Mwogeleaji Ammaar Ghadiyali ,
Mwandishi nikiwa na mwogeleaji Magdalena Moshi, ambaye anatazamiwa kupambana Jumatano.
Macha (kushoto mwanzo) akiwa na waogeleaji, Magdalena Moshi, Ammaar Ghadiyali , Magdalena na kocha Sheha Mohammed, mazingira ya Olimpiki juzi.
Waogeleaji, Ammaar Ghadiyali, Magdalena Moshi na kocha wao Sheha Mohammed, majuzi ndani ya kijiji cha Olimpiki waliposhukia London.
Kundi la Tamthiliya ya Vijana Uingereza likiwasterehesha wanamichezo wa Tanzania katika shsrehe za kuwakarisha michezoni Alhamisi iliyopita. Sherehe hiyo ilihudhuriwa pia na maofisa mbalimbali wa Ubalozi wetu Uingereza.Picha na Freddy Macha
--
Na Freddy Macha
Mwogeleaji Ammaar Ghadiyali mwenye umri mbichi wa miaka 15, anatazamiwa kushiriki mashindano huria ya mita 100 na 50, kesho hapa London. Hii ni mara ya kwanza kwa Mtanzania mdogo kiasi hicho kushiriki Olimpiki.
Ammaar alinieleza mwaka jana alishiriki pia mashindano ya kimataifa ya Michezo ya majini (FINA world championships) Shanghai, China ambapo alipata uzoefu mzuri sana. Akiwa na umri wa miaka 14 tu alichukua nafasi ya 99 kati ya washiriki 130. Mashindano hayo yanayofanywa kila mwaka sehemu mbalimbali duniani yalijumuisha nchi 181.
“Nilianza kuogelea nikiwa na miaka minane, na mwalimu wa kwanza pale International School, Dar es Salaam sitamsahau. Jina lake ni Ferrick Kalengela.”
Ammaar ambaye ana asili ya Kihindi anaona fahari kuiwakilisha Tanzania na haoni sababu ya watu kumbagua au kutoamini imani na moyo wake katika uogeleaji na michezo. Nlipomuuliza kwa nini anaupenda sana mchezo huu, Ammaar hakupepesa. Alijibu haraka: “ Nikiogelea ninatulizana na kufurahi sana.”
Mwenzake ambaye ni mwanamke kijana mwenye miaka 21 anasomea shahada ya mwanzo ya Sayansi ya Afya, ni Magdalena Moshi. Magdalena anauhusudu mchezo huu wa kuogelea alianzia shule hiyo hiyo ya International School akifundishwa na Bi Tony Ongala, mjane wa mwanamuziki maarufu, hayati Remmy Ongala.
“Tony Ongala alinipa moyo sana,” anakiri, Magdalena ambaye pia atashiriki mbio za mtindo huria wa mita 100 na 50.
Wanariadha hawa wawili wanasaidiwa na kocha mwenye uzoefu wa miaka mingi, Shea Mohammed, mzawa wa Zanzibar. Sheha anasema alianza kuogelea mwaka 1989 na sasa hivi ni kocha wa askari wa majini waitwao- KMKM, visiwani.
“Nnaamini hawa vijana watafika mbali, maana kila wanaposhiriki katika michuano ya kimataifa wanazidi kusonga mbele kiufundi na kimbinu.”
Vijana hawa wamewataka wananchi na wanahabari wasiwe wanawakatisha moyo wanamichezo wake. “Nchi yetu haina utamaduni wa kuwapa moyo wanariadha wetu,” anasema Magdalena, ambaye hufanya mazoezi kila siku mara mbili bila kukosa. “Mtu unafanya tizi kwa bidii lakini badala ya kuungwa mkono unakosolewa. Hivi si vizuri. Toka nikiwa mdogo nimekuwa na ari na moyo na ndoto wa kuipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa! Na sasa wakati karibu umefika.”
Baadaye nilipoongea na Balozi wetu Uingereza , Mheshimiwa Peter Kallaghe alidokeza kwamba riadha ni fani ambayo ina uwezekano wa kuwapa Watanzania sifa kuliko michezo inayojumuisha watu wengi kama mpira, mathalan.
Akitoa mfano wa mkimbiaji maarufu wa miaka ya Sabini ambaye siku hizi ndiye Katibu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, Balozi Kallaghe alisema ushindi wake Bayi mwaka 1974 hadi 1980 ulilijenga sana jina la Tanzania. “Na yeye ni mtu mmoja tu.”
Bayi aliweka historia katika mbio za mita 1,500 alipoongoza wakimbiaji maarufu wa kimataifa enzi hizo, mjini Christchurch, New Zealand, Ben Jipcho (Kenya) na John Walker (Marekani) akaweka rekodi ambayo haijavunjwa katika Jumuiya ya Madola.
Baadaye Bayi na Mtanzania mwingine, Suleiman Nyambui walitwaa medali ya fedha Olimpiki ya Moscow mwaka 1980.
Sifa hii ina faida ya kulijenga jina la Tanzania na kutusaidia kiuchumi kupitia watalii na mahusiano ya kimataifa. Tumwangalie, Usain Bolt alivyolijenga jina la Jamaika toka aanze kuwika baada ya michuano ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008.
TUWATAKIE USHINDI NA USHIRIKI MWEMA WA MICHEZO AMMAAR GHADIYALI NA MAGDALENA MOSHI.
TANZANIA OYEEE!
Msome Freddy Macha zaidi: