Pages

Sunday, June 24, 2012

Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki Atoa Wito Kwa Wanananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam Kujitokeza Kwa Wingi Kuulaki Mwenge Wa Uhuru

Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaowasili jijini Dar es Salaam wiki ijayo ukitokea Mkoa wa Kusini Pemba. Pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa wanananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge huo.
-----
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaowasili jijini Dar es salaam siku ya jumatatu ukitokea mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utakabidhiwwa kwa uongozi wa wilaya ya Temeke saa 4 asubuhi na kuanza mbio zake ukipita katika wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam kwa muda wa siku 3.
Amesema mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu zinaongozwa na Kauli Mbiu ya Shiriki Kikamilifu Katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na Mapambano dhidi ya Rushwa, Ukimwi na Dawa za kulevya.
Ameto wito kwa waajiri na wakuu wa taasisi zote za Serikali kushiriki kikamilifu katika maeneo yao ya kazi kuulaki Mwenge huo.
Aidha katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ametoa msimamo wa mkoa wa Dar es salaam kuhusu mgomo wa madaktari kwa kuwataka madaktari hao kusitisha mgomo wao na kutoa huduma kwa wananchi kama kawaida.
Amesema kufuatia Chama cha Madaktari nchini (MAT) kutangaza kuanza mgomo wa madaktari nchi nzima mkoa wa Dar es Salaam umefuatilia kwa karibu mgomo huo na kubaini kuwa hospitali zote za Serikali za mkoa huo zimeendelea kutoa huduma kwa wananchi kama kawaida.
Bw. Meck Sadiki ameeleza kuwa hakuna taarifa zozote za kugoma kwa madaktari waliopangiwa zamu katika hospitali za Mwananyamala, Kinondoni na Temeke na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“ Ninachukua fursa hii kuwapongeza madaktari wote wa hospitali za Serikkali za mkoa wa Dar es salaam waliooendelea kutoa huduma kama kawaida licha kutangazwa kwa mgomo kwa kuonyesha nia ya kugoma na kutii sheria”. Amesema.
Amewataka wale wote wanaoendesha mikutano ya kuhamasisha migomo ndani ya maeneo ya hospitali za serikali kuacha mara moja huku akisisitiza kuwa serikali haitawavumilia na watakaobainika watachuliwa hatua za kisheria.
“ Ninatoa angalizo kwa wale wote wanaopenyeza mikutano ndani ya maeneo ya hospitali za serikali waache mara moja kwa sababu majengo yale ni kwa ajili ya matumizi ya huduma za afya tu”
Ameongeza kuwa tayari suala la mgomo wa madaktari liko katika vyombo vya sheria na kufafanua kuwa tayari mahakama ya kazi imeshabainisha wazi kuwa mgomo wa madaktari ni batili.
“ Kwa bahati nzuri suala hili limepata nguvu kisheria kwa kuwa mahakama imeshabainisha wazi kuwa mgomo wa madaktari hao kuwa ni batili na kwa yeyote yule atakekutwa ndani ya maeneo ya hospitali akiendesha mikutano sheria itafuata mkondo wake” amesema.
Aidha mkuu wa mkoa huyo amebainisha kuwa maeneo yote ya hospitali ni maeneo ya kutolea huduma za afya kwa wananchi na si mahala pa kuhamasisha mikutano ya kisiasa na kutoa onyo kwa vikundi vyote vinavyojiita vikundi vya wanaharakati kutopenyeza harakati zao katika maeneo hayo
Na.
Adrophina Ndyeikiza na Aron Msigwa
– Ofisi ya RC -DSM

Popular Posts