HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA MAWASILIANO NA
UJENZI YA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA
YA ARDHI MAKAAZI MAJI NA NISHATI
KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kunijaalia afya njema na uzima wa kuweza kusimama mbele ya Baraza lako tukufu katika kutekeleza majukumu ya kulijenga taifa letu. Aidha napenda kwa moyo wa dhati nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii muhimu ya kutoa maoni ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Waziri wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mheshimiwa Ramadhani Abdalla Shaaban pamoja na watendaji wa Wizara hii wote kwa mashirkiano yao ya dhati wanayoipatia Kamati yetu katika kutekeleza kazi zake za msingi kama ilivyoelekezwa katika kanuni za Baraza la Wawakilishi. Aidha, napenda kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Wizara hii, tunaamini kwamba uzowefu na jitihada zake zitasaidia ufanisi wa Wizara hii ngumu, aliyokabidhiwa. Mheshimiwa Spika, kwa moyo thabiti kabisa napenda pia kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kamati hii kwa mashirikiano yao wanayonipatia katika kuhakikisha kwamba Kamati yetu inaweza kukamilisha kutekeleza kazi zake za kuliwakilisha Baraza katika kusimamia na kufuatilia shughuli mbali mbali za Wizara inazozisimamia.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza msisitizo wa Shukurani zangu naomba uniruhusu niwatambue wajumbe wa waliounda Kamati hii kwa majina.
Mhe. Makame Mshimba Mbarouk M/kiti
Mhe. Rashid Seif Suleiman M/Mwenyekiti
Mhe. Hassan Hamad Omar Mjumbe
Mhe. Subet Khamis Faki Mjumbe
Mhe. Salma Mussa Bilali Mjumbe
Mhe. Shawana Bukhet Hassan Mjumbe
Ndg. Aziza Wazir Kheir Katibu
Ndg. Abdalla Ali Shauri Katibu
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi ni miongoni mwa Wizara muhimu sana kwa maendeleo na mustakabali wa nchi na wananchi wa nchi yetu, hii ni kutokana na ukweli kwamba Wizara hii imebeba sekta muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu pamoja na maisha ya wananchi kwa ujumla, miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na Sekta ya Ardhi, Maji na Umeme. Umuhimu wa sekta hizi umepelekea kuwepo kwa changamoto nyingi katika Wizara ya Ardhi Makaazi Maji na Nishati. Kutokana na hali hiyo yamekuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na uendeshaji wa taasisi zinazohusika na sekta hizo katika kuwahudumia wananchi. Hivyo ni wajibu wa watendaji wa Wizara hii kufanya kazi kwa uadilifu na umakini mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi pamoja na taifa kwa ujumla. Aidha, kwa upande wa Serikali ni vyema ikahakikisha kwamba inazijengea mazingira mazuri taasisi zilizomo katika wizara hii, ikiwemo suala zima la kuwajengea uwezo watendaji wake, pamoja na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili waweze kuona kasoro na kuchukua hatua zinazofaa katika kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wa shughuli za kawaida za Wizara hii.
Mheshimwa Spika, baada ya maelezo hayo machache sasa naomba kutoa maoni ya Kamati ya mawasiliano na Ujenzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Hotuba hii ya maoni ya Kamati, itagusa baadhi ya maeneo ambayo Kamati yetu imehisi kuwa hatuna budi kuyatolea maelezo. Maeneo hayo ni kama yafuatayo;
UWAJIBIKAJI WA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, kufanya kazi kwa kujituma na kwa ubunifu ni suala muhimu sana katika kufikia malengo ya tasisi yoyote ile, kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia wafanya kazi wengi wa taasisi za umma wakifanya kazi kwa mazoea bila ya kujali ni kwa kiasi gani wanaweza kufikia malengo ya kazi zao kwa mujibu wa muongozo na mwelekeo wa taasisi hizo. Mheshimiwa Spika, hali hii inajitokeza kutokana na ukweli kwamba wafanyakazi wengi wa taasisi za umma hufanya kazi katika hali ya utaratibu wa kawaida tu yaani ‘daily rootine’ bila ya kuwa wabunifu na kuzingatia mipango na miongozo maalum ya kazi kama vile mipango kazi (action plans), sera (policies), na dira (vision) za taasisi za Wizara wanazozifanyia kazi, hali hii hupelekea kutokuwepo kwa ufanisi wa kazi hizo. Aidha, wafanyakazi hushindwa kujitathmini wao wenyewe namna wanavyozisaidia taasisi zao ili ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ya taasisi hizo. Aidha Kamati yetu inazidi kusisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa na Serikali na inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi za kukemea tabia hizo na kuwataka watumishi wa umma wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazowea ili kuleta mabadiliko katika sekta zote na wananchi waweze kunufaika na huduma za taasisi hizo.
