Pages

Showing posts with label IKULU - STATE HOUSE. Show all posts
Showing posts with label IKULU - STATE HOUSE. Show all posts

Wednesday, January 2, 2013

RAIS JAKAYA KIKWETE ALIVYOUKARIBISHA MWAKA MPYA 2013 KIJIJINI KWAKE MSOGA NA WANAKIJIJI


Wanakiji wa Msoga wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani wakiangalia fashifashi wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya kijijini hapo. 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakichangayika na wanakijiji wenzao wa kijijiji cha Msoga, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, kuukaribisha mwaka mpya kwa fashifashi na ngoma za utamaduni
 ms3:Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimtambulisha kaka yake Mzee Selemani Kikwete kwa  wanakijiji wenzake  wa kijiji cha Msoga, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, wakati wa sherehe za  kuukaribisha mwaka mpya kwa fashifashi na ngoma za utamaduni
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakipeana mkono wa heri na wanakijiji wenzao wa kijiji cha Msoga, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, wakati wa kuukaribisha mwaka mpya kwa fashifashi na ngoma za kienyeji.Picha na IKULU

Thursday, November 8, 2012

Jakaya Kikwete ameeleza furaha na shangwe yake kufuatia ushindi wa jana, Jumanne, Novemba 6, 2012 wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.


  Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza furaha na shangwe yake kufuatia ushindi wa jana, Jumanne, Novemba 6, 2012 wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.

Katika salamu zake za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa tena na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Kikwete amesema mapema leo, Jumatano, Novemba 7, 2012:
Rais Barack Obama akisheherekea ushindi wake dhidi ya mpinzani wake, Bw. Mitt Romney, na kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili.

“Nimepokea kwa furaha na shangwe habari za kuchaguliwa tena kwako kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe na kupitia kwako Chama cha Democratic pongezi nyingi kwa ushindi wako wa maana sana.”

Ameongeza Rais kikwete katika salamu zake hizo: “Kuchaguliwa kwako tena kuendelea kuongoza nchi yako muhimu na wananchi wake, ni ishara ya wazi ya uaminifu na imani ambayo wananchi wa Marekani wanayo katika uongozi wako wa mfano.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati unajiandaa kuchukua tena uongozi wa nchi hiyo katika kipindi chako kipya, napenda kukuhakikishia msimamo wangu binafsi na ule wa Serikali yangu kuwa tutaendelea kufanya kazi kwa karibu kabisa na wewe na Serikali yako ya kutukuka, ili kuendeleza uhusiano bora ulioko kati ya nchi zetu mbili ndugu.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu .
Dar es Salaam .
7 Novemba, 2012

Monday, October 22, 2012

RAIS JAKAYA KIKWETE AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA KENYA IKULU DAR ES SALAAM


 Rais JAkaya Mrisho Kikwete akipeana mkono na Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu. Wengine ni Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya, Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha TNA. Kushoto kwa Rais ni Wengine ni (kulia), Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda (kushoto) na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli alipokutana na ujumbe huo Ikulu jijini Dar es salaam Jumapili Oktoba 21, 2012 
Rais JAkaya Mrisho Kikwete akipeana mkono na Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha TNA. Kushoto kwa Rais ni Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Wengine ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu (kulia), Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda (kushoto) na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli alipokutana na ujumbe huo Ikulu jijini Dar es salaam Jumapili Oktoba 21, 2012 
 Rais JAkaya Mrisho Kikwete akipeana mkono na  Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Kulia kwake  Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa  chama cha TNA. Kushoto kwa Rais ni  Wengine ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu (kulia), Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA  Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda (kushoto) na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli alipokutana na ujumbe huo Ikulu jijini Dar es salaam Jumapili Oktoba 21, 2012
  Rais JAkaya Mrisho Kikwete akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha TNA, Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya, Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu (kulia), Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda (kushoto) na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli alipokutana na ujumbe huo Ikulu jijini Dar es salaam Jumapili Oktoba 21, 2012 .Picha na IKULU
--

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa  Jakaya Mrisho Kikwete ametaka wananchi wa Kenya wapewe nafasi ya kuamua ni viongozi gani wanawataka katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Machi mwakani.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wananchi wa Kenya wanayo haki ya msingi kabisa kuamua hatma ya taifa lao katika Uchaguzi Mkuu huo.

Mheshimiwa Rais aliyasema hayo  Oktoba 21, 2012 alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge wa vyama mbalimbali vya siasa vya nchini Kenya uliomtembelea Ikulu jijini Dar es salaam.

Ujumbe huo uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Waziri wa Fedha Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa  chama cha TNA na Waziri wa Sheria wa Kenya Mhe Eugene Wamalwa wa chama cha New Ford Kenya. Wote wawili ni wagombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi ujao.

