Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ,alipokuwa akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali vya Bara na Visiwani,katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar Jana.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad,na Mawaziri wakimsikiliza Rais wa Zanzibar Dk. AliMohamed Shein akizungumza na Waandishi Ikulu Zanzibar.
Mawaziri wa Serekali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar
--
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amesema kwamba Serikali italinda amani kwa nguvu zote na kuonya kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua watakaochochea na kufanya vurugu.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar jana,Dk. Shein alisema “Tutailinda amani kwa nguvu zote, atakayethubutu kuchezea tutamshughulikia kwa mujibu wa sheria”
Rais Shein alisema amesikitishwa sana na vitendo vilivyotokea wiki iliyopita na kuelezea vurugu hizo zimeharibu sifa njema ya Zanzibar ambayo kwa miaka mingi ianjulikana kwa uvumilivu wa kidini kiasi cha hata Serikali ya kikoloni mwaka 1953 kuamua kufanya shindano la uchoraji wa stamp ya uvumilivu wa kidini.
“Kwa masikitiko makubwa nataka kusema kuwa vitendo vilivyotokea vya kuvunja amani ni vya aibu, vimetusononesha sana na haya wananchi lazima wajue kuwa amani yetu ni muhimu kuliko jambo lolote lile” Alisema Rais Dk. Shein.
Alisema ameshangazwa na vitendo vya uchomaji makanisa moto vilivyofanywa wiki iliyopita akihoji kwamba kulikuwa na uhusiano gani baina ya Muungano na makanisa “Mie nilikuwa nashangaa sana hivi kuna uhusiano gani kuzungumzia Muungano na kuchoma makanisa,kupora mali za watu”
Alisema Dk. Shein. Rais Dk. Shein alisema matatizo ya Muungano yanashughulikiwa chini ya utaratibu uliokubaliwa na Serikali mbili, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kuna kamati ya kushughulikia kero za Muungano na hadi sasa kuna mambo 12 yanafanyiwa kazi ikiwemo suala la mafuta na gesi asilia.
“Taratibu za kutatua kero za Muungano zinaendelea, kuna mambo 12 yamewasilishwa katika kamati na yanafanyiwa kazi, miongoni mwa hilo ni suala la mafuta na gesi asilia, sisi tumeshaamua, SMT bado haijaamua ,lakini sisi tumeamua kuyaondoa katika Muungano, lakini nasema ndugu wawili hawagombani…tutakubaliana” Alisema Rais Dk. Shein.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao na akielezea kuwa hiyo ni fursa muhimu kwa Wazanzibari kueleza wanataka katiba iweje na kuwatoa wasiwasi kuwa hakuna atakayetishwa na wasiogope,lakini akasisitiza ni lazima wasubiri Tume ndipo watoe maoni yao maana wakieleza sasa hakuna anayewasikiliza.
“Wanaotoa maoni yao kuhusu Muungano kwa hivi sasa wanapoteza muda wao, ni sawa na kusema na ukuta tu kwani hakuna anayewasilikiza, hakuna anayechukuwa maoni yao maana Tume haijaanza kazi,wasubiri itakapoanza wakatoe maoni yao”
Alisema Rais Dk. Shein. Rais Dk Shein alitoa ufafanuzi huo akijibu swali la waandishi waliohoji kuwepo kwa kamati ya kutatua kero za Muungano na mjadala wa katiba mpya kwamba Serikali ingesubiri matokeo ya Tume ya Katiba kuhusu Muungano maana inawezekana mambo yakabadilika.
“Sheria ya Tume ipo wazi, lazima wafuate sheria na taratibu hatazuiwa mtu kutoa maelezo yake,lakini kero za Muungano zinaendelea kushughulikiwa kuwepo kwa Tume ya Katiba hakuzuii kamati iliyo chini ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar kushughulikia kero za Muungano.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Shein ameipongeza Polisi kwa busara na hatua walizochukua kushughulikia vurugu zilizotokea wiki iliyopita Visiwani Zanzibar ” Nilipopigiwa simu nikauliza kuna alijeumizwa,vifo nikaambiwa hakuna nikasema Alhamdulillah salama”
Alisema Dk Shein. Alisema kwamba licha ya Polisi kuchokozwa na vijana waliokuwa wakichoma moto matairi ya magari barabarani, kuweka mawe na magogo kuziba njia,lakini Polisi ambao walikuwa na silaha hawakutumia silaha hizo,zaidi ya kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.
”Jeshi la Polisi halibebi lawama,linastahili sifa na kupongezwa…Polisi wana busara sana wanafanya kazi vizuri hawa ndugu zetu wa Polisi kwa kweli lazima tuwapongeze” Alisisitiza Rais Dk. Shein wakati akijibu swali kwamba Polisi wanastahili kulaumiwa, Rais alisisitiza kuwa Polisi walitimiza wajibu wao kwa uzalendo mkubwa wa kuepusha madhara kwa jamii.
”Mimi nilikuwa natoka mazikoni, nilipita barabara ya amani, mwanakwerekwe, nimejionea namna vijana walivyoweka mawe,magogo, kuchoma matairi,lakini Polisi hawakutumia nguvu zaidi ya kuwatawanya kwa kutumia mabonu ya machozi, tuwapongezeni Polisi wetu wamejitahidi sana” Aliongeza.
Rais Dk Shein alisema kwa wale wote waliokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,haki itatendeka kwa kila mtu na kwamba hakuna atayakeonewa wala kudhulumiwa.
Pia alisema Serikali inafanya tathimini kuweza kuelewa athari za matukio yaliyotokea. Pia alitumia fursa hiyo kuwapa pole wale wote waliopatwa na matatizo ya vurugu zilizotokea.