Pages

Tuesday, July 17, 2012

TAARIFA KWA UMMA Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

TAARIFA KWA UMMA
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kinakanusha taarifa zilizotolewa na gazeti la Kiswahili la kila Jumatano, Mwanahalisi, ambazo zinadai kupitia toleo lake namba 301 la Julai 4- 10, 2012 kwamba kuna ufisadi mkubwa unaodaiwa kufikia Shilingi Bilioni Mbili.

Katika taarifa hiyo isiyokuwa na chembe ya ukweli gazeti hilo linadai fedha hizo ziliibwa kati ya mwaka 2008 na 2012. Kumekuwa na mlolongo wa taarifa za uzushi na uongo kwenye baadhi ya magazeti, likiwemo Mwanahalisi, zenye nia ya kukichafua Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) na viongozi wake wa ngazi za juu. Taarifa hizo,kwa kiasi kikubwa, zimekuwa zikishabikia watu wanaoshukiwa kuhusika na upotevu wa rasilimali za Chuo, ikiwemo fedha.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) hutumia njia mbalimbali zilizoainishwa katika Hati Idhini ya Chuo ya 2007 na kadiri ya sheria husika za nchi kuhusu kutoa taarifa rasmi za mahesabu yake ambayo kila mwaka hukaguliwa na CAG na taarifa ya ukaguzi wa mahesabu ya chuo ya mwaka 2010/11 imeishatolewa na Chuo kimepata hati safi. Taarifa hizo zitapelekwa Bungeni hivi karibuni na hakuna sababu ya mtu mwingine au gazeti kama Mwanahalisi kutengeneza mahesabu ya Chuo nje ya utaratibu huo rasmi ambao ndio unatumika na Baraza la Chuo kusimamia matumizi ya fedha na raslimali zote za Chuo kama msingi wa utawala bora. Mtindohuu wa gazeti la Mwanahalisi kutengeneza mahesabu yake ya Chuo ni uvunjaji wa sheria za nchi nani Kinyume kabisa na matarajio ya uandishi adilifu na una nia ya kuupotosha umma na kushirikiana na mafisadi. Ni matumaini ya chuo kwamba vyombo husika vitachukua hatua mbalimbali kulizuia gazeti hili kuendeleza kuandika uzushi.

Chuo Kikuu Huria Tanzania kinasema kuwa mlolongo wa taarifa zinazochapishwa katika magazeti haya ni za uongo, uzushi na zenye lengo la kuchafua jina zuri la chuo chetu chenye kutoa elimu nafuu na bora ya masafa kwa jamii.

Ni ushauri wetu kwa uongozi wa magazeti husika kuwa endapo watahitaji taarifa sahihi kuhusu uendeshaji wa chuo ni bora kuwasiliana na wasemaji wa chuo katika njia muafaka.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano na Masoko,

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA

Kwa Mawasiliano Zaidi;

Albert Z. Memba, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania S.L.P 23409, Dar es Salaam,Tanzania. Tel. + 255 22 2668445; Fax. + 255 22 2668779; E‐Mail: dcm@out.ac.tz

Popular Posts