MAFUNZO KWA WAFANYA KAZI
Mheshimiwa Spika, Suala la kuwajengea uwezo wafanyakazi ni muhimu sana katika kukuza ufanisi na uwezo wa watendaji. Kamati yetu inapenda kuiomba Wizara izidishe juhudi zaidi za kuwapatia mafunzo wafanyakazi wake, mafunzo ambayo ni muhimu sana katika kukuza uelewa na kuwajengea uwezo wa kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa. Aidha Kamati yetu inaipongeza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kuweza kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wapatao 84 kwa mwaka 2011/2012 katika vyuo mbali mbali, ndani na nje ya nchi pamoja na kuwapatia mafunzo ya muda mfupi wafanya kazi wapatao 91 .
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inasomesha wafanyakazi wake kwa lengo la kupata wataalamu katika sekta husika, ni vyema kukawekwa mikakati maalum kuhakikisha kuwa wafanya kazi hao wanapomaliza masomo yao wanarejea kuitumikia Serikali hasa katika taasisi zao walizotoka. Ili kuwabana watendaji hao wanaosomeshwa na Serikali kurudi kufanya kazi katika taasisi zao za awali ni vyema Serikali ikazingatia kuwapatia wafanyakazi maslahi yanayoendana na utaalamu wao baada ya kumaliza masomo yao.
IDARA YA MIPANGO, SERA, NA UTAFITI
Mheshimiwa Spika, pamoja na malengo iliyojiwekea Wizara, Kamati inasisitia haja ya kuwepo kwa chombo cha kusimamia ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini na kitakachoratibu uhalali wa bei za umeme na maji. Pia Kamati inaitaka Wizara kuharakisha nia yake ya kuweka sheria ya tathmini ya ardhi na majengo na kupatikana kwa taasisi hiyo.
Mheshimiwa Spika, sheria inayohusu uhaulishaji ardhi au mali isiyohamishika bado ina mapungufu na ni moja kati ya chanzo cha migogoro. Wizara inapaswa iliangalie upya na kuona haja ya kufanya marekebisho ili kuepusha migogoro na kupatikana kwa uadilifu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuandikwa lengo la kufikisha umeme katika vijiji vilivyokosa huduma hiyo, Idara inapaswa isimamie ufikishaji umeme huo vijijini badala ya suala hilo kubakia kwenye maandishi tuu.
IDARA YA UTUMISHI NA UENDESHAJI
Mheshimiwa Spika, kwa vile Idara hii ndiyo inayoshughulika na maslahi ya wafanyakazi, Kamati inaitaka Wizara kupitia Idara hii kuendeleza mawasiliano na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora kutatua tatizo lililojitokeza hivi sasa la baadhi ya watumishi wa ngazi ya chini wa Wizara hii kutofaidika na nyongeza ya mishahara iliyoanza kulipwa mwezi wa Oktoba, 2011.
IDARA YA ARDHI NA USAJILI, MIPANGO MIJI NA VIJIJI NA IDARA YA UPIMAJI NA RAMANI.
