Pages

Showing posts with label Katiba - Constitution. Show all posts
Showing posts with label Katiba - Constitution. Show all posts

Monday, January 7, 2013

CCM , CUF NA CHADEMA Vyawasilisha Maoni Yao Tume ya Mabadiliko ya Katiba



Mmoja wa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Andrew Chenge akiwasilisha maoni ya chama chake kuhusu Katiba Mpya katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo Januari 7, 2013 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akifafanua jambo kuhusu mfumo wa uchambuzi wa maoni ya wananchi kwa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliofika katika ofisi za Tume kuwasilisha maoni ya chama hicho kuhusu Katiba Mpya leo Januari 7, 2013:. Viongozi hao pia walipata fursa ya kutembelea Kitengo cha Taarifa Rasmi (Hansard) na Kitengo cha Utafiti. Kulia kwa Mwenyekiti ni Katibu wa Tume Assaa Rashid na kushoto ni Mwenyekiti wa CUF Prof. Lipumba.
  Mmoja wa Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya chama chake kuhusu Katiba Mpya katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Jumatatu, Jan 7, 2013) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
 Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (kulia) wakiongozwa na Dkt. Salim Ahmed Salim wapokea maoni kuhusu Katiba Mpya kutoka kwa uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ulioongozwa na Mwenyekiti wake Ndg. Freeman Mbowe katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam leo Januari 7, 2013
 Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba akiwasilisha maoni ya chama chake kuhusu Katiba Mpya mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Jumatatu, Jan 7, 2013) katika Ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Warioba na kulia kwa Prof. Lipumba ni Katibu wa Tume Assaa Rashid.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Ibrahim Lipumba mara baada ya chama hicho kuwasilisha maoni yake kuhusu Katiba Mpya kwa Tume jijini Dar es Salaam leo Januari 7, 2013.

Sunday, November 11, 2012

MKUTANO WA TAFITI KUHUSU JINSIA NA MASUALA YA UUNDWAJI WA KATIBA 2012 WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM


 Jaji wa mahakama kuu ya Tanzani, Sivangilwa Mwanges (kushoto)akikata utepe kuzindua kitabu cha utafiti kuhusu jinsia na mifano bora katika masuala ya uundwaji wa katiba ya 2012 tafiti kutoka nchi za Ghana, Kenya ,Rwanda,na Afrika ya kusini.mara baada ya kufungua mkutano huo wa siku mbili (kulia)mwenyekiti wa jukwaa la jinsia , Magdalena Rwebaugira.
Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania, Sivangilwa Mwangesi (kulia) akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa mkutano wa utafiti kuhusu jinsia na mifano bora katika masuala ya uundwaji wa katiba ya 2012 tafiti kutoka nchi za Ghana, Kenya ,Rwanda,na Afrika ya kusini mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwenye ukumbi wa karimjee jijini Dar es saalaam ulioshirikisha makamishna wa tume ya katiba,na wajumbe kutoka nje ya nchi ulioandaliwa na chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TWLA) kushoto mwenyekiti wa jukwaa la jinsia (GFC) ,Magdalena Rwebaugira.
Baadhi ya wanachama wa jukwaa la jinsia na katiba wakiwa katika mkutano wa uzinduzi wa utafiti kuhusu jinsia na mifano bora katika masuala ya uundwaji wa katiba ya 2012
Baadhi ya wanasheria wakimsikiliza kwa umakini Mwenyekiti wa jukwaa la jinsia (GFC) (watatu kulia), Magdalena Rwebaugira mara baada ya kuharishwa kwa mkutano huo wa utafiti kuhusu jinsia na mifano bora katika masuala ya uundwaji wa katiba ya 2012.
Mjumbe wa tume ya kuregebisha Sheria, Maria Kashoda akichangia mada kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba akichangia mada kwenye mkutano huo

Friday, October 19, 2012

Wakazi Wa Iringa, Waendelea Kutoa Maoni Kuhusu Katiba Mpya

Heny Mkenja, akijaza fomu maalumu ya maoni ya katiba mpya 
Baadhi ya wakazi wa Iringa ,kata ya Mivinjeni wakifatilia maoni ya wenzao kwa makini
Christina Mgongolwa, mkazi wa kata ya mivinjeni amependekeza kwamba katika katiba mpya ijayo,somo la maarifa ya nyumbani lipewe mhimu wake

Monday, September 10, 2012

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki Atembelea Ofisi ya Tume ya Katiba Zanzibar

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki, akiwa nje ya Jengo la Ofisi ya Tume Maisara, baada ya kuzitembelea Ofisi hizo kuona ,maendeleo yake.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki akizungumza na Katibu wa Tume na Msaidizi wake baada ya kumaliza kutembela Ofisi hizo za Tume Zanzibar.
Katibu wa Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Tanzania Assaa Rashid, akitowa maelezo kwaNaibu Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania alipofanya ziara ya kutembelea Ofisi za Tume Zanzibar.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Angellah Kairuki, akizungumza na Maofisa wa Tume ya Mabadfiliko ya Katiba Tanzania alipokuwa akitembelea Ofisi za Tume zilioko Zanzibar katika Jengo la Mfuko wa Barabara Maisara Zanzibar.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Angellah Kairuki, akitembelea Ofisi za Tume zilioko katika jengo la Mfuko wa Barabara Maisara kuona maendeleo ya Ofisi hizo zinaliopo Zanzibar.akiwa na Maofisa wa Tume ya Marekebisho ya Katiba Tanzania.(kushoto) Katibu wa Tume Assaa Rashid.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah KKairuki, akizungumza na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tamzania Assaa Rashid alipofika katika Ofisi za Tume hiyo zilioko Zanzibar katika maeneo ya Maisara katika Jenjo la Mfuko wa Barabara Zanzibar.

