Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya Kiislamu (JUMIKI) imepinga uvumi uliosambazwa nchini kuwa jana kungekua na maandamano ya Jumuiya hiyo na kudai kuwa propaganda hizo zinaendeshwa na baadhi ya watendaji katika jeshi la polisi na usalama wa taifa ambao hawaitakii mema Jumuiya yao.
Hayo yamesemwa na Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Ahmed wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo ZanzĂbar kuhusiana na tuhuma ambazo wamezitoa kwa Jeshi la Polisi dhidi ya Jumuiya yao.
Amedai kuwa Jumuiya haijapanga maandamano kwani ni taasisi inayofanya kazi zake kisheria nakwamba hata ikitokezea kufanya maandamano basi watafuata taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaarifu rasmi Jeshi la Polisi.
Aidha amedai kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kutaka kuwabatiza viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kesi za ugaidi hususan Amir Mkuu wa jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikh Farid Hadi Ahmed ili kuzima vuguvugu la kudai Zanzibar huru.
Shekh Faridi amedai kuwa inasemekana kuna mahusiano makubwa baina ya watendaji ndani ya Jeshi la polisi pamoja na baadhi ya wageni wanaosadikiwa kuwa ni raia wa Marekani juu ya kuutekeleza mkakati huo baada ya kuwa tayari umeshakamilika.
Amedai kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia ambao umekuwa ukifanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kuwanyima haki ya kufanya mihadhara yao ndani ya Misikiti ambapo Juni 17 mwaka huu wananchi mbalimbali walijeruhiwa kwa mabomu katika vijiji vya Donge,Mkwajuni na Mahonda.
Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi zake za kulinda usalama wa wananchi na mali zao na kuacha kufanya kinyume chake kwani huko ni kuchochea chuki kati ya Jeshi hilo na raia.
Amesisitiza haja ya wazanzibari kuungana na kuachana na Itikadi zao za kivyama katika kudai hadhi ya Rais na mamlaka ya Nchi ya Zanzibar ndani na nje ya Zanzibar pale tume ya mabadiliko ya Katiba itakapoanza kazi zake.
Kwa upande wake Naibu Naibu Amir Jumuiya Ya Uamsho Na Mihadhara Ya Kiisilam Sheikh, Azan Khalid Hamdan amewaomba wanahabari nao kuwa makini katika taaluma yao kwa kufanya usawa wa taarifa ambazo wamekuwa wakizitoa.
Hivi karibuni Jumuiya hiyo ilitangaza rasmi kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadili msimamo wao wa awali wa kuisusia Tume hiyo.
MWISHO.
IMETOLEWA NA
HABARI MAELEZO ZANZIBAR