Afisa Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Nd. Juma Kimtu akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Mchango wa Maafa wa Shilingi 10,000,000/- hapo ofisini kwake Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Nyuma yake ni Meneja Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis Phil Phil Than.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea mchango wa Maafa wa shilingi 10,000,000/- kutoka kwa Meneja Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis Phil Phil Than hapo katika Ofisi yake iliyopo Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
---
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wananchi kuendelea kuiamini Serikali katika kupokea Taarifa zake hasa wakati wa kutokea Majanga na Maafa.
Nasaha hizo amezito hapo katika Ofisini yake iliyopo Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akipokewa mkono wa Pole kutoka kwa Taasisi mbali mbali za Umma na Kijamii.
Salamu hizo za mkono wa pole zimetolewa kwa Balozi Seif na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } na ule wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii ya Tanzania { NSSF } ambapo kila moja ilikabidhi mchango wa Shilingi Milioni kumi { 1,000,000/- }.
Balozi Seif alisema Jamii kujenga tabia ya kuiamini Serikali hupelekea kuwepuka kuchanganywa wakati wa kupokea Taarifa hizo kutoka vyombo vya Habari vinavyopokea Baadhi ya Taarifa zisizo rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii Bara na Zanzibar kwa kufikiria jambo hilo muhimu la kutoa mchango ambalo Taifa linahitaji kuungwa mkono katika kukabiliana nalo.
Aliuhakikishia Uongozi wa Taasisi hizo kwamba michango hiyo itasimamiwa vyema kwa ajili ya kuwafika waliohusika kwa kutumia utaratibu uliotumika wakati wa ajali iliyotokea Mwaka jana.
Alisema licha ya zoezi la uokozi kuwa na gharama kubwa lakini Serikali inaendelea kutoa huduma zote za mazishi na usafirishaji wa maiti zinazopelekwa Tanzania Bara ambazo zilipatikana kutokana na ajali ya Meli ya M.V Skagit hapo juzi.
Aliongeza kuwa shughuli hiyo ikiwemo gharama za vyombo, mafuta, Chakula na uokozi zinahitaji kuungwa mkono na taasisi na jumuiya ya kiraia ndani na nje ya Nchi. “ Serikali imeshachukua jukumu la kuzizika zile Maiti zilizoshindwa kutambulika hadi sasa, kuzisafirisha maiti tatu hadi Tanzania Bara pamoja na familia nne wakati maiti moja ya raia wa kigeni bado haijatambulika”. Alifafanua Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo wazamiaji wa Israel walioko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja wameamua kusaidia kazi ya uokozi kwenya Meli hiyo ili kuendelea kutafuta miili ya Watu iliyopotea.
Mapema Meneja Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Ndugu Khamis Phil Phil Than alisema yapo mambo mengi kwenye tukio hilo la Maafa ambayo yanahitajika kupata msukumo kutoka kwa Washirika, Taasisi na Jumuiya za Kiraia. Ndugu Phil Phil alisema mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar umekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yake yaliyolenga zaidi kwenye eneo la Jamii.
Naye kwa upande wake Ofisa Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } kutoka Makao Makuu Mjini Dar es salaam Nd. Juma Kimtu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo imeamua kutoa mchango huo baada ya kuona uzito Maafa yaliyotokea ambayo yameigusa Jamii yote.
Ndugu Kimtu alisema Serikali kwa kuwa ni ya watu haina budi wakati wote kusaidiwa hasa katika masuala ya Majanga na Maafa ambayo kwa kiasi kikubwa huigusa Jamii yote.
Na
Othman Hamisi Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Rais Zanzibar