Siwezi kukulaumu wewe na Mamlaka unayoisimamia, wakulaumiwa ni wa Wabunge.
Labda hawakusoma vizuri, lakini wewe ni timu yako naamini ndo chanzo cha
Sheria hii. Hisia zangu na wafanyakazi waliowengi, kama unavyoona makelele,
sijarizika kabisa na hatua hii! Mimi ni mfanyakazi na hata huo ufafanuzi
wako wa Julai 20, 2012 nimeusoma, haikidhi kiu ya kuamini kwamba FAO LA
KUJITOA kufutwa kunafaida yoyote ukiondoa fursa ya kukopa nyumba!!!??? SSRA
inasisitiza eti tuelimishwe, Hatuelimishiki katika hili! "*Mla Mla Leo
bwana Mla Kesho Kala nini?"* Sisi wenye vipato vya chini tunafanya
maendeleo kupitia vijisenti hivyo; tunasomesha, tunajenga kwa awamu,
tunajisomesha wenyewe. Sasa mnatupeleka wapi?
Maisha ya Mtanzania ni ya kubahatisha; wachache wanapita hadi uzee, ndo
maana tunawazee wachache. Wastani wa kuishi kwa Mtanzania wa leo ni Miaka
58 na miezi miwili tu. Sisi mnatutaka kufikishe 55 ili tuishi miaka 3 tu
kisha tufe!! Natukitaka kuendelea na kazi hadi miaka 60 tutakuwa tumekufa
hata kabla ya kuchukua mafao hayo.Bado kuna magonjwa mengi sana yanayoua
mara moja ikiwemo VVU/UKIMWI, lo! Achilia mbali ajali za mala kwa mala;
yote haya yanaashilia kwamba tutafanyia kazi kwaajili ya Miradhi ya watoto
wetu tu, au waume zetu/wake zetu wakibahatisha kufika. MLA MLA LEO mkuu.
Fedha ya nchi yetu pendwa, Tanzania ni ya kuporomoka kila kunapokucha!
Mamlaka yako pamoja na Bunge mnatutaka tutunze hayo makaratasi hadi uzeeni,
huku thamani nayo inaporomoka! Ninahitaji maelezo zaidi hapo yakihusisha
thamani ya pesa yetu na kuporomoka kwake na MAfaho ya Uzeeni.
Ndugu Mkurugenzi, "Kupanga ni Kuchagua", Mwalimu Nyerere alisema. Mbona
sisi hatujachagua kujitoa? Mbona hatukushirikishwa kikamilifu. SSRA
imekimbilia kurubuni wafanyakazi eti "ili kutimiza lengo na mathumuni ya
hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapata mafao bora".
Mafao bora menyewe hayajawahi kutolewa. Tumeona ndugu zetu, watangulizi
wetu akipokea vijihela kiduchu tu! Njia iliyotumika kushirikisha
wafanyakazi hakukidhi haja na mahitaji halisi ya wafanyakazi. Wabunge
hatukuwatuma hilo, jamani. Haya ndo matatizo ya uakilishi. Mwakilishi
anajiamulia tu ya kusema Bungeni, bila kukusanya maoni halisi ya
anaowawakilisha.
Hata SSRA ambayo naamini ndio chanzo cha maudhi haya yote haikufanya
utafiti wa kutosha kuhusu mahitaji halisi ya wafanya kazi. Mahitaji siyo
nyumba pekee. Na si kila mtu anataka kukopa nyumba. Wengine tunataka hela
tuanzishe maduka, wengine tunataka twende kusoma tukiwa ngali vijana.
Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii tunaitumia kujiwekea akiba wenyewe na pindi
malengo yetu akikamilika tunazitoa na kuzifanyia kazi tulizopanga. Enzi
hii, siyo Enzi ya Mwalimu! Ni enzi ya soko huria likiwemo Soko Huria la
Ajira. Mtu anauwezo wa kujenga nyumba hata kama si mfanyakazi wala si
mfanya biashara! Wafanyakazi si mbumbumbu kiasi cha kulazimishwa kujiwekea
fedha. Hebu tuachwe tuamue mambo yetu wenyewe.
Binafsi sioni faida ya Mifuko hii nje ya FAO la Kujitoa. Siwezi hata kukopa
fedha mfano NSSF wakati wao wanatumia fedha zangu ninazoendelea kuweka
kujenga majumba ya kitega Uchumi pasipo mimi kupewa Mgao hata kidogo
angalao. Faida yoooote inakwenda NSSF. Mimi faida yangu ni mafao
madogomadogo tu, kama vile matibabu kiduchu, Kifo (wala sitafaidi). FAO la
kujitoa ndo lenyewe kwa Mfanyakazi. *Mla Mla Leo. *
Mikataba yetu ni ya muda mfupi-Miezi Sita, Mwaka Mmoja, Miwili, nk. Katyika
hali hii unanitaka ni subiri hadi Miaka 55 kwa mafao yangu ya miaka Miwili
au Mitano!? Hii sheria labda tuwaachie watumishi wa Serikali ambao wan
mikataba ya muda mrefu, hadi umri wa miaka 60. Sekta zingine haiwezekani.
Nawasilisha,
Mhangwa, Vincent Manoni
+255 782 396953