Wengine katika msafara huo walikuwa ni Naibu Waziri wa Afya na mbunge wa Mombasa Mhe. Kambi Kazungu, Mbunge wa kuteuliwa wa chama cha TNA  Bi Rachel Shebesh, na Mbunge wa Kajiado kwa tiketi ya TNA Moses ole Sakuda na mbunge wa zamani Mhe Abdullahi Alli.

Rais Kikwete aliwapongeza kwa kuamua kufanya kazi kwa pamoja licha ya kuwa watakuwa  washindani katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu huo.
Mheshimiwa Rais ameitakia heri nchi ya Kenya katika uchaguzi huo ujao, na kusisitiza kwamba nchi hiyo ya jirani ina umuhimu katika mustakabali wa kiuchumi kwa nchi  za Afrika Mashariki.

Rais Kikwete wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alikuwa miongoni mwa viongozi walioshughulika sana kutafuta ufumbuzi wa ghasia na vurugu zilizozuka kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya.

Rais Kikwete alikaa siku tatu nchini Kenya akitafuta usuluhishi wa vurugu hiyo ya kisiasa nchini humo, ambayo katika mazungumzo yake leo ameyataja kama ajali iliyolipata Taifa la Kenya, na ambayo majirani wake hawaitarajii kutokea katika uchaguzi ujao.

Mwisho

Imetolewa na:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS
DAR ES SALAAM,
21 Oktoba, 2012

Wednesday, October 17, 2012

RAIS WA ZANZIBAR DK ALI SHEIN AWAAPISHA MJUMBE (MBM), NAIBU MAWAZIRI NA NAIBU KATIBU WAKUU WA WIZARA MBALI MBALI IKULU ZANZIBAR


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Mhe,Saidi Mohamed Said,kuwa Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, wakaati wa  hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar, leo mchana.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha CDR Julius Nalimy Maziku,kuwa Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Idara Maalum za SMZ katika hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar leo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Bw Juma Ameir Hafidh,kuwa Naibu Katribu Mkuu Ofisi ya Rais (Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo), katika hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar leo. Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Bw Mustafa Aboud Jumbe,kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Makaazi,Maji na Nishati, katika haflailiyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar, leo mchana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Bw Tahir M. Abdulla,kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar, leo mchana.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Mhe.Shawana Bukheti Hassan, kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akimuapisha Mhe, Mtumwa Kheir Mbarak,kuwa Naibu Waziri Kilimo na Maliasili,  wakati hafla iliyofanyika Ikulu MjiniZanzibar leo.Picha na Ramadhan Othman,Ikulu-Zanzibar

Rais Jakaya Kikwete aweka jiwe la Msingi kuzindua ujenzi wa Jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Oman


 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi kuashiria kuanza rasmi ujenzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania  nchini Oman katika mtaa wa balozi jijini Muscat Oman jana.Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, (watatu kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Oman, Ali Ahmed Saleh na (kulia) ni Afisa Mwandamizi Ubalozi wa Tanzania nchini Oman,  Bwana Abdallah Kilima.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizindua ujenzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Oman jana.Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe,watatu kushoto ni  Balozi wa Tanzania nchini Oman, Bw. Ali Ahmed Saleh, (wanne kulia aliyeshika karai) ni Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, Bw. Abdallah Kilima na (kulia anayeshuhudia) ni  Afisa katika Ubalozi huo, Bw. Saidi Mussa.Picha na Freddy Maro-IKULU

Monday, September 10, 2012

Rais Jakaya Kikwete Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Balozi wa Ubelgiji na Qatar

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ubelgiji hapa nchini Mheshimiwa Adam Koenvaad huko Ikulu tarehe 10.9.2012.
Rais Jakaya Kikwete akifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar hapa nchini Mheshimiwa Jassim Mohamed Mubarak Darwesh mara baada ya Balozi huyo kutoa hati zake za utambulisho kwa Rais Kikwete huko Ikulu tarehe 10.9.2012.Picha Zote na John Lukuwi

Friday, September 7, 2012

Rais Jakaya Kikwete Akutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Hui Liangya