Thursday, September 6, 2012

JUKWAA LA KATIBA LALAANI MAUAJI YA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI

TAMKO LA JUKWAA LA KATIBA TANZANIA DHIDI YA MAUAJI YA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI
‘‘Mauaji Ya Waandishi Na Wananchi YatavurugaMchakato Wa KupataKatiba Mpya Tanzania!’’


JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumepokea taarifa za kuuawa kinyama kwaMwandishi Daudi Mwangosi wa Channel 10na Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC) kwa mshtukona masikitiko makubwa. Kama ilivyokwishaelezwa na wengi, kifo cha mwandishi huyu ni cha kwanza cha aina yake katika tasnia ya habari nchini na kinatishia si tu uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa habari kwa ujumla wake, bali pia kifo hiki na vingine vya siku za karibuni vinauweka mchakato wa Katiba Mpya njia panda.

Vitendo vya mauaji ya raia vinazidi kushamiri siku hadi siku. Wapo wananchiwanaouawa na watu wanaoitwa wenye hasira kali kwa tuhumaza uhalifu. Wapo raiawanaouliwa na majambazi na wahalifu wenginekwa sababu ya ulinzi duni katika maeneowanayoishi. Aidha, wapo pia wananchi wanaopoteza maisha yao kila siku kwa tuhuma za kwamba ni wachawi.Ukiacha hao, idadi kubwa ya watanzania wanaishi na ulemavu wa ngozi wamepotezamaisha kwa kukatwa viungo au kuuliwa kabisa kwa imani za kishirikina.

Hali sasa imefikia kuwa mbaya hadi kuna watanzania wanajisikia salama zaidi wakiwa mwituni kuliko majumbani. Yote haya yanasikitisha sanakwa ujumla wake! Haki ya kuishi inayowekwa na kulindwa na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzakuingia dosari katika Tanzania.Ukiacha mauaji yanayofanywa na watu wasiojulikana au miongoni mwa raia, yamekuwepo pia mauaji yanayozidi kuongezeka ya raia yanayofanywa na wawekezaji au matajiri nchini. Zipo kesi kadhaa za mauaji ya namna hii.

Hayo nayo yamekuwa yakitokea kwa sababu ya ulinzi mdogo ambao wananchi wanao kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini. Jeshi la Polisi, ambalo ndio lenye dhamana ya kulinda watu na mali zaohaliwezi kukwepa lawama katika aina zote hizo za mauaji. Itakumbukwa pia kuwa ajali za magari, mabasi na meli zinagharimu sanamaisha ya watanzania katika siku za karibuni. Kwa kiasi fulani, hata kukithiri kwa ajali hizi nako kunahusishwa na mwenendo mbovu wa usimamizi wa vyombo vya usafiri unaofanywa na idara mbalimbali za serikali ikiwemo kikosi cha usalama barabarani. Roho zawatanzania zinazidi kupotea kutokana na udhaifu mkubwa unaosababishwa na rushwa na mambo mengine ya ukosefu wa maadili katika vyombo vya usimamizi wa haki. Mauaji ya raia yanayofanywa moja kwa moja naaskari wa Jeshi la Polisi nayo yanazidi kuongezeka sanakiasi cha kutishia amani na utulivu wa nchi yetu. Aidha, mauaji yanayohusishwa na siasa nayo yanazidi kuongezeka na kuzidisha chuki ya kisiasa ambayo ni mbaya sana kwa ustawi wa nchi yetu. Kwa mfano katika miezi ya Karibuni, kumekuwepo matumizi ya nguvu kuzidi kiasi kwa raia wanaokuwa wakipanga na kufanyamaandamano au mikusanyiko yenye lengo la kujadili au kupinga jambo fulani. Matokeo yake, kumetokea majeruhi na mauaji ambayo
yamesababishwa na vurugu ambazo zinatokana na Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo halali vya wananchi. Kwasababu hiyo, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunatoa witoufuatao kwa Jeshi la Polisi na idara nyingine za serikali zenye dhamana ya kulinda usalama wa raia, malina mipaka ya Nchi yetu:

1.1. Jeshila Polisi liache kutumia nguvu kuzidi kiasi katika matukio yote ya kulinda mikutano na matukio ya hadhara. Tujuavyo sisi, Jeshi la Polisi linalotumia risasi za moto, mabomu ya kivita, maji ya kuwasha na gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia ambao hawajabeba hata fimbo za kuchungia mifugo. Ni Jeshi lisilojiamini na linaloonesha woga wa ajabu. Kwa hadhira kama za Nyololo, Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam na nyinginezo miezi yaKaribuni, Jeshi la Polisi lingeweza kuwatuliza wananchi kwa kutumia filimbi tu. Matumizi ya nguvu na kumwagia maji ya kuwasha hata wazee wastaafu wanaodai haki zao inaweza kuwa ndio laana inayopelekea Polisi kusikia furaha kuua kila mara. Ipo kanuni ya kimataifa inayowataka Polisi kutumia nguvu kidogo sana inayolingana tu na nguvu ya umma wanaokabiliana nao katika kutuliza ghasia.

