Pages

Sunday, August 12, 2012

Tamko la Prof. Shivji kuhusu habari ya "Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe"

JUU YA MUUNGANO: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimeshitushwa na gazeti moja la kila siku (Tanzania Daima la tarehe7 Agosti 2012) lilonipandikizia maneno katika kichwa chake cha habari kwamba ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’. Siwezi nikamsemea Dr. Lwaitama lakini kwa upande wangu sijasema wala kumaanisha kwamba ‘Muungano uvunjwe’.

Mosi, kwamba wasomi, wakiwemo wanahabari, wana jukumu zito la kutokupinda ukweli wa kihistoria kwa lengo la kuhalalisha mtazamo na msimamo wao kuhusu Muungano. Nikatoa mfano wa jinsi Merehemu Sheikh Karume anavyodekezwa katika msimamo wake juu ya Muungano. Wasemaji hapa bara wanamsifu kwa kuwa muasisi mwaminifu na mshabiki mkubwa wa Muungano tangu mwanzo. Huko Zanzibar, wasemaji hawachoki kumnukuu Mzee Karume kuwa tangu mwanzo yeye hakutaka Muungano isipokuwa alikuwa anafikiria Shirikisho.

Wanaendelea kusema kwamba aliposaini Mkataba wa Muungano, Mzee Karume alifikiri kwamba anasaini Shirikisho la Serikali tatu, lakini kutokana na kiwango cha elimu yake hakuelewa vizuri mantiki na maana ya alichokuwa anasaini.

Nikaendelea kueleza kwamba maelezo haya yote mawili hayaungwi mkono na ushahidi wa kihistoria. Ukweli ni kwamba, Mzee Karume aliingia katika Muungano kutokana na hesabu zake mwenyewe za kisiasa. Muungano kwake ulikuwa njia ya kuondoa upinzani, au upinzani tarajiwa, wa utawala wake. Yaani ilikuwa ni tendo la mwanasiasa yeyote yule kudumisha utawala wake (political survival).

Na kwa watawala wote wa Zanzibar waliomfuata, wakiwemo wa upinzani, ndivyo ilivyokuwa. Wamekuwa wakitumia mwavuli wa muungano wakati utawala wao uko hatarini na kushawishi wananchi wao dhidi ya muungano wakitafuta umaarufu wa kisiasa.

Nikitoa mfano nikasema kwamba kuna taarifa kwamba chama kimoja huko Zanzibar kinapandikiza pendekezo la ‘muungano wa mkataba, sio wa katiba’ bila ya kueleza waziwazi maana yake. Ukweli ni kwamba huwezi ukawa na muungano wa mkataba bila kwanza kuuvunja muungano. Kwa hivyo, wanachoshawishi moja kwa moja ni kuuvunja muungano. Basi waseme hivyo badala ya kujificha nyuma ya pazia la ‘muungano wa mkataba’.

Jambo la pili nililorudia ni kwamba tuliangalie suala zima la muungano kwa mtazamo na maslahi na matakwa ya Umma wa Zanzibar na Umma wa Tanzania bara, hususan matabaka ya hali ya chini. Katika hali yao kimaisha – kiuchumi na kisiasa – hakuna tofauti kati ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania bara. Uduni wa hali yao ni uleule; ukosefu wa ajira ni uleule; kutokuwa na mfumo wa dhati wa demokrasia unaojali walalahoi ni kulekule.

Kwa hivyo, umuhimu kwao ni mshikamano wao kuboresha mifumo ya uchumi na siasa. Wasiburuzwe na wanasiasa na vyama vyao kwa maslahi yao binafsi ya muda mfupi ya kudumisha, au kuingia kwenye, utawala.

Jambo la mwisho nililogusia ni kwamba kiini cha suala la muungano si idadi ya serikali (mbili au tatu) bali ni mgawanyo wa madaraka (distribution of power) kati ya dola la Zanzibar na dola la Muungano. Na katika hili kila muungano duniani ni wa kipekee kutokana na hali halisi yao ya kihistoria na uwiano wa kisiasa. Sisi pia tukiwashirikisha wananchi kikamilifu na tukaelewa vizuri matakwa yao tunaweza kubuni muundo wetu wa muungao ambao ni wa kipekee bila kujali idadi ya serikali.

Nimeona niweke wazi mtazamo wangu kwa sababu ya baadhi ya vyombo vya habari kuwa na hulka ya kupotosha mambo kutokana na ushabiki wao bila kujali madhara yanayoweza kutokea.

Mwishoni ningependa kusema kwa dhati kwamba uvunjaji wa muungano hauwezi kuwa kwa manufaa ya walio wengi. Ukweli ni kwamba unaweza ukasambaratisha nchi na jamii zetu pande zote mbili za muungano. Tukianza kubaguana kati ya Watanganyika na Wazanzibari, tutaendelea kubaguana kwa msingi wa Uislamu na Ukristo, na Usukuma na Uchaga, Uarabu na Uafrika, weusi na weupe bila kikomo.

Kama alivyosema Mwalimu, ukishaonja nyama ya mtu basi utaendelea kumtafuna.

Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Agosti 8, 2012

Popular Posts