Freeman Aikaeli Mbowe | Mwenyekiti CHADEMA Taifa
MHESHIMIWA rais,
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba kakujalia afya njema tangu ubebe jukumu kubwa la kutawala taifa hili. Naendelea kumwomba aendelee kukujalia afya njema na akupe busara za kukabiliana na vikwazo mbalimbali vya kulijenga taifa la Tanzania na akuepushe na nguvu yoyote ya giza yenye azma ya kulibomoa.
Mheshimiwa rais,
Leo nimeamua kukuandikia waraka huu. Pengine utashangaa kama watakavyoshangaa wananchi wako wengi unaowaongoza. Najua wengine watahoji, iweje nikuandikie kupitia gazetini na isiwe moja kwa moja. Sababu ni rahisi. Kwa kuandika gazetini, nina hakika itakufikia.
Wengine wanaweza kuona ni utovu wa nidhamu kuweka hadharani barua kwenda kwa mtawala mkuu wa nchi. Katika mazingira ya kawaida, hii yaweza kuwa kweli, lakini kwa mazingira na utamaduni uliojengwa na ofisi yako sambamba na chama chako, rais wetu, unayeitwa “mtu wa watu”, uko radhi kuonana kikazi au hata kistarehe na watu wengine wote isipokuwa viongozi wenzako wa vyama vya siasa.
Hata hivyo nikiri, serikali yako, kama ilivyokuwa iliyokutangulia, hukumbuka viongozi wa vyama vya siasa pale panapokuwepo ugeni wa kimataifa, jambo lenye kawaida ya kuambatana na hafla ya ulaji na unywaji Ikulu. Hapo, wapinzani huitwa kwa zamu kwenye ulaji na unywaji.
Aidha, unapokuwa kwenye ziara zako nje ya nchi, serikali yako imejijengea utamaduni wa kuwabeba “msukule” wabunge wa upinzani.
Wapinzani wanaoambatana na wewe hawana jukumu lolote wanalopewa zaidi ya kuwa sehemu ya kundi kubwa la “watalii” wenye jukumu moja tu, la kuhalalisha matumizi ya kodi za wananchi, kutambulishwa kwenye kila kikao au mikutano kwa lengo la kujenga taswira chanya ya serikali yako.
Wengi hubebwa bila hata kujua madhumuni ya safari ni nini! Na wakirejea, biashara huishia pale uwanja wa ndege!
Yatokeapo maazimisho ya sherehe za kitaifa, wapinzani hukumbukwa. Hapa ni kuwahadaa wananchi wakiwemo waandishi wa habari. Tutaonana Uwanja wa Taifa kukuona ukikagua gwaride, kisha tutaachana pale, kusubiri sikukuu nyingine ya kitaifa.
Ninaamini wengi wa viongozi na wabunge wa upinzani hukubali kushiriki mambo haya kama ishara ya utayari wao na vyama vyao katika kujenga utaifa wetu na si kwa ajili ya kingine chochote.
Hata hivyo nikiri, upande wa pili wa mchezo huu mchafu, ghafla umedhoofisha wapinzani dhaifu na wabinafsi na umejenga taswira ya rushwa ya kisiasa na kimaslahi. Mwaliko mmoja tu wa Ikulu au safari moja na msafara wako au waziri mkuu, vimeweza ghafla kubadilisha misimamo ya baadhi ya watu walioonekana awali kuwa makini katika kutetea maslahi ya taifa.
Kila baya lina jema, utamaduni huu kwa upande mwingine unasaidia taifa hili kujua mchele ni upi na pumba ni zipi.
Naamini kwa dhati kabisa, nia ya serikali yako si njema, kwani ina kusudio la kuwatumia wapinzani kama chambo, hasa mbele ya macho ya viongozi wenzako wa nje, kujenga sura ya kinafiki kuwa ndani ya nchi yetu, tuna mshikamano wa kisiasa.
Mheshimiwa rais,
Waraka wangu kwako leo unakusudia kukukumbusha jambo moja la muhimu sana, ambalo napenda kuamini unalijua. Cha ajabu ni kwamba, kama ungekuwa hulijui nisingesikitika. Lakini nasikitika kwa sababu naamini unalijua, lakini pengine unalidharau.
Nikiri jambo moja. Kama kuna kitu kinaniweka kwenye siasa, si chuki binafsi, si ajira na wala si cheo, bali ni ndoto yangu ya siku moja kuona nimeshiriki mchakato wa kuistawisha nchi yangu, kwa pamoja na mambo mengine, kujenga umoja wa kitaifa.