2.Wakati huu wa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Tanzania na hata baada ya hapo, Jeshi la Polisi lijiepushe kuingilia shughuli za Kisiasa kwa kuziunga mkono au kuzivuruga. Mikusanyiko mingi ambayo imepelekea mauaji wakati polisi ikijaribu kuivunja ni matukio yaliyolenga kupata majibu ya kisiasa na siyo ya kipolisi. Wajibu wa Jeshi la Polisi
katika wakati kama huo ni kulinda na kuwezesha wananchi husika kueleza madaiyao kwa uhuru na bila kuvurugwa na kundi jingine lolote la watu wasiopendezwa na madai ya kundi husika. Tabia inayozidi kushamiri ya Jeshi la Polisi kutaka kujibu au kuzima hoja za Kisiasa au kiuchumi kwa mtutu wa bunduki, mabomu, maji ya kuwasha na virungu ni tabia ya Jeshi kutaka kuingilia kazi isiyo yake na ndio maana inawashinda. Aidha, kama Polisi wangekuwa niwataalam wa Siasa, wangegundua kuwa wanachokifanya ni kuahirisha matatizo na si kuyatatua!

3. Jeshi la Polisi na vyombo venye dhamana ya ulinzi vijitambue upya kuwa vina wajibu wa kulinda raia, mipaka na mali zao si vinginevyo. Mauaji yanayoendelea nchini ni uporaji wa haki ya kuishi na haki nyingine nyingi chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniana ile ya Zanzibar.Aidha, Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha na kudumisha ustawi wa wananchi kwa mujibu wa ibara ya 8 (1) (b) nahawana mamlaka ya kuua raia. Ikumbukwe kuwa mamlaka yote kikatiba katika Tanzaniayako kwa wananchi na serikali pamoja na Jeshi lake la Polisi watapata madaraka na mamlaka hayo kutoka kwa Wananchi. Nani amewapa Polisi mamlaka ya kuua watanzania? Nani amewapa Jeshi la magereza mamlaka ya kuwapiga na kumwaga damu za Waandishi? Nani amewapa askari wanyamapori mamlaka ya kupiga risasi hovyo nakuua ng’ombe mbele ya wenye maliyao?

4.Athari za matukio ya mauaji na fujo zinazosababishwa na Jeshi la Polisi kutawanya waandamanaji au mikusanyiko mingine ni kubwa sana katika kuathiri vibaya hamasa ya wananchi kwenye Mchakato wa Katiba. Mpaka sasa, tayari watu wengi wameingia wasiwasi na wameamua kutoshiriki mikutano ya kutoa maoni ya Katiba inayoendeshwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini. Endapo Jeshi la Polisi halitaacha kuua na kutishiaraia kwa kila wanachokifanya, mchakato wa Katiba utavurugika kabla Katiba mpya haijapatikana. Kwa mwenendo wa sasa, Jeshi la Polisi litakuja kupiga mabomu na kuua hata wananchi watakapokuwa katika Mabaraza ya Katiba wakijadili na kupinga baadhi ya vipengele vitakavyoingizwa katika rasimu ya Katiba. Pia, itafika wakati wananchi watataka kuandamana kwa amani kuunga mkono au kupinga mambo Fulani katikaKatiba. Kwa hali ilivyo, Jeshi la Polisi litaona hiyo ni fursa ya kutumia mabomu na risasi kuzuia wasiseme wanayotaka kusema. Hii ni hatari kubwa sana!

5. Mikusanyiko, maandamano na shughuli za mikutano ya Siasa ni matendo halali na haki ya kila mtanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 ibara ya 8, 20 na 21. Suala la kutoa taarifa kwaJeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Polisi ni suala la kuwajulisha tu kwa lengo la kuwaweka tayari endapo kutahitajika msaada wa Jeshi la Polisi wakati wa shughuli kamahiyo. Tabia iliyoota mizizi ya Polisi kujiona kama wamepewa taarifaili watoe au kukataa kibali ni uelewa finyu wa Katiba na sheria za Nchi. Ipo haja ya kuongeza uelewa wa wasimamizi wetu wa sheria ili wawe na uelewa mpana wa sheria na ibaraza Katiba wanazozisimamia badala ya kujiona kama wana wajibu wa Msajili wa vyama vya Siasa wa kuratibu shughuli za vyama. Mikutano, mikusanyiko, mihadhara, maandamano na mijadala ni haki ya Kikatiba ya Kila mtanzania binafsi na kwa makundi. Kwa kuwa haki ya kuishi iliyoporwa kwa MwandishiDaudi Mwangosi ndio haki kubwa kuliko zote, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunataka jambo hili lisiishiekuunda Tume za uchunguzi pasipo kufanyia kazi mapendekezo yake. Aidha, kwa kuwa uchunguzi unaofanywa hauhusiani na kilichomuua ndugu Mwangosi wala kundi gani limemuua, tunapendekeza busara itumike kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, kuanzia Kamanda wa Polisi Mkoawa Iringa kuachia ngazi ili kupisha uchunguzi huru wa Tume itakayoundwa na Mheshimiwa Rais ikihusisha na kuongozwa na mhimili wa Mahakama. Taarifa ya uchunguzi ipelekwe Bungeni na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kujadiliwa na ushauri wa kibunge. Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi tunaitamka rasmi kuwa batili kwa kutumia kanuni ya sheria za kiasili inayosema kuwa mtu au kundi hawezi kuwahakimu wa kesi inayomhusu mwenyewe. Bila kufanya hivyo, tunapata wasiwasi kama Tume ya namna hiyoinaweza kufanya kazi yake kwa uhuru. Kuachia ngazi kwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa kutakuwa ishara kuwa Jeshi la Polisi linahitaji kuwa makini zaidi katika kufanya kazi yake ya kulinda amani, mali na maisha ya watanzania. Kwa sasa, zipo hisia kuwa Jeshi la Polisi lipo juu ya sheria na Katiba, jamboambalo tunapenda kulikanusha vikali!

