Pages

Showing posts with label TFF Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Show all posts
Showing posts with label TFF Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Show all posts

Tuesday, September 11, 2012

*MUSSA MGOSI, AYOUB HASSAN WAPIGWA 'STOP' JKT RUVU, TWITE, YONDANI WACHEZAJI HALALI WA YANGA

Musa Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji Musa Hassan Mgosi ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya Uganda.
Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
YANGA DHIDI YA SIMBA KUACHA WACHEZAJI WANNE:-
Kamati imetupilia mbali pingamizi hizo kwa vile hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji juu ya kuvunjiwa mikataba yao.
Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Ikiwa wachezaji hao watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo litafikishwa katika Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
MBUYU TWITE:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 18 (3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji halali wa timu ya YANGA. Hata hivyo, kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo kwa Simba.
KELVIN YONDANI:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kelvin Yondani, hivyo ni mchezaji halali wa timu ya YANGA.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
Toto dhidi ya Kagera Sugar kumsaini Enyinna Darlinton Ariwodo,
Toto Africans ilipinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa upande wake Kagera Sugar, ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Ramadhan Chombo ‘Redondo’
Redondo ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.
Mchezaji David Luhende kusajiliwa Yanga
Yanga ilikiri kutolipa ada ya uhamisho ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana na Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga mwamba benki (bounced cheque). Shauri hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu.
Super Falcon dhidi ya Edward Christopher kusaini Simba
Simba imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo (compensation) kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
Toto Africans dhidi ya Mohamed Soud kusajiliwa Coastal Union
Toto Africans iliweka pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi wa Fair Play, mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono kati ya klabu.
Rollingstone dhidi ya Kigi Makassy kusajiliwa Simba
Simba imetakiwa kuilipa Rollingstone gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na mchezaji huyo kwa kuzingatia kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Super Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija kusajiliwa Coastal Union
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 23, Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia kumhudumia mchezaji huyo.
African Lyon dhidi ya Razak Khalfan kusaini Coastal
Lyon imesema bado ina mkataba na mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Lyon umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union.
Flamingo dhidi ya Kelvin Friday kusajiliwa Azam
Friday ruksa kucheza Azam, lakini klabu hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu kuilipa Flamingo gharama za kuvunja mkataba.
Super Falcon dhidi ya Robert Joseph Mkhotya kusaini African Lyon
Lyon imeagizwa kuilipa Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ambaye imemsajili. Fedha hizo zitalipwa kwa awamu nne kutokana na makato ya mlango yatakayofanywa na TFF. Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF.
Oljoro JKT dhidi ya Othman Hassan kusajiliwa Coastal
Kwa mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa mchezaji huyo na Oljoro JKT unamalizika mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni mchezaji halali wa Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.

Vodacom Tanzania na TFF zasaini mkataba wa udhamini wa ligi kuu kwa miaka mitatu

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom,Rene Meza akimkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi , Said Abeid mkataba wa udhimini wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara,katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom,Rene Meza akimfafanulia jinsi mkataba ulivyo wa udhamini wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ,Said Abeid,katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam,wanaoshuhudia wapili toka kushoto Makamu wa pili wa Rais wa TFF, . Nasibu Nyamlani,Ofisa Mkuu wa maswala ya Sheria wa Vodacom Bw.Wallarick Nittu.
--
. Klabu ya Simba Sports Club ndio bingwa mtetezi.
.Msimu wa ligi kuanza Septemba 15, na kushirikisha timu 14.
. Polisi Morogoro, Tanzania Prisons na Mgambo JKT ni timu mpya katika ligi.
-
Dar es Salaam, 11 Septemba, 2012…….
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) leo limeingia katika mkataba wa udhamini kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, wakati maandalizi ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania yakielekea ukingoni.
Kampuni ya Vodacom imekuwa mdhamini wa ligi kuu kwa miaka mitano iliyopita, na sasa imeingia mkataba mpya wa udhamini kwa miaka mitatu na TFF, mkataba utakao liwezesha shirikisho hilo kupoea fedha za udhamini kwa miaka mitatu.
Ligi kuu ya Vodacom itaanza tarehe 15 ya mwezi huu, ikitarajia kushuhudia michezo 182 ikichezwa katika viwanja mbalimbali na kushirikisha timu 14, zikiwemo timu za Dar es Salaam Young Africans, Kagera Sugar na Simba Sports Club ambaye ndie bingwa mtetetzi wa kombe hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, amesema kuwa kampuni ya Vodacom iko katika mstari wa mbele katika kuunga mkono maendeleo na shughuli mbalimbali za kimichezo ndani ya nchi.
“Wanamichezo wote ni mabalozi wazuri katika nchi. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunawaunga mkono katika kutambua na kukuza vipaji vyao kadri tutakavyo weza,” alisema Meza na kuongeza kuwa, “Kama jina linavyojulikana ligi kuu ya Vodacom, kombe hili linashuhudiwa na mashabiki zaidi ya milioni 10 katika mechi 182 zitakazo chezwa sehemu mbalimbali za Tanzania bara.”

Meza amejivunia kampuni hiyo kuwa wadhmini wa ligi kuu kwa kipindi kingine, na kufafanua kuwa mpira wa miguu ndio unaongoza kitaifa na unapendwa na Watanzania wengi.
Michuano ya mwaka huu itashuhudia timu mpya tatu ambazo ni timu ya Polisi Morogoro, Tanzania Prisons na Mgambo JKT. Mkataba huu umehusisha pande zote ambazo ni kampuni ya Vodacom Tanzania, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kamati ya ligi.

Kwa upande wake makamu wa Rais wa TFF, Nasibu Nyamlani, ameipongeza kampuni ya Vodacom Tanzania akisema kuwa anaamini kuwa maendeleo ya sasa yatalenga zaidi katika kuunga mkono vipaji vipya na vilivyopo ndani ya nchi.

“Kwa niaba ya TFF, napenda kuwashukuru Vodacom Tanzania kwa kuonyesha nia na kuendelea kuunga mkono mpira wa miguu nchini. Nasi tunaahidi kuendelea kuthamini vipaji vya wachezaji wetu na kuhakikisha tunapata mafanikio zaidi,” alisema Nyamlani.
Mwisho …

Friday, August 31, 2012

17 WAWEKEWA PINGAMIZI USAJILI WA LIGI KUU TZ BARA

Klabu mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.

Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.

Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.

Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.

Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.

Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.

Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.

Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.

Monday, July 23, 2012

TFF YATUMA PONGEZI KWA UONGOZI MPYA WA DOREFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Julai 21 mwaka huu).

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DOREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Dodoma.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya DOREFA chini ya uenyekiti wa Nasoro Kipenzi ambaye amechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Dodoma kwa kuzingatia katiba ya DOREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya DOREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika hoteli ya Dear Mama ni Nassoro Kipenzi (Mwenyekiti), Thadeo Kaliza (Makamu Mwenyekiti), Stewart Masima (Katibu Mkuu), Kepha Maswaga (Mhazini), Mulamu Ngh’ambi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Mohamed Aden (Mwakilishi wa Klabu TFF), Zawdi Kassim (Mjumbe Kamati ya Utendaji).

TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA MTANGAZAJI JOSEPH MAPUNDA

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mtangazaji wa michezo wa Radio Wapo, Joseph Mapunda kilichotokea jana asubuhi (Julai 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Mapunda alifanya kazi na TFF kwa kuripoti shughuli zetu nyingi za mpira wa miguu, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mapunda, Radio Wapo na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mapunda mahali pema peponi. Amina

Popular Posts