CHANGAMOTO ZA IDARA
MIGOGORO YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, moja kati ya matatizo sugu katika nchi yetu ni suala la migogoro ya ardhi ambapo mara kwa mara imekuwa ikiibuka katika sehemu mbali mbali. Miongoni mwa migogoro hiyo ni pamoja na kuchukuliwa kwa baadhi ya maeneo ya wananchi kwa mabavu, kufutiwa hati kwa baadhi ya wawekezaji bila ya kufuata taratibu za sheria ya umiliki wa ardhi. Vilele vile kuna baadhi ya wawekezaji hufutiwa hati za ardhi na kupewa wawekezaji wengine bila kuzingatia taratibu za kisheria. Mheshimiwa Spika, iwapo hali hii itaendelea inaweza kupelekea wawekezaji kutokuja nchini kuwekeza na hivyo kutuletea athari kubwa ya kiuchumi. Aidha kwa upande mwengine kumekuwa na shutuma kwa baadhi ya Masheha, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhusika kwa namna moja ama nyengine katika migogoro hii, pia inawezekana kuna baadhi ya watendaji wa Serikali wachache wasio waaminifu kuhusika katika kadhia hii. Hali hii inajitokeza kutokana na ukweli kwamba ardhi imekuwa ni rasilmali muhimu na ambayo thamani yake inaongezeka siku hadi siku, hivyo baadhi yao wamekuwa wakijenga tamaa ya fedha na kukuika maadili ya kazi zao.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inasisitiza kuwa pamoja na ahadi nyingi zinazotolewa na Serikali kuhusiana na utatuzi wa suala la migogoro ya ardhi, ipo haja kwa Serikali yetu kuwawajibisha wahusika wote wanaotumia nafasi zao kinyume na ilivyokusudiwa wakiwemo baadhi ya viongozi wa Serikali na watendaji wote wanaohusika na kadhia hiyo. Hatua hiyo italeta matumaini kwa wananchi walio wengi ambao wamekumbwa na suala la migogoro ya ardhi na wamekata tamaa kwa sasa.
UJENZI HOLELA
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia kuendelea kwa ujenzi holela ambao hauzingatii mipango maalum na mahitaji ya baadae “Master Plan” Kumekuwa na wimbi kubwa la uvamizi wa maeneo ya kilimo na maeneo mengine ya wazi, ambayo yanavamiwa na kujengwa majengo ya biashara na makaazi. Kamati yetu inatoa wito kwa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ya wazi hayatolewi kwa ajili ya shuguli za biashara na makaazi.
Mheshimiwa Spika, Kwakuwa nchi yetu ni kisiwa na haina eneo kubwa sana la ardhi, ni vyema kwa Serikali ikalizingati hilo kwa kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi. Ardhi ni raslimali muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi iwapo itatumika vizuri, hivyo ipo haja kwa Serikali kujiwekea mipango mizuri katika kuhakikisha inatenga maeneno maalum kwa ajili ya kilimo, maeneno ya uwekezaji na maeneno ya makaazi ya wananchi, kinyume na hali ilivyo hivi sasa ambapo hakuna utaratibu maalum wa kudhibiti hali hiyo. Iwapo ardhi haitotumika vizuri inaweza ikawa ni sababu ya kuliingiza taifa letu katika umasikini kwa kukosa kuweka maeneno maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupima maeneo na kugawanywa kwa wananchi na taasisi bila kupeleka miundombinu siyo tu inazorotesha maendeleo ya ujenzi bali pia inachangia katika uvamizi wa maeneo ya njia na sehemu za wazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukaribu wa kazi zinazofanywa na Idara tatu hizi ambazo ni Idara ya Ardhi na Usajili, Idara ya Mipango Miji na Vijiji na Idara ya Upimaji na Ramani, Kamati inatoa msisitizo kuwa ile fikra ya kuziweka chini ya mwamvuli mmoja Idara hizi zikawa kama “Kamisheni” iharakishwe ili ziweze kufanya kazi kwa mashirikiano na kurahisisha kazi za Idara hizo kwa kuwahudumia wananchi kwa wakati na hatimaye kupunguza migogoro ambayo imekua ikiibuka na kuongezeka kila siku.
Mheshimiwa Spika, Kamati pale inapoamua kukutana na Idara zote tatu kwa pamoja umuhimu wa kufanya hivyo huonekana ambapo maafisa kutoka katika Idara hizo walishirikiana kujibu hoja za Wajumbe na kutoa rai zao ambazo ni za msingi katika kuziimarisha taasisi hizo, na kupelekea Kikao hicho kwenda kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa vile Wizara hii kupitia Idara tatu hizi ndiyo inayogawa maeneo ya ujenzi wa nyumba, viwanda, mahoteli na mengineyo, na kuwa ni dhamana wa kufuatilia ripoti ya tathmini ya mazingira (Environmental Impact Assessment- E I A) ni dhahiri kuwa Idara ya Mazingira mahali pake ni hapa. Kwa vile Idara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo wanafuatilia Mazingira ya baharini na maeneo ya kilimo, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais ingepewa jukumu la uratibu wa mazingira yote kwa ujumla.
