Aliyeuawa jana na wafuasi wanaaminika kuwa ni wa Chadema, ametajwa kuwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Ndago, Yohana Mpinga mwenye umri wa miaka 30. Imeelezwa kutoka mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Linus Vicent Sinzumwa amesema leo kwamba, Mpinga amefariki dunia baada ya kupigwa kwa fimbo na mawe, na baadhi ya wafuasi wa Chadema, Julai 14 mwaka huu, saa kumi alasiri katika kijiji cha Ndago.
Alisema siku hiyo Chadema walikuwa na kibali cha kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hicho cha Ndago na mgeni rasmi katika mkutano huo,alikuwa mbunge wa jimbo la Ubongo jijini Dar-es-salaam, John Myika.
Akifafanua,kamanda huyo, alisema mara baada ya Chadema kuanza mkutano huo,viongozi wake walianza kuporomosha kashifa dhidi ya mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba ,kitendo kilichowaudhi baadhi watu waliokuwepo kwenye mkutano huo.
Sinzumwa, alisema watu hao ambao walichukizwa na kitendo cha kukashifiwa mbunge wao,walianza kupiga kelele kuwa hawataki mbunge wao akashifiwe na badala yake wanataka kusikia sera za Chadema tu lakini viongozi hao waliendelea tu kuporomosha kashifa dhidi ya Mwingullu na kusababisha kuanza kwa vurugu.
Alisema kuwa vurugu hizo zilihusisha kundi la wanachama wa Chadema na wa CCM na zilisambaa haraka.Wanachama hao walianza kurusha mawe ovyo na askari wachache wa polisi waliokuwepo,walizidiwa nguvu na makundi hayo.
Amesema, Mwenyekiti wa UVCCM Yohana,yeye baada ya kuona vurugu zinaendelea kukua, akikimbilia kwenye nyumba ya Mwalimu Shume Manase Mpinga ili kuokoa maisha yake hata hivyo, kundi la wana-Chadema wakiwa wamebeba fimbo na mawe,walimpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusbabisha kifo chake papo hapo.
Alisema katika kundi hilo ambalo wamelikamata,watawahoji na wataobainika kuhusika,watafikishwa mahakamani wakati wo wote.
Aidha polisi wamefuta mikutano yote ya Chadema iliyokuwa iendelee katika kijiji cha Shelui na Kiomboi mjini jimbo la Iramba magharibi leo.
-