Pages

Sunday, July 29, 2012

TAARIFA YA MWENYEKITI KWA VYOMBO VYA HABARI KUFUATIA AJALI YA KUZAMA MV SKAGIT

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT YA KAMPUNI YA SEAGUL NA MAAFA YA ABIRIA WALIOZAMA NA KUFAMAJI ILIYOTOKEA TEREHE 18/08/2012
1. CUF – Chama cha Wananchi tumepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa sana taarifa ya kuzama kwa meli Mv. Skagit iliyotokea Jumatano mchana, Julai 18, 2012 katika bahari ya Hindi, ambapo inahofiwa watu zaidi ya 100 wamefariki. Kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Wanachama na wapenzi wa CUF, na kwa kweli kwa Watanzania kwa ujumla tunatoa pole kwa familia, ndugu, marafiki wa wafiwa, Wazanzibari na Watanzania wote kwa msiba wa kitaifa uliotokea kabla hata mwaka mmoja haujapita baada ya meli ya Mv. Spice Islander kuzama katika mkondo wa Nungwi Septemba 10, 2011 na watu zaidi ya 200 kupoteza maisha.

2. Mnamo tarehe 18/07/2012 kiasi cha saa 5:00 asubuhi meli ya Mv. Skagit inayomilikiwa na kampuni ya SEAGUL iliyosajiliwa Zanzibar iliondoka Dar es Salaam ikiwa na kiasi cha abiria 290 wakiwemo watoto wadogo wanaofika 40. Mpaka tunaandika taarifa hii idadi ya abiria waliookolewa imeripotiwa kufikia 145 na maiti waliopatikana ni 68.

3. Wakati meli hiyo inaondoka Dar es Salaam, hali ya hewa haikuwa nzuri sana. Hata hivyo iliendelea na safari na ilipofika eneo la Chumbe umbali wa nautical miles 3 kutoka katika kisiwa cha Chumbe meli hiyo ilipigwa na dhoruba kali jambo lililosababisha ilale ubavu kwa muda mfupi sana na baadae kugeuka kabisa juu chini, chini juu. Hali hii ilisababishwa na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na upepo mkali.

4. Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza Meli ya Mv. Skagit ilitengenezwa mwaka 1989 na kufanya kazi Seattle, Jimbo la Washington, Marekani. Iliachishwa kufanya kazi mwaka 2006. Hatimaye kuuzwa na kuletwa Tanzania. Inasemekana ilifanyiwa marekebisho Mombasa na kuongezwa urefu. Kuongeza urefu kuliifanya isiwe thabiti (stable) hasa abiria na mizigo ikiwa juu. Ilianza kufanya kazi Oktoba 2011. Kuna taarifa kuwa ilikuwa inayumba sana wakati wa safari ya kutoka Unguja kwenda Pemba na ilisimamishwa kufanya safari hizo.

5. Taarifa ya kupoteza muelekeo na kuzama meli hiyo iliripotiwa kwa Control Tower, Zanzibar na Dar es Salaam kabla ya meli hiyo kuzama. Aidha nahodha wa meli hiyo aliomba msaada kutoka kwa Control Tower pamoja na Harbour Master. Hata hivyo msaada wa uokozi ulishindikana kwenda kwa haraka kutokana na vyombo vilivyokuwepo bandarini kukosa mafuta.

6. Zoezi la uokozi lilikuwa gumu sana kutokana na sababu zifuatazo kwa sababu ya hali mbaya ya bahari na upepo mkali ilisababisha zoezi la uokozi kuwa gumu sana. Waokozi hawakuwa na taaluma ya uokozi kwani wengi wao walikuwa ni raia wa kawaida na vyombo vilivyotumika katika zoezi la uokozi vilikuwa ni vya kiraia ambavyo havikuwa na uwezo mzuri wa kuokoa. Na kwa sababu hiyo waokoaji walishindwa kuifikia na kuifunga mipira meli hiyo ili kuizuia isiendelee kuzama.

7. Pamoja na Tume ya Maafa na Mwenyekiti wake kufika katika eneo la tukio haikuweza kutoa msaada wa kutosha kutokana na kuwa haikuwa na wataalamu wa masuala ya maafa. Aidha katika zoezi hilo hakukuwa na Kikosi cha Uokozi na kamanda wake jambo ambalo lilikuwa dosari kubwa na kusababisha zoezi hilo kukosa muongozo.

8. Vikosi vya ulinzi vilikosa kutimiza wajibu wao kwa wakati. Kwa mfano kikosi cha KMKM kilifika katika eneo la tukio saa 12 jioni wakati kikosi cha wanamaji cha JWTZ kilifika katika eneo la tukio siku ya pili yake. Jambo hili limepelekea watu wengi kukosa msaada wa kuokolewa.

9. Kikosi cha Wanamaji cha JWTZ kilipaswa kuwa na jukumu la uokozi wa meli hiyo lakini hata hivyo halikufanyika mapema kutokana na kutokuwepo na kikosi imara cha dharura (standby unit) pamoja na kukosa vifaa vya kutosha vya uokozi kama vile rubber boats na fibre boats. Badala yake vifaa hivi vilifika katika eneo la tukio na kuanza kutumika siku ya pili yake wakati watu tayari wameshafariki.

