Pages

Monday, October 22, 2012

(CHADEMA)Chaelezea vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala na Zanzibar


 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabele Marando akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam juzi juu ya matukio makubwa yaliyotokea nchini Tanzania yakiwemo yale ya kuchomwa kwa makanisa, maandamano ya wafuasi wa dini ya Kiislamu pamoja na tukio la kutoweka kwa Sheikh Farid wa Zanzibar ambaye kwa sasa amepatikana akiwa hai.
  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
---
IMEELEZWA kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni ni matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la Dar es Salaam wiki hii.
 
Marando alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo kushughulikia matatizo yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha Waislamu wengi wenye msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi kutotawalika.
 
“Kabla ya uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU, kwa ajili ya kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua kuwawekea Waislamu Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue matatizo ya Waislamu wote hayasimamiwi na Bakwata, waitwe Waislamu na waulizwe shida zao,” alisema Marando.
 
Aliongeza kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini walikuwa wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko yoyote, hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa kutoka katika mikono ya wakoloni.
Alisema serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na makundi yote kutafuta muafaka.
 
“Siamini kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo wa serikali unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa, hawasikilizwi hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji Marando.
 
Akizungumzia utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema serikali haiwezi kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa Ikulu kuwa hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.
 
“Sheikh Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu la serikali kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya ulinzi vikisema havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni majibu kama yale yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.
 
Kwa upande wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa serikali imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.
 
“Jeshi la Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka ya Bunge,” alisema Safari.
Aliongeza kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro baina ya Waislamu na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.

Popular Posts