Hakuna jambo lolote la “neema” linalowezekana katika taifa lililogawanyika. Si rahisi wote kuwa na fikra sawa, lakini ni rahisi kwa asilimia zaidi ya 80 ya wananchi kuupenda, kujivunia na hivyo kuuulinda utaifa wao. Hii haijalishi kama nchi ni maskini au tajiri. Hali hii hata hivyo, haizuki. Hufanyiwa kazi, tena kimkakati.
Nasisitiza, sifa ya kwanza ya taifa lolote ni umoja wa utaifa wake. Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na kundi lolote la kijamii ndani ya nchi kama vile chama, dini au kabila. Hujengwa pale dhamira ya mtawala inapowaongoza watu wake kuweka kama agenda kuu ya uongozi na dira ya nchi msingi wa kuunganisha taifa bila kujali mipaka ya kiitikadi, kidini, kikabila, kijiografia, kijinsia au rangi.
Baada ya kiongozi kujidhihirisha kwa fikra zake, huzitafsiri kuwa dhamira ambayo huitoa kama kauli, si mara moja, bali kila fursa itokeapo, kwani kwake ni sawa na sala. Ni uumini. Naye hatimaye hukamilisha uumini wake kwa vitendo, tabia na mienendo yake ya kila siku.
Ndiyo, watu na hususan viongozi watapingana kwa mengi ikiwemo mitazamo, lakini yote haya hayawi mapenzi yao kwa taifa lao.
Watalipenda, watajivunia na kamwe hawatalikimbia!
Mheshimiwa rais,
Dhuluma, nguvu na rushwa vinaweza kushinda uchaguzi, lakini haviwezi kujenga umoja wa kitaifa. Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na fedha, majeshi au mifumo ya kiusalama. Mifumo hii hujenga hofu na ukondoo!
Penye dhamira nzuri, kila jambo lililo kikwazo cha umoja wa taifa huwa ajenda yenye kipaumbele kwa kiongozi yeyote anayestahili sifa ya kuwa mtu wa watu kama ambavyo naamini ungependa. Kwa vyovyote vile, hutafurahisha wote, lakini wenye kupenda haki katika maisha haya ni wengi kuliko wenye kudhulumu na kuichukia haki.
Utawala ni kazi ngumu. Inahitaji uwezo wa kufikiri na kutafakari, ambao nina hakika unao. Penye umoja wa kitaifa, hata baadhi ya maamuzi magumu ambayo hayapendwi na wananchi huridhiwa.
Kiongozi makini lazima akubali lawama pale anaposimamia jambo ambalo anaamini lina maslahi kwa taifa. Hali hii inamfanya kiongozi awe mkweli, muwazi na asiyefanya mambo kwa kificho. Kiongozi mzuri ni lazima basi kwa kiwango kikubwa atende yale anayoyahubiri.
Mheshimiwa rais,
Niruhusu nikukumbushe jambo moja, ambalo kwa mara nyingine, naamini unalijua, lakini bado napata wakati mgumu kujua unalitafakari vipi. Hili linamhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye baadhi ya wananchi wako wameamua kukuita JK kama yeye.
Sikusudii kufungua ukurasa wa somo la Mwalimu, ila nakumbuka wakati wa kampeni, wapiga debe wako wakuu, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mzee Stephen Wassira – ambao vilevile leo ni mawaziri wako, walifanya mkutano na waandishi wa habari wakidai sina haki ya kumzungumza Mwalimu kwenye kampeni zangu, kwani wewe unamjua Mwalimu kuliko mimi!!
Dhamira nyoofu na kauli, vilivyoshabihiana na matendo, ndivyo viliyompa Mwalimu jeuri, kujiamini, kupendwa, kuheshimika, kuogopwa, kusamehewa, kuombewa na hatimaye leo, wengine (ndani ya imani yake) wanatafakari uwezekano wa kumfanya mwenye heri na hatimaye mtakatifu.
MWALIMU ALIJENGA TAIFA!
Mwalimu, kama binadamu, alikuwa na makosa kadhaa ya kisera na hasa ya kimaamuzi, hususan katika masuala ya baadhi ya sera za kiuchumi.
Aliongoza Tanzania wakati mgumu sana, lakini pamoja na umaskini ule, kila alichofanya Mwalimu kililenga utaifa, Utanganyika na hatimaye Utanzania wetu!
Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, umezungumza mengi. Ndani ya nchi na hata nje. Uzuri wa maendeleo ya kiteknologia, yanatusaidia sisi walalahoi kujua wewe rais wetu umezungumza nini popote duniani.
Nimeona nivunje itifaki zote, niweze kukupongeza bila kificho chochote mbele ya Watanzania wenzangu, kuhusu hotuba uliyoitoa bungeni Desemba 30 mwaka 2005, wakati ukizindua Bunge jipya baada ya uchaguzi.
Wengine wataendelea kushangaa! Mbona Mbowe anazungumzia mambo ya kale! Hapana!
Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, hakuna maneno mazito, ya kizalendo, ya kiungwana na yenye kutia matumaini ambayo ulishawahi kuyazungumza kama yale. Sifa zote hizi nakupa kwa sababu moja tu: Hotuba ile ilijenga MATUMAINI YA UTAIFA.
Mheshimiwa rais,
Hotuba yako ya kufungua ilikuwa ya kujiamini mno. Ilifurahisha wengi, wakiwemo wa vyama vingine vya siasa. Uliamsha ari ya wananchi wako na wengine tuliamini angalao kwa kipindi cha wiki chache kuwa, sasa mambo huenda yatabadilika. Uliweza kuendelea kuwapagaisha wananchi na kuwafanya “misukule” angalao kwa wiki kadhaa.
Kwa kumbukumbu zangu na ufahamu wangu mdogo wa kisiasa, mara ya mwisho kusikia hotuba iliyogusa wengi kwa kiwango kile, ni wakati wa uhai wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alitania kwenye hotuba zake, lakini hukufanya utani, uzushi au masihara na kauli zake au yeyote atakayekwaza dhamira yake na TAIFA lake!
Kwangu, ile ilikuwa dira ya taifa. Ilijenga hoja za msingi za utaifa bila kujali zimetoka kwenye ilani ya CHADEMA, ya CCM au ya chama kingine chochote.
Tunajua kipindi kile, ulikuwa umetingwa na mambo mengi sana ikiwepo kushangaa, pengine kisirisiri, wingi wa kura zako pamoja na mshikemshike tuliokupatia kwenye kinyang’anyiro. Busara za kawaida zitajua kuwa ulikuwa unatafakari namna ya kuzawadia wale wote waliowezesha miujiza ile kutokea. Ni dhahiri ulikuwa unatafakari namna ya kuunda serikali yako. Naamini kipindi kile ulikuwa hujatulia na kupumzika.
Siku hiyo, nilikuwa ndani ya Ukumbi wa Bunge kama mwalikwa. Bado nilikuwa na mimi natibu majeraha. Nilikusikiliza kwa makini na kujisemea:
Hotuba ya mheshimiwa rais yaweza kuwa jibu la nchi yetu. Je, ameandika vipi hotuba nzuri kiasi hiki wakati ametingwa sana?
Nikakumbuka rais wangu una wasaidizi! Lakini nikajiuliza tena; basi rais utakuwa na wasaidizi na washauri makini sana! Nikajiuliza umewapata wapi ghafla? Kwani nilijiaminisha hawawezi kuwa wale wazee walionikebehi bila haya eti “nisimtumie” Nyerere kwenye kampeni zangu!
Naam, hata kama umeandikiwa, kwa vyovyote umeipitia na kuikubali kwani hata ulipokuwa unaisoma, uliisoma kwa kujiamini na hata kuongezea mengine nje ya karatasi. Hivyo basi, lolote lililo ndani yake ni lako. Napenda kuamini ilikuwa ni dhamira yako! Ni hadidu ya rejea ya miaka mitano ya utawala wako!
Mheshimiwa rais,
Hotuba yako bado naiwaza na kuisoma mara kwa mara. Nina mengi ya kukupongeza ndani yake na waraka huu mmoja hautoshi. Najua nawe una majukumu mengi. Naomba uniruhusu niishie hapa kwa leo na wiki ijayo niingie kuijadili hotuba yako kama walivyofanya wabunge wetu kule Dodoma na mijadala yao ikabaki kwenye kumbukumbu za Bunge, ili zije kusomwa na vizazi vya mbele.
Niruhusu mheshimiwa nifanye kazi hiyo ya kukukumbusha kauli zako mwenyewe, kifungu kwa kifungu na namna ulivyotekeleza kwa vitendo, ahadi zako. Nitakuchosha, lakini ndiyo wajibu na heshima yangu kwa utaifa wetu!
Mheshimiwa rais,
Naomba kutoa hoja…
-