Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, itaanza zoezi la kutembelea na kuhakiki Vyama vya Kijamii ambavyo vimesajiliwa na Wizara hiyo ili kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usajili wa Vyama.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Vyama vya Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Numbilya Mpolo amesema leo kuwa zoezi hilo litaanza mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza katika Banda la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo Maonyesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea, Mpolo alisema mambo yatakayokaguliwa ni uhai wa Vyama hivyo na utekelezaji wa Katiba zake kama zilivyosajiliwa.
Mambo mengine yatakayokaguliwa ni kama Vyama hivyo vinalipa ada ya kila mwaka kwa mujibu wa Sheria, na pia utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya kufanya vikao vya Chama na kuandaa taarifa za fedha ambazo zinapaswa kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama kila mwaka.
Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa vyama vitakavyobainika kukiuka masharti ya Sheria za uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na kupewa notisi za kusudio la kufuta chama husika.
Kwa mujibu wa Sheria za Vyama, chama kitapewa notisi ya kusudio ya kukifuta, na ikiwa hakitatoa hoja kwa nini kisifutwe, ndani ya siku 21, basi Msajili wa Vyama anaweza kutoa notisi ya kukifuta chama, na baadaye kutoa tangazo la kukifuta chama hicho, katika Gazeti la Serikali.
Akizungumzia kuhusu malalamiko yanayopokelewa na Msajili wa Vyama, Mpolo amesema ni pamoja na taarifa za migogoro inayotokana na kugombea madaraka na pia ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya vyama.
Kuhusu Vyama ambavyo vinabadilisha Katiba zao bila mabadiliko hayo kukubaliwa na Msajili, amesema Katiba kama hizo hazitambuliki kisheria.Amesema hadi sasa jumla ya Vyama vya Kijamii 6,469 vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kati ya hivyo 875 ni Taasisi za kidini.
Amesema zoezi la kusajili Vyama vya Kijamii bado linaendelea na wananchi wenye mahitaji ya kusajili hivyo wanaweza kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wowote ili kupata huduma hiyo.
(Background)
Usajili wa vyama vya Kijamii unafanywa chini ya Sheria ya Vyama, Sura ya. 337 iliyofanyiwa Mapitio mwaka 2002.
Sheria hii inatoa maelezo muhimu kuhusu Vyama hivi, ikiwa ni pamoja na kufafanua kanuni na mwenendo ambayo Vyama hivi vinatakiwa kuufata.
Vyama vya Kijamii ambavyo vinasajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii ni pamoja na Vyama vya Kidini, Vyama vya Maendeleo ya Kijamii, Vyama vya Kimataifa na Vyama vya Kitaalamu.
Baadhi ya mahitaji ya Vyama kuweza kusajiliwa ni pamoja na:
· Kuwa na wanachama waanzilishi wasiopungua,
· Katiba ya Chama,
· Majina na maelezo binafsi (CV) na picha za viongozi wa Chama,
· Barua kutoka Mamlaka ya inayohusika kutambua Chama, inayotambuliwa kisheria, kwa mfano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, au Wizara Mama,
· Barua toka kwa Mwombaji (anayetaka kusajili Chama).
Baada ya kukamilisha vigezo vilivyotajwa hapo juu, na vinginevyo kufuatana na Sheria ya Usajili wa Vyama, Sheria inasema, Msajili wa Vyama, akiridhika na malengo ya kuanzishwa kwa Chama husika, atafanya usajili wa Chama hicho, huku akitilia maanani matakwa umma na taifa kwa ujumla.
Usajili wa Chama, katika mazingira ya kawaida, unachukua siku tano hadi 7 na wakati mwingine unaweza kuchukua muda mrefu kutegemeana na aina ya Chama, ambapo wakati mwingine itahitaji uchunguzi wa kina zaidi kabla ya kusajiliwa.
MWISHO