Pages

Friday, June 1, 2012

MAKAMU WA RAIS DK. GHARIB BILAL AKUTANA NA MKURUGENZI MKUU WA WWF

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la WWF, Jim Leape (wa pili kutoka kwa Makamu) na ujumbe wake wakati walipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam jana, Mei 31, 2012 kwa mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirik la Kimataifa la WWF, Jim Leape (wa pili kushoto) na ujumbe wake, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Dar es Salaam jana Mei 31, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-Ofisi ya Makamu Wa Rais
--
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na ujumbe wa Mfuko wa Dunia wa Kuhifadhi Maumbile (WWF) ambao umeelezea nia yao ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuendeleza uvunaji endelevu wa raslimali asilia bila ya kuathiri mazingira.


Mkurugenzi Mkuu wa WWF James Leape ambaye alifuatana na ujumbe wa watu watano alimweleza Makamu wa Rais alipomtembelea ofisini kwake Ikulu jana, kuwa mara nyingi miradi inayohusiana na raslimali asilia ikiwemo ya madini inapotekelezwa husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo husika.

Alisema tathmini ya athari kwa mazingira ni muhimu ili kuendeleza uchimbaji endelevu wa madini hayo na kuiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika kilimo na hivyo kufanikisha malengo yake ya kufikia uchumi wa kijani.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais alisema pamoja na matatizo yaliyopo lakini wakati miradi inapoanzishwa suala la tathmini ya mazingira huwa linapewa kipaumbele akitoa mifano ya miradi ya gesi asilia ya Songo songo pamoja na ya chuma na makaa ya mawe iliyoko Ludewa katika mkoa mpya wa Njombe.

Alisema serikali inaamini kwamba miradi hiyo itaharakisha maendeleo kwa kuwa itasaidia kufua umeme na hivyo kuwawezesha wananchi kupunguza matumizi ya mkaa kwa kupikia na pia kupitia mgodi wa chuma kuna fursa ya kujenga viwanda vya chuma kwa matumizi ya hapa nyumbani na kuuza nje ya nchi.

Aliuambia ujumbe huo kuwa suala la utunzaji wa mfumo wa ekolojia ni sera ya nchi na kusema asilimia 40 ya eneo la nchi limehifadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kuhusu uchumi wa kijani, Dk. Bilal alisema serikali imejipanga vizuri kwa hilo kwa kuwa tayari mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Ruvuma na Morogoro inapewa uzito wa pekee kwenye suala la kilimo kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kijani.

MWISHO

Popular Posts