Mwisho, tunapenda kutoa rai kwa serikalikutangaza rasmi kuwa itachukua jukumu la kutunza, kusomesha, kulisha na kuhudumia familia aliyoiacha Daudi Mwangosi kuanzia sasa kwa muda wa miaka 20 watakapoweza kujitegemea wenyewe. Itakuwa ni fedheha kuiona familia aliyoianzisha Marehemu Mwangosi ikisambaratika kwa sababu kichwa cha nyumba hiyo kimesambaratishwa na bomu la Polisi ambalo kodi yake Mwangosiilichangia kulinunua. Kufikia hapa, tunapenda kutangaza rasmi kuwa msiba huu nimsiba wa KIKATIBA na tunaomba ufahamike hivyo kwa umma wote wa watanzania na kote duniani.

Mungu ailazeroho ya Marehemu Mwanahabari Daudi Mwangosi mahali pema peponi Amina!

Imetolewana kusainiwa kwa niaba ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA,
Deus MKibamba
Mwenyekiti
Alhamis, 06 Septemba 2012

Monday, August 27, 2012

MAONI KUHUSU KATIBA MPYA

Maoni yangu kwa leo kuhusu katiba yetu ijayo.

SUALA LA DINI
Amani yetu tuliyo nayo katika Tanzania inachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya katiba yetu ya sasa kutamka waziwazi kuwa serikali kuwa haina DINI.KUINGIZA VIPEGERE VYA AINA YEYOTE VINAVYOZUNGUMZIA DINI KINYUME NA ILIVYO SASA ITATULETEA MGOGORO NA MAFARAKANO.

Katiba mpya ibaki kama ilivyo sasa katika suala la dini. nalisema hili baada y...
a kuona machapisho yakishawishi masuala ya dini yaingizwe kwenye katiba mpya ikiwemo sheria mabalimbali za kidini kuingizwa kwenye katiba kwa kutamka wazi kutambuliwa na katiba na ama kuwa na uwakilishi wa dini katika BUNGE, Hali hii isikubalike hata kidogo kwani kwa zaidi ya miaka 50 tangu tumepata uhuru tumeweza kuishi kwa amani kwa vile tu serikali yetu haikujihusisha na dini za watu bali kuwapa uhuru wa kuabudu kila mtu kwa kadri ya imani yake ili mradi havunji sheria.

MUUNGANO
Kumekuwa na manuguniko ya muda mrefu ndani ya muungano wetu ya baadhi ya watu ndani ya muungano kudhani kuwa hawatendewi haki sawa sawa na upande mwingine wa muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maoni yangu ili kuondoa hali hii, nashauri muungano wetu ufuate mfumo wa USA (Marekani), yaani tuwe na majimbo, jimbo la Tanganyika na la zanzibar then tunakuwa na Rais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania atakayeongoza serikali moja ya pande zote hizi, kwa upande mwingine majimbo haya mawili yaongozwe na magavana. nadhani wataalamu mtakuwa mmenielewa.

BUNGE
Tangu tumepata uhuru tumekuwa tukiambiwa kuwa nchi yet ni ya wakulima na wafanyakazi, kwa kipindi sasa makundi haya yanayozalisha na kutegemewa kuinua uchumi wa nchi hii yamekuwa hayasemewi au haywakilishwi ipasavyo bungeni japo ni makundi makubwa ambayo siyo lazima yafungamane na chama chochote cha siasa.

Maoni yangu tuwe na uwakilishi wa wafanyakazi angalau wawili bungeni watakaochaguliwa na wafanyakazi wenyewe kupitia vyama vyao vya wafanyakazi, ili kupata wakuwasemea na kupunguza MIGOMO NA MIGOGORO ILIYOPO.