MAHAKAMA YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, Bado tunakabiliwa na tatizo la mrundikano wa kesi za ardhi hususan katika kisiwa cha Unguja, Wakati Kamati yetu ikipitia bajeti ya Wizara ilielezwa kuwa kati ya kesi 95 zilizofunguliwa Unguja kati ya Julai hadi Machi 2012 ni kesi 15 tu ndizo zilizotolewa hukumu, hali hii inatokana na uchache wa Mahakimu katika mahakama hizo, ili kuondokana na tatizo hilo Kamati yetu inashauri Wizara ichukue hatua za dharura kwa kuiombea Mahakama ya Ardhi iongezewe Mahakimu pamoja na kufungua Mahakama za Ardhi za Mikoa.
Aidha, Kamati yetu inaiomba Wizara katika Bajeti ya 2012/2013 iangalie uwezekano wa kuwajengea mazingira bora ya kimaslahi watendaji wa Mahakama ya Ardhi kutokana na unyeti wa majukumu yao, ni vyema watendaji hawa wakajengewa mazingira bora ya kimaslahi ili kuepusha uwezekano wa kuchukua rushwa wakati wa kutekeleza kazi zao.
IDARA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika, Ili kukuza uchumi wa nchi yetu suala la kuwepo kwa nishati ya uhakika ya umeme ni suala la lazima, na hatuwezi kuendelea bila ya kuwa na nishati ya uhakika, moja kati ya vitu vya msingi ambavyo wawekezaji huangalia kabla ya kuekeza ni kuwepo kwa nishati ya uhakika. Kwa muda mrefu sasa nchi yetu imekosa umeme wa uhakika na ambao hautoshelezi mahitaji yetu ya kawaida. Katika hali kama hii athari yake ni kupoteza fursa nyingi za wawekezaji kuja kuekeza katika nchi yetu, hususan katika sekta za viwanda sekta ambayo kimsingi huhitaji kuwepo kwa nishati ya umeme ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imefarajika kusikia kwamba, ripoti ya wataalamu wa Jumuiya ya Ulaya ‘European Union’ (EU) kuhusu uwezekano wa Zanzibar kuzalisha nishati mbadala, inayoonesha kwamba, Zanzibar inaweza kuzalisha umeme mbadala kwa kutumia upepo, takataka na jua. Kamati yetu inaishauri Serikali kuifanyia kazi ripoti hiyo ya wataalamu kuhusu njia muafaka kwa uzalishaji wa umeme ili kuharakisha mchakato wake wa kupatikana kwa nishati mbadala ya uhakika na ambayo itakuwa ina gharama nafuu ili kuwapunguzia ugumu wa maisha wananchi kwa kuwa hali ya hivi sasa sio nzuri ambapo bei ya nishati hiyo iko juu na inazidi kupanda siku hadi siku.
NISHATI YA MAFUTA
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imefarajika na taarifa ya Idara ya Nishati kwamba kwa hivi sasa masuala yanayohusu nishati yatasimamiwa moja kwa moja na Idara hiyo badala ya kusimamiwa na Wizara ya Fedha. Aidha, tumefarijika kupata taarifa kwamba Wizara inaandaa Rasimu ya Sheria ya usamabazaji wa Mafuta (Zanizbar Petroleum Supply Act), pamoja na Sheria ya udhibiti wa mafuta, ili bidhaa ya mafuta iweze kusimamiwa na sekta husika kwa ufanisi zaidi na kuwa na mdhibiti mahususi wa bidhaa ya mafuta. Kamati yetu inaisisitiza Serikali kuzingatia kuwaandaa watendaji wa Idara ya Nishati kwa kuwapatia mafunzo yanayohusiana na masuala ya Nishati ili kuwaweka tayari na mabadiliko ambayo tunayatarajia likiwemo suala la kuanzisha nishati mbadala pamoja na suala la uchimbaji wa mafuta.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utegemezi mkubwa wa nishati ya umeme hapa Zanzibar kutoka Tanzania bara, Idara hii ina jukumu kubwa la kutafuta mbinu za nishati mbadala. Kutokana na jukumu hilo ambalo lingehitaji utafiti, taaluma na mikakati ya hali ya juu ambayo itaweza kuipeleka nchi katika nishati inayotumia nyenzo tulizonazo na ambayo haiharibu mazingira ( Environmental friendly).
