Nukuu hiyo si ya kweli. Nimesikitishwa sana na upotoshaji mkubwa wa kunilisha maneno mdomoni uliofanyika katika sehemu kubwa ya habari hiyo (mbali na nukuu hiyo) kwa maslahi ambayo sijui ni ya nani.
Wakati ukijiandaa kuchukua hatua kutokana na sababu ya pili ya kukuandikia barua hii ambayo nitaieleza punde hapa chini, naomba utafakari masuala kadhaa, ikiwemo; kwa nini ilichukua siku zaidi ya tano kwa habari hiyo kuandikwa?
*
Pili, kutokana na usumbufu mkubwa ambao nimeupata kutoka kwa Watanzania wa maeneo mbalimbali wanaotarajia kuniona mwakilishi wao nikizungumzia masuala yanayowahusu wao, ambayo ni muhimu zaidi kuliko jambo jingine lolote kwa sasa.
*
Lakini pia nikiwa Mtanzania anayetambua umuhimu na unyeti wa nafasi ya urais katika nchi hii na kwamba inaamuliwa kwa maslahi mapana ya umma wa Watanzania wala si uchu wa watu wachache, hivyo nisingeweza kutamka maneno hayo ambayo gazeti lako limeandika, naomba kukuandikia rasmi kukutaka ukanushe habari hiyo ukurasa wa mbele kwa uzito huo huo ulioipatia habari hiyo katika toleo tajwa.
*
Lakini pia nikiwa Mtanzania ambaye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kinaamini kuwa kwa sasa suala la urais si kipaumbele, bali muhimu kwa wakati huu ni kushughulika kujua mizizi au vyanzo vya matatizo makubwa yanayowakabili Watanzania ikiwemo umaskini, ujinga, maradhi, ufisadi na utawala mbovu wa CCM, kwani serikali imekuwa ikishughulikia matokeo.
Kama ambavyo chama changu, Watanzania wengine makini na mimi mwenyewe, naamini kuwa kwa sasa suala la muhimu kwetu kama taifa ni kutafuta mizizi au vyanzo vya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ya Watanzania.
*
Kwa chama changu na mimi mwenyewe pia kama mwakilishi makini wa Watanzania, naamini kuwa siku zote suala la urais linategemea mahitaji ya Watanzania na kamwe haliwezi kuamriwa kwa kufuata matakwa na utashi au uchu wa watu binafsi.
*
Lakini pia suala la nikiwa kama mwanachama mwaminifu wa CHADEMA na ninayeipenda nchi yangu kwanza, naamini kuwa suala la urais linafuata katiba, kanuni na taratibu za chama, hatua ambayo haijafikiwa kwa sasa.
*
Naomba kusisitiza kuwa sijawahi kutamka, siwezi kutamka na sitarajii kutamka maneno hayo uliyoyaandika kwenye gazeti tena kwa kuninukuu na kuniwekea maneno mdomoni. Naomba kurudia tena kukutaka ukanushe habari hiyo ukurasa wa mbele kwa uzito huo huo ulioipatia habari hiyo katika toleo tajwa.