NA AARON

Friday, August 17, 2012

Wanahabari washiriki semina elekezi kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya katiba mpya

Mwandishi Mkongwe hapa nchini,Mzee Phill Karashani ambaye aliwahi kupata tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya Habari mwaka 2011,katika tuzo ya Wanahabari Bora wa Mwaka 2011,akifafanua jambo kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya iliyowahusu Wanahabari/Wachora Katuni na wadau wengine mbalimbali iliyofanyika kwenye moja ya ukumbi wa Land Mark hotel,Ubungo jijini Dar Es Salaam.Semina hiyo imeandaliwa na Kikundi Cha Sheria na Haki za Binadamu Cha TIFPA kwa Msaada wa Shirika la Ford Foundation la Marekani .
Baadhi ya Wanahabari,Wachora Katuni na Wadau wengine mbalimbali wakifuatilia mada mbali mbali zilizokuwa zikitolewa kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya iliyofanyika kwenye moja ya ukumbi wa Land Mark hotel,Ubungo jijini Dar Es Salaam.Semina hiyo imeandaliwa na Kikundi Cha Sheria na Haki za Binadamu Cha TIFPA kwa Msaada wa Shirika la Ford Foundation la Marekani .hiyo kuhusiana na mchakato wa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya na pia namna ya kuielimisha jamii katika umuhimu wa kushiriki
Mchora Katuni mahiri Masoud Kipanya na Mmoja wa watangazaji wa kutoka Times FM Radio Ibrahim Issa wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiendelea kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya iliyofanyika kwenye moja ya ukumbi wa Land Mark hotel,Ubungo jijini Dar Es Salaam.Semina hiyo imeandaliwa na Kikundi Cha Sheria na Haki za Binadamu Cha TIFPA kwa Msaada wa Shirika la Ford Foundation la Marekani .
Naibu Mhariri Mtendaji wa Free Media ambao ni wachapishaji wa gazeti la Tanzania Daima na Sayari, Ansbert Ngurumo akifafanua jambo mapema leo kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya iliyofanyika kwenye moja ya ukumbi wa Land Mark hotel,Ubungo jijini Dar Es Salaam,kushoto kwake ni Mwandishi Mkongwe hapa nchini,Mzee Phill Karashani
Mwenyekiti wa Kikundi Cha Sheria na Haki za Binadamu Cha TIFPA (Chama Cha Wanafunzi waliofadhiliwa na Shirika la Ford Foundation la Marekani) akielezea jambo kwa Wanahabari,Wachora Katuni na wadau wengine mbalimbali kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya.
Mijadala ikiendelea kwenye semina hiyo elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya
Mwandishi Mwandamizi kutoka Magazeti ya Serikali,Beda Msimbe akifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikitolewa kwenye semina elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya.
Washiriki wa Semina hiyo wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikiendelea kwenye semina hiyo.
Washiriki wa Semina hiyo wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikiendelea kwenye semina hiyo elekezi ya jinsi ya ushiriki wa vyombo vya habari kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya.

MWONGOZO KUHUSU UTARATIBU WA WATANZANIA WANAOISHI UGHAIBUNI KUSHIRIKI KUTOA MAONI YAO KUHUSU UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
_____________________

MWONGOZO KUHUSU UTARATIBU WA WATANZANIA WANAOISHI UGHAIBUNI KUSHIRIKI KUTOA MAONI YAO KUHUSU UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA
_________________________

Kwa kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ni utaratibu unaosimamiwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83; tunashauri kuwa Watanzania wote wanaotaka kushiriki katika mchakato huo ni vizuri kuzifahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambazo zote zinapatikana katika tovuti ya Tume ambayo ni www.katiba.go.tz

Kusoma Sheria hizo kutasaidia kuielewa Katiba ya sasa ubora na upungufu wake na kuelewa utaratibu na masharti yanayoainishwa kisheria kuhusiana na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.


1. MAMBO YA KUZINGATIA

Kwa kuwa uratibu na ukusanyaji wa maoni unatawaliwa na kusimamiwa na Sheria, Tume inaelekeza mambo yafuatayo yazingatiwe:

(a) Nani Mwenye Haki ya Kushiriki:

Mtu yeyote ambaye ni Mtanzania kwa uraia wake anayo haki ya kushiriki katika mchakato huu. Mtu ambaye kwa asili yake ni Mtanzania, lakini amepoteza uraia wa Tanzania hatoweza kushiriki; na akifanya hivyo atakuwa ametenda kosa chini ya Sheria.

(b) Utaratibu wa Utoaji Maoni:

Njia tatu za ukusanyaji wa maoni zitatumika. Njia hizo ni kama zifuatazo:

(i) Utoaji wa maoni kupitia mitandao ya kijamii, tovuti (www.katiba.go.tz) barua pepe ya Tume, (katibu@katiba.go.tz), nukushi + 255-22-2133442 na +255-224-2230769

(ii) Utoaji wa maoni kupitia nyaraka na barua zitakazotumwa kwa Tume kutumia anwani ya Tume, ambao ni: Katibu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 1681 DSM au Ofisi ndogo ya Tume, S.L.P. 2775 Zanzibar.

Endapo Mtanzania anayeishi Ughaibuni atabahatika kuwepo Tanzania wakati wa ukusanyaji wa maoni, anaweza kushiriki katika mchakato huo kama Watanzania wengine walioko nchini kwa kuhudhuria mikutano ya kukusanya maoni iliyoandaliwa na Tume.

