya mpira wa pete, Judith Ilunda kutoka Bandari ya Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mh. Baraka Konisaga akikabidhi kikombe cha ushindi kwanza wa michezo ya inter-ports, kapteni wa timu ya mpira wa miguu, Vitalis Salila wa Bandari ya Dar es Salaam.
---
Na Mwaandishi Wetu
Bandari ya Dar es Salaam imeibuka na ushindi wa jumla katika michezo ya inter-ports games ambayo imefanyika jijini Mwanza hivi karibuni na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mh. Baraka Konisaga.

Michezo hiyo imefanyika jijini huko kwa muda wa siku tano ambapo zaidi ya wanamichezo 400 wafanyakazi wa Bandari walishiriki michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, pete, kikapu, riadha, bao na kuvuta kamba.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vikombe na zawadi nyingine kwa wanamichezo hao, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana aliwaasa wanabandari kuendelea kushiriki michezo kwa ajili ya kujenga afya zao lakini kubwa zaidi kutekeleza majukumu yao ya kila siiku kwa ufanisi.
“Leo isiwe mwisho wa kushiriki michezo endeleeni kushiriki ili kuoboresha afya zenu lakini pia niwashauri kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na mkumbuke kwamba mmepewa dhamana kubwa na taifa lenu hivyo ni wajibu wenu kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa,” amesema Konisaga.

Katika michezo hiyo Bandari ya Dar es Salaam iliibuka na vikombe vingi zaidi ambapo katika mpira wa soka waliibuka washindi wa kwanza kwa kujinyakulia alama nyingi huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Makao Makuu.

Kwa upande wa mpira wa pete mshindi ni Bandari ya Dar es Salaam na nafasi ya pili ilinyakuliwa na Bandari ya Tanga. Katika mchezo wa kikapu nafasi ya kwanza ilikwenda Makao Makuu wakati Bandari Tanga wakinyakua nafasi ya pili.

Nafasi ya kwanza ya mchezo wa kuvuta kamba wanaume ilikwenda kwa Bandari ya Dar es Salaam na nafasi ya pili ilinyakuliwa na Bandari ya Tanga.   Mchezo wa kamba wanawake nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga ilishika nafasi ya pili.
Kwa upande wa riadha Bandari ya Dar es Salaam iliibuka tena kidedea huku Bandari ya Tanga ikishika nafasi ya pili. Kwa upande wa wakimbiaji mita mia moja kwa wanawake medali ya dhahabu ilikwenda kwa mkimbiaji kutoka Makao Makuu, medali ya fedha ilikwenda kwa mkimbiaji wa Bandari ya Tanga na mshindi wa tatu alikuwa mkibiaji kutoka Bandari ya Dar es Salaam aliyeibuka na medali ya shaba.

Kwa upande wa wakimbiaji wa mita mia moja wanaume medali ya dhahabu ilichukuliwa na mkimbiaji wa Bandari ya Dar es Salaam, fedha mkimbiaji wa Bandari ya Dar es Salaam na shaba ilikwenda kwa mkimbiaji kutoka Bandari za Maziwa (Mwanza, Kigoma na Kyela).
Kwa upande wa mita mia nne wanawake dhabau ilikwenda Bandari ya Dar es Salaam, fedha ilikwenda Bandari ya Dar es Salaam na shaba ilikwenda kwa mkimbiaji wa Makao Makuu. Kwa upande wa mita mia nne wanaume dhahabu ilikwenda Tanga, fedha ilikwenda Makao Makuu na shaba ilinyakuliwa na Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa mchezo mkongwe na wa jadi maarufu kama bao, Bandari ya Dar es Salaam iliibuka tena na ushindi wakati nafasi ya pili ilikwenda kwa Bandari ya Tanga. Kwa upande wa wachezaji bora wa kila mchezo, mlinda mlango mahiri wa timu ya Mtwara, Douglas Bahati aliibuka mshindi.

Kwa upande wa mchezo wa mpira wa pete, Matalena Mhagama ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa aliibuka kidedea na nafasi ya kwanza. Kwa upande wa timu bora ya kuvuta kamba Makao Makuu waliibuka na ushindi huku Bandari ya Mtwara ikiibuka na ushindi wa timu bora ya kuvuta kamba wanaume.

Mchezaji bora wa riadha ni Lucy Kyoma kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Bandari zilizoshiriki katika michezo hiyo ni pamoja na Bandari Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kyela, Kigoma na Makao Makuu yenyewe. Michezo hiyo hufanyika mara moja kila mwaka kwa kuwashirikisha wanabandari na hufanyika mara moja kwa kila kituo.

-mwisho-

Popular Posts