Pages

Thursday, July 5, 2012

Wabunge hawa ni mfano wa kuigwa Juni 4, 2012

Tunawapongeza wabunge kutoka kamati za Kudumu za Bunge za Huduma za Jamii, Katiba, Sheria na Utawala na ile ya masuala ya UKIMWI kwa kukubali kukutana na kusilikiza maoni na mapendekezo ya Sikika, bila kudai posho.

Sikika ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Tanzania kwa lengo la kufanya utetezi katika utoaji na upatikanaji wa huduma bora za afya kote nchini. Kwa kipindi cha miaka mitano sasa, Sikika imekuwa ikikutana na Wabunge na kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali na uchambuzi wa bajeti. Tafiti hizo, pamoja na mambo mengine, zimekuwa zikionesha jinsi ufanisi katika mgawanyo wa rasilimali unavyoweza kusaidia kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii.

Kwenye mikutano ya awali, Sikika ilikuwa ikigharamia malipo ya posho kwa wabunge, jambo ambalo liligharimu shirika fedha nyingi na kuathiri shughuli nyingine za jamii.Sikika imekuwa ikipinga matumizi yasiyo lazima ya fedha za umma, ikiwamo malipo ya posho za vikao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Wabunge wana jukumu la kukusanya na kuwasilisha maoni ya wananchi kwa Serikali. Kwa muktadha huo, mwaka jana (2011), shirika lilielezea masikitiko yake na kutoridhishwa na tabia ya kudaiwa kuwalipa posho Wabunge kwa kazi ambazo wanapaswa kuzifanya.

Tofauti ni miaka ya nyuma, hivi karibuni, Wabunge kutoka kamati hizo, walijitokeza kwa nyakati tofauti na kushiriki kikamilifu kwenye mikutano ya Sikika, huku wakifahamu kwamba hakutakuwa na malipo ya posho. Tulifurahishwa pia na ushirikiano na usikivu wa wabunge wa kamati hizo ambao walipokea matokeo na mapendekezo ya tafiti zetu na kuahidi kuzifanyia kazi katika Bunge la bajeti litakaloanza Juni 12, 2012.

Tunawapongeza sana wenyeviti wa Kamati hizo, Mh. Margareth Sitta- (Huduma za Jamii), Mhe. Pindi Chana- (Katiba, Sheria na Utawala) na Mhe. Lediana Mngo’ng’o- (Masuala ya UKIMWI) ambao wameonesha kuelewa na kuthamini mchango wa tafiti zinazofanywa na asasi za kiraia. Sikika tunaamini kwamba matokeo ya utafiti yanawasaidia wabunge kupata takwimu, picha halisi, kuwa na uwezo wa kujadili na kupendekeza namna ya kukabili changamoto mbalimbali katika kuboresha huduma za jamii nchini.

Asasi za kiraia kama Sikika na watanzania wamekuwa wakiguswa na suala la ulipaji wa posho kwa wabunge wakati wanalipwa mishahara.Tunaamini kwamba wabunge wanaweza kutimiza wajibu wao bila kulipwa posho. Vilevile, kwa kuzingatia nafasi yao ya uwakilishi, Wabunge waisaidie Serikali kuokoa fedha zinazotengwa kwa ajili ya posho na kuzielekeza katika maeneo yatakayowanufaisha wananchi wengi, kama vile afya na elimu.

Mr. Irenei Kiria

Mkurugenzi wa Sikika, P.O. Box 12183 Dar es Salaam,

Simu: +255 222 666355/57, Faksi: 2668015, Barua pepe:info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz

Popular Posts