(c) Utambulisho wa Mtoa Maoni:

Kila mtu atakayetoa maoni yake Tume anapaswa kubainisha mambo yafuatayo:-

(i) majina yake matatu;
(ii) namba ya pasi yake ya kusafiria na mahali ilipotolewa;
(iii) nchi na mji anaoishi;
(iv) endapo atatumia nyaraka au barua, ataambatanisha kivuli cha pasi yake (ukurasa unaoonyesha maelezo ya mtu mwenye pasi hiyo).

Tume inapenda kuwakumbusha tena Watanzania kuwa utoaji wa maoni ni jambo la uhuru na hiari ya mtu na kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya unawahusu raia wa Tanzania pekee.

Kwa maelezo zaidi bofya: www.katiba.go.tz/index.php/maoni-nje-ya-nchi

Monday, August 13, 2012

MAMBO YA MSINGI YA KUCHANGIA KATIKA KATIBA

MAMBO YA MSINGI KWA WANA WA UFALME KUCHANGIA WAKATI TUME YA KATIBA ITAKAPITA KWENYE ENEO LAKO

  1. Uhuru wa kuabudu dini anayotaka mtu na kubadilisha dini ubaki pale pale kama inavyosomeka katika Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977
  2. Katiba isitoe mwanya wowote wa Serikali/Nchi yetu kujiunga na jumuiya yoyote ya kidini. Ibara ya 3 nayosema kuwa nchi yetu haina dini isibadilike tena iheshimiwe sana
  3. Mahakama ya Kadhi pamoja na sheria zake zisiruhusiwe kabisa kuingia katika Katiba ya Nchi yetu kwani hiyo itaisababishia Nchi kuwa na gharama kubwa sana za kugharamia makadhi wote katika nchi hii. Mahakama ya Kadhi iwe nje ya Katiba kama ambavyo imetangazwa na viongozi wetu tayari. Nchi hii haina dini. Ibara ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ikumbukwe kuwa katika Katiba yetu hakuna sehemu yeyote ambapo imetaja Askofu, Mchungaji, Padre au Mwinjilisti. Vipi atajwe Kadhi? Endapo Kadhi ataingizwa katika Katiba, basi Ibara ya 26 (1) itakuwa ni mwiba kwa watu wote kwani kifungu hicho kinawataka Watanzania wote kufuata na kutii Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano. Na hivyo wote tutalazimika kumtii Kadhii na sheria zake
  4. Katiba mpya isiruhusu mifumo yote ya kiuchumi kuingiliwa na sheria za Kiislamu. Benki zote ambazo zimeruhusu ubaguzi huo zifutwe au ziache utaratibu huo mfano NBC – Islamic Banking Division, Amana Bank ambayo kwa sasa iko mbioni kuja Mwanza, Peoples Bank of Zanzibar n.k. Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 9 (g) “…Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vitatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu..”
  5. Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya sasa inayohusu Haki ya Uhuru wa Mawazo kwa kila raia isibadilishwe kabisa
  6. Katiba itoe uhuru ulio wazi kwa Wakristo kuendesha shughuli zao za kidini, kiuchumi, na kijamii ndani ya Zanzibar
  7. Chaguzi mbali mbali za kisiasa zisifanyike siku ya Jumapili ili kutoa fursa kwa Waumini wa Kikristo kuabudu. Badala yake chaguzi zifanyike Jumatatu, Jumanne, Jumatano au Alhamisi. Hili liwe jambo la kikatiba
  8. Katiba mpya iweke bayana kuwa kila Waumini wa dini mbali mbali wachinje wanyama au ndege wao kwa mujibu wa imani yao tofauti na ilivyo sasa ambapo machinjio yote yameshikiliwa na Waislamu na hata imedhaniwa kuwa wao ndio wenye haki ya kisheria ya kuchinja. Wakristo tumeagizwa kuchinja katika Jina la Yesu na si vinginevyo
  9. Katiba mpya ipige marufuku uvaaji wa mavazi yanayowakilisha dini katika shule za Serikali na hata katika shule binafsi au za kidini watoto wasiokuwa wa dini hiyo wasilazimishwe kuvaa mavazi ya imani isio ya kwao na pia wasilazimishwe kushiriki mafunzo yasiokuwa ya Imani yao. Katika kila shule wanafunzi wapewe nafasi ya kuwa na vipindi vya imani yao.
  10. Katiba itamke bayana ulinzi wa walemavu wa ngozi (Albino)
  11. Mambo mengine endelea kusikiliza KWA NEEMA FM RADIO 98.2 MHz
  12. Nitumie anuani pepe (email) kwa taarifa na mafundisho zaidi: Tuma kwenye namba 0767 982 111 au tuandikie: kwaneemafmradio@gmail.com

MAONI YA KATIBA MPYA-MTAZAMO WA WAKRISTO

WALA MSIACHE KUTUMIA AKILI ZENU IPASAVYO!!

MFUMO WA KUITAWALA: Tuendelee na mfumo wa Kisekula na wa kijamhuri katika kuongoza, kutawala na kuendesha shughuli zote za nchi, kama ilivyo sasa, sawa na Ibara 3 (1) ya katiba iliyopo sasa.

