Mwenyekiti wa sasa wa Taasisi za Mabenki ya Maendeleo ya Afrika (AADFI) Peter Noni, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), akizungumza na jopo la wataalamu wa AADFI kabla ya kumkaribisha Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe kufungua mkutano wa 38 wa mwaka wa Taasisi hiyo jana mjini Arusha. Jopo la wataalamu limekutana kujadili ni kwa jinsi gani taasisi hiyo inaweza kusaidia maendeleo katika nchi za Afrika. Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Taasisi za Mabenki ya Maendeleo ya Afrika (AADFI) Peter Noni kabla ya kufungua rasmi mkutano wa 38 wa mwaka wa Taasisi hiyo jana mjini Arusha. Kulia ni Mwenyekiti wa heshima (Honorary Chairman) Geoffrey Qhena wa AADFI. Picha na mpigapicha wetu Arusha.
--
JOPO la wataalamu kutoka Taasisi za Mabenki ya Maendeleo ya Afrika (AADFI) linakutana kujadili ni kwa jinsi gani taasisi hiyo inaweza kusaidia maendeleo katika nchi za Afrika.
Taasisi hiyo imebainisha kuwa itajikita katika kuzungumzia masuala ya miundombinu kwa nchi za Afrika kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa. Akifungua mkutano wa 38 wa mwaka wa AADFI jana mjini Arusha jana, Waziri wa Uchuluzi Dk. Harrison Mwakyembe alisema, ujenzi wa miundombinu kwa nchi zinazoendelea ni suala linalogharimu gharama kubwa.
Alisema kutokana na gharama hizo serikali nyingi zimeshindwa hata kukarabati miundombinu iliyokuwapo tangu mwanzo na kusababisha maendeleo kushindwa kupatikana na kwa urahisi.
“Bila Miundombinu huwezi kupiga hatua, hawa leo wamekutana kuumiza vichwa na kuona ni jinsi gani wanaweza kuchangia au kutoa fedha katika kuendeleza Bara la Afrika.“Sisi tuna Reli ya Kati Dar – Kigoma, Tabora – Mwanza, Reli ya TAZARA Dar - Tunduma. Lakini hebu tuangalie Reli hiyo ina uzito gani katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.
Dk. Mwakyembe alibainisha kuwa matatizo yanayoikumba sekta ya miundombinu kwa sasa yamesababishwa na ukosefu wa mitaji mikubwa ya fedha ikiwamo ukosefu wa mikakati mizuri ya kuendeleza mitaji. “Leo hii zaidi ya asilimia 95 ya mizigo ina safirishwa kwa magari badala ya kutumia usafiri wa Reli ambao ungeweza kabisa kupandisha uchumi wa nchi yetu,” alisema Dk. Mwakyembe
“Bila kutumia hawa wenzetu mfano Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) huwezi kupiga hatua katika nyanja muhimu za usafiri wa Anga, maji, reli kwani sekta zote hizo zinahitaji fedha nyingi zaidi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa sasa wa Taasisi ya AADFI Peter Noni akizungumzia mkutano huo wa 38 alisema, wamekutana kipindi cha mikutano ya ADB, lakini pia kama Taasisi watazungumzia jinsi gani watasaidia maendeleo kwa nchi zao.
“Tumechagua kuzungumzia miundombinu kwani mpaka sasa mahitaji ni makubwa na serikali zetu zimekuwa zikitegemea fedha za bajeti ambazo ni ndogo na fedha kutoka ADB au Benki ya Dunia,” alisema Noni.
Noni ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIB alibainisha kuwa Benki za Maendeleo barazani Afrika zina majukumu ya kusaidia Serikali zao japokuwa bado zilikuwa hazijapewa fursa ya kusaidia.“Kikao hiki tumekutana kujadili jinsi gani tuzihusishe serikali zetu na zitutambue kwamba na Benki hizi zinaweza kutoa mchango japokuwa bado ni change,” alisema Noni na kuongeza.