Pages

Monday, July 16, 2012

Mwita Waitara Mwikabwe Mbaroni kwa mauaji ya Mwenyekiti wa UVCCM

Afisa wa sera na utafiti CHADEMA makao makuu,Mwita Waitara Mwikwabe,(wa kwanza kulia walioketi) akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) la CHADEMA kutohusika na mauaji ya mwenyekiti wa umoja wa vijana (CCM) kata ya Ndago jimbo la Iramba Magharibi.

Afisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Mwita Waitara Mwikwabe (wa tatu kushoto) akitoka nje ya ofisi ya CHADEMA mkoa wa Singida, baada ya kumaliza kutoa tamko la CHADEMA kutohusika na mauaji ya mwenyekiti wa umoja wa vijana CCM kata ya Ndago jimbo la Iramba Magharibi.

Na Nathaniel Limu.

Jeshi la polisi mkoani Singida linamshikilia Afisa wa sera na utafiti wa Chama cha CHADEMA Makao Makuu Waitara Mwita Mwikwabe, kwa tuhuma ya mauaji ya mwenyekiti wa umoja wa vijana CCM (UVCCM) kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi Yohana Mpinga (30).

Kiongozi huyo wa CHADEMA alikamatwa muda mfupi baada ya kumaliza kutoa tamko la chama hicho kutokuhusika na mauajio ya kijana huyo kiongozi wa CCM kwa waandishi wa habari.

Waitara, mbunge wa jimbo la ubungo jijini Dar -es- salaam Mh. John Mnyika na mshauri wa CHADEMA na Mhadhiri wa chuo kiku cha Dar- es- salaam Dk. Kitila Mkumbo, inadaiwa walichochea mauaji hayo kwa kitendo chao cha kumkashifu mbunge wa wa jimbo la Iramba magharibi Mwigulu Lameck Nchemba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Singida Linus Vicent Sinzumwa, kashifa hizo zimetolewa na viongozi hao wa CHADEMA, Julai kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi, pia karibu kabisa na kituo kidogo cha polisi cha Ndago, ambapo viongozi hao wanatuhumiwa kutoa kashifa hizo dhidi ya Mwigullu.

Sinzumwa amesema baada ya viongozi hao kuacha kueleza sera za chama chao na kuanza kumkashifu Mwigullu, baadhi ya wananchi waliwataka kuacha mara moja kumkashifu mbunge wao, lakini viongozi hao walipuunza maombi hayo ya wananchi.

Amedai kitendo hicho kilichochea kutokea kwa vurugu ambazo mwisho wake, ulipelekea kikundi cha wanachama wa CHADEMA kumuuwa Yohana Mpinga kwa kumpiga kwa fimbo na mawe.

Jeshi la polisi lilimkamata Waitara muda mfupi baada ya kutoa tamko kwa waandishi wa habari kuhusu yaliyojiri katika mkutano wa CHADEMA uliofanyika katika kata ya Ndago julai 14 mwaka huuu.

Katika tamko hilo, Afisa huyo wa sera na utafiti, amesema wakati wanajiandaa kuanza hotuba, vijana wanane walianza choko choko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka sehemu mbali mbali.

Amesema kikundi hicho kiliwaogofya wananchi ambao waliondoka katika eneo hilo, lakini muda mfupi baadaye, walirejea na mkutano uliendelea kwa amani na utulivu hadi ulipomalizika.

Katika hatua nyingine, viongozi hao wa CHADEMA, wamelaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinadai kuwa polisi wanawahusisha wao CHADEMA na tukio la mtu aliyeuawa kwenye vurugu zilizotokea Ndago.

Popular Posts