1. MIFUMO YA KI-DINI, KI-KABILA NA YA UBAGUZI WA AINA YOYOTE ISIINGIZWE KATIKA KATIBA. Kulingana na hali iliyopo sasa, dalili za wazi zimeanza kujitokeza kwa baadhi ya Viongozi kuwa watiifu kwa Imani zao na wengine jinsia, ukabila na sehemu wanakotoka badala ya kuzingatia utaifa na Utanzania wao. Mifano ni pamoja na:-

a) Kurudishwa kwa Mahakama ya kadhi na serikali kuamua kugharimia masomo ya viongozi wake kinyume kabisa na Ibara ya 19(2), kama Waziri Mkuu alivyotamka hivi karibuni.

b) Matamshi ya Waziri wa Katiba, Zanzibar kutaka watu wote wageni na wenyeji kutii sheria za Kiislamu zinazohusiana na mfungo wa mwezi wa Ramadhani – akikiuka kifungu cha (1) cha Ibara hiyo ya 19 ya katiba iliyopo sasa.

Ibara ya 19 (1) inasema: Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, Imani na Uchunguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au Imani yake.

19(2) nayo inasema: Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi , na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini kufanya zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Kutoka na maamuzi ya Serikali yaliyotamkwa kupitia Waziri Mkuu, na matamshi ya Waziri wa katiba Zanzibar, tunaona kuwa hata yale mambo ya ki-ibada, mfano:

a) Kulazimisha uvaaji wa sare zinazoonyesha dini au imani au ubaguzi wa aina fulani katika mashule, vyuo na taasisi mbalimbali za Serikali na za umma.

b) Kulazimisha majengo ya ibada katika mashule, vyuo na taasisi mbalimbali za Serikali na za Umma.

c) Kulazimisha uchinjaji wa wanyama na ndege kufavywa na waislamu peke yao na wengine kuonekana haramu.

Haya yote ni uvunjifu wa katiba iliyopo, kukiuka haki za watu wengine katika uhuru wa kuabudu na pia yanaleta mgawanyiko katika Taifa.

Kama Serikali haikuangalia kwa makini jambo hili, punde si punde, machifu nao watataka kurudishiwa mamlaka zao za uchifu, mamlaka za kidini hasa sisi Wakristo tutataka kurudishiwa mali zetu zilizotaifishwa na kudai kuwa na Mahakama zetu chini ya Waamuzi kama Biblia inavyobainishwa – nazo zigharimiwe na Serikali.

3.UENDESHAJI WA TAASISI ZA SERIKALI NA SERIKALI ZENYEWE.

· Katiba ya nchi itamke na kuheshimiwa na wote tupewe dhamana kulinda na kuitetea.

· Mambo ya dini yoyote yasipenyezwe kwa siri au kwa wazi katika kuendesha vyombo vya Umma (Dola, Mbunge na Mahakama)

· Kiongozi yeyote akionekana kufanya upendeleo huo kinyume na Katiba ashitakiwe na kuondolewa katika utumishi huo.

· Kukatisha kazi za Serikali ili kutoa mwanya kwa mambo ya dini moja ni upendeleo na si haki jambo hilo lisifanywe kabisa.

· Serikali isiruhusu au kushabikia mvutano wa kidini ama ushindani ambao unaweza kuleta vurugu katika nchi.

4. MAMBO YA MUUNGANO.

· Kupokezana Urais kati ya Tanzania ya Zanzibar na Tanzania ya Bara, hili lisiingie katika katiba Mpya.

· Rais achaguliwa toka popote Tanzania kulingana na uzalendo wake kwa nchi, uwezo maadili (Sio kwa ubaguzi wowote wa rangi na dini.

· Tanzania Zanzibar kuna Wakristo lakini hatuwaoni kuwakilishwa katika simulizi kuwepo na usawa katika kuwapa nao fursa wasibaguliwe. Mfano Tume ya kukusanya maoni hakuna Mkristo yoyote kutoka Zanzibar

· Wakristo wa Zanzibar wasilazimishwe kutii sheria za kiislamu hasa mwezi wa Ramadhani maana wao kwao sio imani yao huo ni ubaguzi na Unyanyasaji.

5. SHERIA ZA DINI MBALIMBALI.

· Sheria za dini zenye mkazo wa imani ya dini fulani tu zisingizwe katika katiba mpya (zitaleta vurugu)

· Mfano: sheria za kiislam, kikristo (kikatoliki) kimila kitume ambazo hazilingani na mfano wa kisekula zisiingizwe katika katiba mpya

· Kuingizwa kwa sheria za dini moja au baadhi utaleta hisia za kidini na chuki cha kidini

· Waumini wa dini husika watii sheria zao kwa uhuru wao bila kulazimishwa au kulazimisha wengine wasio wa dini hiyo

· Mifumo ya kiuchumi yenye harufu ya kidini isiingizwe katika sera za uchumi wa taifa mfano mfumo wa benki za kiislamu zinawabagua wakristo

· Alama za kidini mfano mavazi yenye sura ya kiibada yasitumiwe ndani ya maeneo ya ibada wasiohusika wasilazimishwe kuzitumia kwa visingizio vyovyote vile (sare za hijabu mashuleni)

6. CHAGUZI MBALIMBALI

Kuwepo Tume huru yenye mamlaka kamili ya kusimamia uchaguzi

· Siku ya kupiga kura isiwe siku ya ibada kwa dini yoyote

· Mgombea binafsi aruhusiwe kwa ngazi zote hiyo ni haki ya msingi ya kila mtu

· Mgombea achaguliwe kwa kuzingatia sifa za uwezo, maadili na uzoefu

· Sifa za udini, ukabila,ukanda,rangi na nasaba zisihusike (katiba izikataze)

· Mgombea yeyote atakayetumia kampeni za udini au ushawishi wa kidini, ukanda,ukabila,ubaguzi wa rangi au nasaba afutwe kwenye ugombea.

