Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Bw. Klaus Brendes wakipewa maelezo na Meneja wa Mradi Bi. Grace Mwang'onda jinsi watakavyokata utepe kuzindua Jengo la huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa.
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) Bw. Klaus Brendes akifungua Kitambaa kuashiria ufunguzi wa jengo hilo la huduma kwa wagonjwa wa ndani (OPD) katika hospitali ya Cardinal Rugambwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Bw. Peter Maduki akisoma ripoti fupi ya mradi kwa mgeni rasmi Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donan Mmbando ambaye alimwakilisha waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Hussein Mwinyi
Meneja wa Mradi Bi. Grace Mwang’onda akiongea na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi huo.Kwa picha na habari zaidi www.afyamtandaonetwork.ning. com, www.cssc.or.tz
---
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kuboresha zaidi ushirikiano na sekta binafsi yakiwemo mashirika ya dini, kwa kuboresha zaidi mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utoaji wa Huduma za afya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk. Hussen Mwinyi katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donan Mmbando wakati wa ufunguzi wa jengo jipya linalohudumia wagonjwa wa nje (OPD) liliojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya Ujerumani iitwayo KfW na kusimamiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za jamii (CSSC) kwa lengo la kuboresha Huduma ya afya na elimu nchini.
Dk. Mwinyi amesema uboreshaji wa mazingira ambao serikali inatekeleza ni pamoja na kutoa ruzuku kadiri hali ya fedha inavyoruhusu, kushirikisha sekta binafsi katika kupanga, kutekeleza na kutathimini utoaji wa Huduma za afya nchini.
Aidha Dk. Mwinyi amebainisha kuwa kwa sasa serikali inatumia hospitali Teule za wilaya zinazomilikiwa na Kanisa 39 na hospitali mbili kama hospitali za rufaa za Kanda. Dk. Mwinyi amefafanua kuwa hivi karibuni Serikali imezipandisha hadhi hospitali 10 za mashirika ya dini na kuzifanya hospitali za rufaa ngazi ya mkoa.
Akiwasilisha ripoti fupi ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Peter Maduki amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo katika hospitali ya Cardinal Rugambwa ulianza rasmi mwaka 2008, chini ya usimamizi wa CSSC na mshauri msanifu wa ujenzi kutoka Kampuni ya Landplan Icon Architects wa Dar es salam na Mkandarasi M/S Build All Contractors.
Bw. Maduki amefafanua kuwa kazi ya kukamilisha ujenzi huo imegharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 900 na fedha hizo zote zimetolewa na serikali ya Ujerumani.
Akielezea jengo hilo la kisasa, Bw. Maduki amesema kuwa lina vyumba vya matibabu kulingana na mwongozo wa wizara ya Afya, vyumba hivyo ni kwa ajili ya Huduma za maabara, upasuaji mdogo, dawa, sindano, ushauri, mikutano uchunguzi (scanning) na mapumziko Aidha vyumba vingine ni kwa ajili ya mazoezi ya viungo, ofisi na sehemu kubwa kwa ajili ya kusubiria.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya Ujerumani KfW, Bw. Klaus Brendes akizungumza katika ufunguzi huo kwa niaba ya balozi wa Ujerumani nchini, amesema serikali ya Ujerumani inafadhili miradi mingi ya maendeleo Tanzania kama vile; maji, afya, elimu nk. inafarijika kuona miradi hii inafanikiwa vizuri ukiwemo mradi huo wa ujenzi wa jengo hilo la hospitali ya Cardinal Rugambwa, na kuahidi kuendelea kusaidia, miradi mingine ya maendeleo.
Akitoa neno la shukrani Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es salaam ambao ndiyo wamiliki wa hospitali hiyo, Mhashamu Eusebius Nzingilwa amewashukuru wafadhili, serikali na CSSC kwa jitahada kubwa walizoonyesha katika ujenzi huo.
“Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na msaada mkubwa wanatoa katika kuboresha huduma za afya nchini pia wafadhili kwa msaada wao wa kifedha pamoja na CSSC kwa utendaji wenu wa kazi katika kusimamia ujenzi huo” amesema Askofu Nzigilwa.
Askofu Nzigilwa amebainisha kuwa Huduma za afya ambazo zinatolewa na Makanisa ni kwa ajili ya watu wote bila bila kubagua dini ya mtu yeyote yule, hivyo amewataka watumishi wa hospitali ya Cardinal Rugambwa kuendelea kutoa Huduma bora yenye kujaa tunu ya upendo kwa wagonjwa.
Hospitali ya Cardinal Rugambwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, ilianza kama zahanati na baadaye kupandishwa na hadhi na kuwa hospitali mwaka 2005. Inahudumia watu kutoka manispaa ya Ilala na maeneo mbalimbali kama vile Kisarawe, Mkuranga pia na watu wengine kutoka maeneo ya Unguja na Pemba.
Kwa habari zaidi tembelea; www.afyamtandaonetwork.ning. com; www.cssc.or.tz