Mchezaji
Millan Mbise kutoka Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) itakayomwezesha kucheza mpira wa miguu nchini Marekani.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu la Marekani (USSF) limemuombea hati hiyo Mbise kama
mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Virginia Youth Soccer.
Klabu
ya zamani ya Mbise aliyezaliwa Agosti 18, 1994 imetajwa kuwa Super
Sport FC, na mechi ya mwisho kwenye timu hiyo alicheza Novemba 15 mwaka
juzi.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika
kabla ya kutoa hati hiyo kwa mchezaji huyo kama ilivyoombwa na
shirikisho hilo la Marekani.
**************************************
TWFA YATAKA ORODHA YA WAPIGA KURA
Kamati
ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA)
chini ya Mwenyekiti wake Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao
ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano
wa uchaguzi.
Wajumbe
wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa
ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.
Mikoa
ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani
na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa
kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu.
Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.
*****************************************
TASMA WAANZA MCHAKATO WA UCHAGUZI
Chama
cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) leo (Oktoba 19 mwaka
huu) kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa
kufanyika Novemba 28 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis
Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho
zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.
Mwisho
wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka
huu. Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi
nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu
Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya
waliojitokeza kuomba uongozi.
Nafasi
zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu
Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa
Kamati ya Utendaji.
Kipindi
cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na
pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya
TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada
kwenye pingamizi.
Pingamizi
zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili
utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo
vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa
kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu.
Rufani
ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa
10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.