Pages

Sunday, July 15, 2012

Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

1. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandaa mikutano ya hadhara katika Jimbo la Iramba Magharibi. Mikutano hiyo ilitolewa taarifa polisi na jeshi hilo lilitoa baraka zake kama utaratibu wa sheria unavyotaka kwa barua yake ya tarehe 12 Julai 2012 Kumb. Na. KIO/B1/1/VOL.V/268

2. Mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika Kata ya Ndago katika viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi ambapo pia ni hatua chache karibu kabisa na Kituo cha Polisi Ndago. Mkutano huu ulipangwa kuanza saa nane mchana.

3. Msafara wa kitaifa unaofanya ziara ya ukaguzi wa chama, katika mkoa wa Singida chini ya uratibu wa Ofisa wa Sera na Utafiti Makao Makuu, Mwita Mwikwambe Waitara, (ikiwa ni maandalizi ya operesheni nyingine kubwa mkoani humo itakayofanyika baadae), uliwasili katika eneo la Mkutano majira ya saa tisa na nusu alasiri. Tulikuta wananchi wengi wakiwa wanatusubiri. Kabla ya Mkutano kuanza tulipewa taarifa kwamba kuna kikundi cha vijana kimeandaliwa kuvuruga mkutano wa CHADEMA kwa kufanya fujo, ikiwemo kurusha mawe ili mkutano huo usifanyike. Suala hilo lilielezwa mkutanoni mapema na Mheshimiwa Waitara, mbele ya askari polisi.

4.
Wakati tukijiandaa kuanza hotuba, vijana wapatao wanane walianza chokochoko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka sehemu mbalimbali. Wakati fujo zinaanzishwa na kile kikundi, Mheshimiwa Waitara alikuwa bado anazungumza na wananchi kuwaandaa kusikiliza wazungumzaji wengine. Vurumai hiyo ilizimwa na wananchi wenyewe wa Ndago waliokuwa na hamu ya kusikiliza ujumbe wa viongozi wa kitaifa wa CHADEMA.

5. Kwa kweli tunawashukuru wananchi wengi wa Ndago walioonesha ujasiri mkubwa kuweza kuwaondoa vijana wale eneo la mkutano, kisha mkutano ukaendelea, huku wananchi wakionesha kila hamasa ya kufurahia hoja kutoka kwa wazungumzaji, akiwemo Mheshimiwa John Mnyika, ambaye aliombwa ahudhurie ziara hiyo kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.

6. Mpaka tunamaliza mkutano huo ambao wananchi waliufurahia sana kwa namna ulivyohutubiwa kwa amani na utulivu huku wazungumzaji wakijenga hoja juu ya mstakabali wa jimbo na taifa lao kwa ujumla, mamia ya wananchi waliohudhuria walitaka tuendelea kuhutubia, lakini tulibanwa na ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, eneo la Kinampanda.

7. Lakini kutokana na vurugu hizo zilizokuwa zikisababishwa na kikundi cha vijana ambao tayari ilishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo, lakini askari waliokuwepo hawakuthubutu kuchukua hatua, tulilazimika kuomba msaada kutoka kwa OCD na R.P.C, ambapo baadae wakati mkutano unakaribia kuisha tuliona gari la polisi kutoka Mjini Singida likiwa na askari waliojipanga rasmi kwa ajili ya kuzuia vurugu likifika pale eneo la mkutano, lakini wakati huo hali ilishatulia na hotuba zimetolewa vizuri.

8. Kutokana na hali hiyo ya vurugu, zilitolewa taarifa Kituo cha Polisi cha Ndago, ambapo lilifunguliwa jalada NDG/RB/190/2012. Katika jalada hilo tulitaja baadhi ya majina ya watuhumiwa waliokuwa vinara wa kundi lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano mbele ya askari polisi. Majina hayo ni; 1. Daniel Sima, 2. Tito Nitwa, 3. Bakili Ayubu, 4. Yohana Makala Mpande, 5. Ernest Kadege, 6. Abel John, 7. Athuman Ntimbu, 8. Martin Manase, 9. James Ernest, 10. Simion Makacha, 11. Anton John, 12. Frank Yesaya

9. Kwa hakika askari polisi wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya kutochukua hatua yoyote dhidi ya fujo tulizofanyiwa ikiwemo kupondwa mawe na kikundi kidogo cha wahuni, fujo zilipozidi askari wote walikimbia eneo la mkutano, akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutotaka kuchukua hatua stahili. Hakuonekana kufanya juhudi zozote za kuhakikisha amani inalindwa na ulinzi unaimarishwa katika eneo la mkutano na hatua zinachukuliwa dhidi ya watu walioonekana kudhamiria kufanya fujo. Mtu yeyote makini angeweza kuona kuwa askari wale walikuwepo pale mkutanoni ‘almuradi’ tu lakini kama vile walikuwa na maelekezo maalum ya kuhakikisha hawachukui hatua yoyote katika kuzuia mpango wowote wa kusababisha vurugu na kuvunja amani.

10. Baada ya kumaliza mkutano wa Ndago kwa amani, tulikwenda Kinampanda ambako tulifanya mkutano mwingine mzuri kwa amani kabisa, ambapo mbali ya wananchi kuwa wametusubiri kwa hamu kubwa na kutusikiliza kwa makini hoja zetu, polisi katika eneo hilo walitupatia ushirikiano mzuri tangu wakati tunafika mpaka tulipomaliza mkutano huo.

11. Jioni wakati tumerudi hotelini, tukasikia kuna taarifa zinasambazaa kuwa kuna mtu/watu wamekufa katika eneo la Ndago. Habari hizo zilikuwa zinakanganya kwa sababu zilikuwa zikitaja idadi tofauti tofauti. Lakini kwa vyovyote vile kama ni kweli kuna tukio la mtu kufariki, CHADEMA tunasikitika sana kwa tukio hilo la uhai wa mtu.

12. Tunalaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinawataja polisi kuwa wanatuhusisha CHADEMA na tukio la mtu aliyefariki. Hii ni ajabu kubwa kwamba tumetoka kwenye mkutano ule kwa amani kabisa mpaka tumemaliza mkutano wa pili kwa amani na polisi wakiwepo sehemu zote mbili, kisha tunasingiziwa masuala ambayo wenyewe hatukuwa na habari nayo tangu mkutano wa kwanza ukiwa unaendelea mpaka mkutano wa mwisho ulipomalizika.

13. Kutokana na habari hiyo ya kifo cha mtu inavyoenezwa kwa kuihusisha CHADEMA, tumebaini kuwepo kwa mbinu na mikakati ya chama tawala pia vyombo vya dola vikihusika kutaka kuwatisha wananchi wa Singida, Watanzania wote wapenda mabadiliko na viongozi wa CHADEMA katika mkoa huu, wasifanye kazi ya kisiasa kwa kuwabambikizia tuhuma na kesi na pia kuwafanya waonekane ni watu wa vurugu.

14. Tunapenda kusema hapa kuwa njama hizo hazitafanikiwa. Zitashindwa kama zilivyoshindwa njama zingine zote ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo vya dola, viongozi wa serikali na chama tawala dhidi ya CHADEMA na vuguvugu la mabadiliko nchini.

15. Tunawataarifu wananchi kuwa ratiba ya kufanya Operesheni nyingine kubwa katika Mkoa wa Singida, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, itafanyika baadae kama ilivyoazimiwa na kikao cha Kamati Kuu.


Imetolewa leo Singida, Julai 15, 2012 na;

Waitara Mwita Mwikwabe

Ofisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu

Popular Posts