Mheshimiwa Spika, kutokana na bajeti ndogo ya Idara hii, Kamati inaona kuwa dalili za kufikiwa mapema malengo hayo hayapo, hivyo Kamati inaishauri Serikali inapopanga bajeti iangalie na unyeti wa malengo yake kwa kuziwekea bajeti ya kutosha Idara zake ili ziweze kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaendelea kusisitiza kuwa Idara hii ikabidhiwe mambo yote yanayohusu nishati ikiwemo udhamini juu ya uingizaji wa mafuta nchini, pamoja na upangaji wa bei na uhalali wa kuyashughulikia makampuni yanayoingiza na kuuza mafuta ya petroli na mengineyo.
SHIRIKA LA UMEME
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme lingehitaji kufanya marekebisho makubwa katika uendeshaji wake. Ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40 kwa mkupuo si utaratibu mzuri bali kama gharama zimeongezeka za uendeshaji ni vyema kwa Shirika na Serikali kwa ujumla kupandisha bei ya umeme kidogo kidogo kulingana na hali za wananchi zilivyo.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme (ZECO) halina budi kujifanyia tathmini ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuwapunguzia wananchi gharama za kuunganisha na kulipia umeme. Aidha udhibiti wa mapato ya Serikali siyo tu ungeliletea faida Shirika bali pia ungepunguza mzigo kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Shirika halina budi kuweka transfoma za akiba za ukubwa tofauti Unguja na Pemba, ili kuwapunguzia usumbufu wananchi wakati transfoma inapoharibika.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme lina azma nzuri ya kuleta vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuwaungia umeme wananchi, hata hivyo Kamati inasisitiza kuwa jambo hilo lifanywe kwa vitendo na Kamati inafuatilia kwa kina ahadi hiyo ili kuona utekelezaji wake unafanikiwa.
MAMLAKA YA MAJI
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya maji (ZAWA) ni taasisi muhimu sana iliyobeba jukumu la uhai kwa maelfu ya wananchiwa Zanzibar, kwani “MAJI NI UHAI”.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaikumbusha Mamlaka kuchukua tahadhari zote za kiutawala na kiufundi kuhakikisha kuwa maji yanapatikana katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa pump za akiba, mabomba na mafundi stadi ni sehemu muhimu za kutoa huduma hii. Ujenzi wa matangi yanayohimili hali ya hewa yetu kunasaidia sana usambazaji maji badala ya kutumia njia ya moja kwa moja. Hata tathmini ya uwezo wa pump zetu unaweza kufanyika.
Mheshimiwa Spika, ili kufuatilia kwa karibu upatikanaji na ukosefu wa huduma ya maji, Kamati inasisitiza ufungaji wa mabomba ya maji kwa zone maalum katika sehemu za miji na kuunganishwa katika maeneo ya dharura. Utaratibu huu utatoa taarifa mapema “Early warning system” katika maeneo ambayo maji yanakosekana na kujua mapungufu yaliyopo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuipa uwezo Mamlaka ya Maji, Kamati inawaomba wananchi wote wanaopata huduma hii ya maji kulipia huduma hiyo bila ya kuchelewa.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Ili Wizara iweze kutekeleza malengo yake na kutoa huduma safi kwa wananchi nawaomba wajumbe wenzangu tuipokee, kuichangia na baadae kuipitisha bajeti ya Wizara ya T.sh. 80,082,728,000 zikiwemo Tsh. 6,708,000,000 kwa kazi za kawaida na T.sh 73,374,728,000 kwa kazi za Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, sasa napenda kutamka kuwa kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Ziwani, naiunga mkono hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa mwaka wa fedha 2012/ 2013.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
………………………
RASHID SEIF SULEIMAN,
M/MWENYEKITI,
KAMATI YA MAWASILIANO NA UJENZI
BARAZA LA WAWAKILISHI
ZANZIBAR