10. Tatizo la kushindikana kuizuia meli isiendelee kuzama na hivyo kukosekana kuokolewa abiria lilitokana na uwezo mdogo wa uokozi waliokuwa nao waokozi waliofika katika eneo la tukio. Tuna vikosi vya baharini alau vitatu:- Kikosi cha Wanamaji cha JWTZ (Navy), Jeshi la Polisi la Wanamaji (Marine Police) na KMKM vyote havikufika mapema na kuwa na uwezo wa kuokoa abiria.

11. Kukosekana kwa mawasiliano baina ya Chombo kinachosimamia hali hewa na Chombo kinachosimamia usafirishaji, kwa ajili ya kupeana tahadhari itakayopelekea ikibidi vyombo kuzuiwa kutosafiri kwa siku husika visimamishwe, hususani vyombo vyenye uwezo mdogo wa kukabiliana na misukosuko ya mchafuko wa bahari.

12. Tuna wasiwasi na uwezo wa manahodha na mabaharia katika kujua uwezo wa chombo chao kama kinaweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa siku husika, na pengine hata SUMATRA na Wakala wa Meli Zanzibar (ZMA) haina sifa sahihi za manahodha na mabaharia hawa, na pia hakuna uhakiki ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa usalama wa chombo na abiria.

13. Nchi yetu ina mapungufu makubwa sana katika Kitengo cha Taifa cha Uokoaji, hawana vituo vya uhakika vya ukoaji, hawana zana na vyombo vya kisasa vinavyokwenda na wakati, lakini pia hawapati mafunzo sitahiki yanayokwenda na wakati katika uokoaji, kiasi ya kutegemea kuomba msaada wa uokoaji na zana kutoka Afrika Kusini pindi maafa yatokeapo, kama ilivyotokea wakati wa kuzama meli ya Mv. Bukoba Mei 21, 1996 katika ziwa Viktoria na meli ya Mv. Spice Islander katika mkondo wa Nungwi Septemba 10, 2012

14. CUF – Chama cha Wananchi tunaitaka Serikali iangalie upya uwajibikaji, utendaji na mwenendo wa SUMATRA, kwani imeshindwa kuwajibika ipasavyo. Kuwepo na chombo cha uhakika cha kusimamia usalama wa usafirishaji, kwa kuhakisha vyombo vinavyopasishwa kwa usafirishaji vinauwezo wa kukabiliana na machafuko ya hali ya hewa. Kuhakikisha vyombo vyote vinabeba abiria na mizigo kulingana na uwezo wa ujazo wa chombo husika.

15. Ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo na mawasiliano kati ya Kituo cha Hali ya Hewa na Chombo cha kusimamia usafirishaji ili kuwepo na TAHADHARI pindi itokeapo mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kuleta na kusababisha maafa kama ambavyo inavyofanyika kwa usafirishaji wa anga.

16. Vyombo vya Uokoaji vipewe mafunzo ya kisasa na vyombo/zana za kisasa za uokoaji zinazokwenda na wakati. Ili kujipanga kwa ajili ya kukabiliana na ajali hapo baadae, tunapendekeza serikali iunde kikosi maalum cha uokozi. Aidha kuwepo kwa Kamanda wa pamoja atakayesimamia na kuratibu vikosi vyote vitakavyoshiriki vikiongozwa na wataalamu wa maafa na uokozi. Kadhalika pawepo na vyombo maalum vya uokozi ambavyo wakati wote vitakuwa standby na viwe na mafuta ya dharura ya kutosha ili kurahisisha zoezi la uokozi kwa ajali nyingine.

17. Ni vyema serikali ikawa na meli za usafiri imara na za uhakika kama ilivyokuwa kwa Mv. Mapinduzi na Mv. Maendeleo. Meli za serikali ziendeshwe kibiashara ili zisiwe na gharama kwenye bajeti ya serikali na faida itumiwe kununua meli nyingine.

18. Baada ya ajali ya MV. Spice Islander Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaahidi Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla yaliyotokea katika ajali hiyo hayatarudiwa. Mpaka sasa serikali haijajipanga kuwa na utaratibu unaoeleweka wa uokoaji ajali ikitokea. Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo ndiyo inayoratibu masuala ya maafa na uokoaji inapaswa kuwajibika.

19. Mwisho tunarudia kutoa rambirambi kwa ndugu na jamaa wote waliopoteza ndugu zao katika maafa haya, CUF tunaungana nao katika kipindi hiki kizito cha majonzi na kuwataka wawe na subira na watambue kuwa msiba huu ni wetu sote, na kila mmoja wetu ameguswa sana na tunawapa pole wale walionusurika pamoja na kuwatakia afueni njema ili warudi tuungane nao katika harakati za maisha na kulijenga Taifa letu, lakini pia Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi AMIN!!!!!

HAKI SAWA KWA WOTE

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti Taifa

Popular Posts