Mhe. Gaudentia Mugosi Kabaka ( MB) Waziri wa Kazi na Ajira akizungumza wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa unaojadilini pamoja na mambo mengine tatizo la ajira na hasa kwa vijana, Mhe. Kabaka anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huu wa wiki moja, ukiwashirikisha mawaziri wanaohusika na masuala ya ajira, fedha na uchumi, mambo ya nje , ILO na wanazuoni. katika mchango wake kuhusu changamoto hiyo ya ukosefu wa ajira, Mhe. Waziri Gaudentia Kabaka anasema kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea. Tanzania pia inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kujaribu kulikabili tatizo hilo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa mataifa tajiri na maskini pia na ni bomu ambalo limeshaanza kufuka moshi.
Baadhi ya ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu unaojadili tatizo la ajira, ni mkutano ambao umeandaliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii maarufu kama ECOSOC. Walio kaa mbele ni Kamishna. Ahmed Makame Haji, kutoka Tume ya Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Omar Hamisi Same kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, Bi. Aziza J. Ali, Mkuu wa kitengo kinachoratibu misaada, Idara ya Fedha za Nje, Serikali ya Mapinduzi Zanziba na Bw. Humphrey Shangarai, mchumi kutoka Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
--
Na Mwandish Maalum
Wakati Jumuia ya kimataifa ikiendelea kukuna vichwa kutafuta mbinu na mikakati ya kukabiliana na hatari inayotokana na ongekezo kubwa la ukosefu wa ajira na hususani kwa Vijana. Tanzania inasema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo imeanza kuandaa mikakati endelevu ya kulikabili janga hilo.
Akizungunza katika siku ya pili ya mkutano unaowakutanisha kwa pamoja mawaziri wanaohusika na masuala ya ajira, wataalamu wa masuala ya fedha , uchumi na wanazuoni. Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Mugosi Kabaka ( Mb) anasema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira.
Mhe. Waziri Kabaka anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa wiki moja unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao umefunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon mwanzoni mwa wiki, umeandaliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii (ECOSOC).
“Kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazo endelea duniani, nchi yangu pia inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na hasa kwa vijana. Na tatizo hili linasababishwa kwa kiasi kubwa na uboreshaji wa elimu yetu hadi ngazi ya elimu ya juu, uboreshani na upanuzi ambazo hauendani sambamba na ongezeko la ajira”.
Amewaeleza wajumbe wamkutano huo kwamba, tatizo la ajira pia lipo zaidi kwa upande wa mijini na hii ni kutoka na wimbi la vijana kuhamia mijini.
“ licha ya kwamba vijana wengi wanahamia mijini na hivyo kuchangia katika ukosefu wa ajira, lakini pia hivi sasa tunashuhudia vijana wale wa vijijini kukoa ajira kutokana na athali za mabadiliko ya tabia nchi , mabadiliko ambayo yamekuwa na athari kubwa kwa upande wa kilimo” akabainisha Kabaka.
Akaitaja baadhi ya mikakati inayofanywa na serikali ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, kuwa ni pamoja na mpango wa kurasimisha mali za wanyonge ( Mkurabita) ili mali hizo ziweze kutumika kupata mikopo, upanuzi vya vyuo vya ufundi stadi ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, na kuanzishwa pamona na mambo mengine sheria ya hifadhi ya jamii, mifuko ya jamii, mifuko ya bima ya afya, na vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa ( SACCOS)
Aidha akasema, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ziwamo taasisi za kitaifa na kimataifa, imekuwa ikiratibu mafunzo mbalimbali yakiwamo ya uwezeshaji katika eneo la kilimo ili vijana wawe kujiajiri katika eneo hilo na kwamba mipango yote inalenga katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia.
Aidha akasema, Tanzania pia inaendelea na jukumu la kuhakikisha kwamba ajira kwa watoto inakomeshwa, kuwapo kwa ajira zenye tija, endelevu na zenye hadhi na kwa sababu hiyo akauomba Umoja wa Mataifa kupitia ECOSOC, kuisaidia Tanzania katika eneo la teknolojia.
Mada kuu ya mkutano huu ni kukuza uwezo wa uzalishaji wa ajira kwa vijana, na kazi zenye heshima kwa lengo la kuondokana na umaskini na kukuza uchumi endelevu ili kufikira utekelezaji wa MDGs.
Mkutano huo unatoa fursa kwa nchi wanachama wa UMum kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ambayo ni changamoto kubwa kwa usalama wa dunia. Na hususani wimbi hilo la ukosefu wa ajira kwa vijana, wimbi ambalo limesha onesha kwamba lisipotafutiwa mikakati ya kudumu ni bomu ambalo tayari limeshaanza kufuka moshi.