7. MGAWANYO WA MADARAKA.

· Uzingatie uwezo wa mtanzania, maadili yake, uzoefu wake pekee.

· Usiwepo ubaguzi wa jinsi, rangi, hali, ukanda, kabila na udini.

· Uwiano wa kidini usiwepo kabisa kwa vile Serikali haina dini pia itaongeza chuki na migogoro isiyo na tija.

· Kupokezana madaraka kwa misingi ya udini usiwepo kwa vile dini nyingi na kila moja ina haki sawa hakuna dini iliyo juu ya nyingine katika mfumo wa kisekula.

8. UHURU WA KUABUDU.

· Uendelee kama ulivyo ainishwa katika katiba ya 1977 Ibara ya 19.

· Kila dini ijiendeshe yenyewe kwa gharama zake bila kuvunja sheria za nchi na kugandamiza makundi mengine.

· Kila dini iheshimu dini nyingine zilizosajiliwa kisheria

· Kila raia ana haki kuchagua dini anayotaka au kuhamia dini anayotaka asibughudhiwe (Hiyo ni haki ya kibinadamu)

· Serikali, Bunge na Mahakama ziheshimu na kulinda uhuru huo.

9. MAANGALIZO/HISIA ZETU KAMA VIONGOZI.

· Tumeona kidogo kidogo Serikali inaingiza mambo ya dini moja kwa kasi na kusahau kwamba kuna dini nyingi katika Tanzania zenye haki sawa, Je? Serikali itakuwa tayari kusikiliza na kuingiza madai ya kila dini katika katiba? Utekelezaji wake utakuwaje? Ikiwa haiwezi kupokea na kuyaingiza madai ya dini zote katika katiba tunashauri iache jambo hilo maana litaleta migogoro isiyoisha ndani ya nchi.

· Tunahisi Serikali inatumia ukimya wa wakristo kufikiri kwamba hawaoni, hawajui, hawajali na hawawezi kusema au wanaogopa? Ama hawana madai au sheria na kanuni za Kimahakama aidha tunahisi Serikali ina dini ingawa haijatamka rasmi maana kuna mambo yanayotokea sasa, yanayoashiria kuingiza mambo ya dini moja wanapolalamika bila kuzingatia athari katika dini zingine ( Kusitisha shughuli za Bunge kwa ajili masilahi ya wabunge wa dini moja).

· Tunahisi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ya Kiislamu ndiyo maana nyumba za Ibada za wakristo zinachomwa moto kila mara na pia wakristo wa Zanzibar hawapati nafasi za uongozi, mfano wajumbe katika Tume ya kukusanya maoni ya marekebisho ya Katiba wajumbe wote 15 ni Waislamu kama kuna madai ya uwiano wa uongozi kwa misingi ya udini mbona huko hauzungumzwi?

HITIMISHO.

Tunatoa wito kwa wananchi wote:-

i. Tunaomba wananchi wote washiriki kutoa maoni bila woga mbele ya Tume ya kukusanya maoni yao, ni haki yao ya msingi

ii. Viongozi wa dini zote waaelimishe na kuwazuia waumini wao kupigania udini na itikadi za dini zao kuingia kwenye katiba inayoongoza watu wote wenye dini na wasio na dini, pia ni vizuri viongozi hao watamke hadharani kulinda na kutetea katiba ya nchi.

iii. Tunawaunga mkono Wabunge wanaopigania utaifa na maslahi ya watu wote tunawatia moyo waendelee kutetea mambo ya Kitaifa na hasa maslahi ya Watanzania wote tuko nyuma yao hata kama watazomewa Bungeni tunaomba wananchi wawaunge mkono na ikibidi kuwachagua uchaguzi ukifika endapo watagombea.

iv. Jambo lolote lenye itikadi za kidini au Kisiasa (Chama) lisiingizwe kwenye katiba kwa tafsiri inayoeleweka na upande mmoja hadi hapo tafsiri hiyo itakapo jadiliwa na pande zote husika na kujiridhisha kuwa halina madhara kwa maslahi ya Taifa.

v. Viongozi waliopo madarakani hivi sasa watamke hadharani ili Watanzania wajue misimamo yao katika kulinda na kutetea katiba, ikiwa ni pamoja na kutounga mkono mambo ya udini, ukabila, ubaguzi wa rangi, jinsia ili kuondoa hisia za watanzania kwamba wanatetea dini zao (Kinyume na walivyo apa) Ni wajibu wa wananchi kuwapima viongozi wote katika misingi hiyo ili kujua kwamba wanatenda haki au la.

vi. Pia tunatoa wito kwa watanzania wote bila kujali itikadi zao wajitokeze kuhesabiwa siku ya Sensa.


Chanzo : MAMBO YA MSINGI YA KUCHANGIA KATIKA KATIBA

Popular Posts