Rais Jakaya Kikwete akipeana Mkono na Naibu Waziri Mkuu wa China, Hui Liangyu alipomtembelea ikulu, Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete akimkaribisha ikulu Jijini Dar es Salaam jana Naibu Waziri Mkuu wa China, Hui Liangyu
--
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatano, Septemba 5, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Hui Liangya kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam mara tu baada ya Mheshimiwa Liangya kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu katika Tanzania kama sehemu ya ziara ya nchi za Afrika, viongozi wote wawili wameeleza kuridhishwa kwao na hali na ustawi wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais Kikwete ametumia nafasi ya ziara hiyo ya Mheshimiwa Liangya kuishukuru China kwa michango yake katika jitihada za maendeleo za Tanzania.
Amesema Rais Kikwete: ”Jamhuri ya Watu wa China imetusaidia mengi katika jitihada zetu za maendeleo kuanzia kwenye ujenzi wa Reli ya TAZARA, ujenzi wa Uwanja wa Taifa, ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam, ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na ahadi ya kusaidia kuanzisha Benki ya Kilimo Tanzania. Kwa hakika Jamhuri ya Watu wa China imetusaidia mengi na tunaishukuru sana.”
Rais Kikwete pia ameitaka China kuendelea kuisaidia Tanzania hasa katika maeneo ya jinsi ya kuongeza kasi ya uchumi. “Tunataka kwa kweli kujifunza kutoka mifano ya mafanikio ya marafiki zetu wa karibu kama China. Hivyo, bado tunaendelea kusisitiza ushirikiano wa China katika kuanzisha na kuendesha maeneo maalum ya uzalishaji –Special Economic Zones “
Naye Mheshimiwa Liangya amemwambia Rais Kikwete kuwa China itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania ambao umekuwa unashamiri tokea ulipoanzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Dung.
Mheshimiwa Liangya amesema kuwa undani wa miradi yote ambayo China inasaidia katika Tanzania ungejadiliwa kwenye mkutano kati yake na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika baada mchana wa jana
Kiongozi huyo wa China pia ameisifu Serikali ya Mheshimiwa Kikwete kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na kuongeza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa umakini mkubwa. “Nawapongezeni kwa uamuzi wenu wa busara wa kuanzisha tena Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Ukitekelezwa vizuri unaweza kusukuma kwa kasi zaidi maendeleo ya nchi yetu.”


Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

5 Septemba, 2012

Sunday, September 2, 2012

Rais Jakaya Kikwete Ashiriki Mazishi ya Kiongozi wa Ethiopia Marehemu Meles Zenawi

Mmoja wa Askari Nchini Ethipia akilia kwa uchungu
Jeneza la aliyekuwa Waziri mkuu wa Ethiopia Marehemu Meles Zenawi likiletwa katika viwanja vya Addis kwaajili ya maombolezo ya kitaifa kabla ya mazishi yake yaliyofanyika leo. Askari wa kike akilia kwa uchungu
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Rais Jackob Zuma wa Afrika ya kusini wakati wa mazishi ya aliyekuwa Waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi jijini Addis Ababa leo mchana.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Rais Yoweri Kaguta Museveni wakati wa mazishi ya kiongozi wa Ethiopia marehemu Meles Zenawi yaliyofanyika leo jijini Addis Ababa.Picha na Freddy Maro-IKULU

Saturday, September 1, 2012

Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete mwisho wa mwezi Agosti 2012

HOTUBAYA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 AGOSTI, 2012

Utangulizi
NduguWananchi;
Kilamwisho wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimukwa taifa letu na watu wake. Leo ninamambo mawili ya kuzungumza nanyi. Lakini, kama ilivyo mazoea yetu hatuna budi kwanza tumshukuru MwenyeziMungu, muumba wetu, kwa kutujaalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezeshakuwasiliana leo tarehe 31 Agosti, 2012.

NduguWananchi;
Jambola kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa ya Watu na Makazilililoanza tarehe 26 Agosti, 2012 ambalo linatarajiwa kumalizika tarehe 01Septemba, 2012. Mtakumbuka kuwa tarehe25 Agosti, 2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze kwa wingi na muwapeushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa watakapopita majumbani mwenukutekekeza wajibu wao. Tumebakisha sikumoja kufikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka2012.

Napendakuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu wote kwa kujitokeza kwa wingikuhesabiwa. Mpaka sasa mwelekeo ni mzurina ugumu ulioonekana kuwepo pale mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi sikukadri utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa unaendelea. Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwaSensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.

Ndugu Wananchi;
Napendakutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo.Naomba waitumie siku moja iliyosalia yaani tarehe 1 Septemba, 2012 kufanyahivyo. Aidha, namuomba Mkurugenzi Mkuuwa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya Muungano na Mtakwimu Mkuu wa Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa kasoro zo zote zilizopo mahali po potezinatafutiwa ufumbuzi ili mambo yakamilike bila upungufu wowote.

NduguWananchi;
Baadaya kazi ya Makarani wa Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, tarehe 2Septemba, 2012, linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu ambaowatakuwa bado hawajahesabiwa. Itakuwepofursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa. Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa Wenyeviti wao waSerikali za Mitaa au Vijiji. Taarifahizo zitafikishwa kwa Kamishna wa Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la kuhesabuwatu litakuwa limefika mwisho. Yuleambaye atakuwa hakutumia fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katikahesabu ya Watanzania ya mwaka 2012. Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu kutumia siku ya tarehe1 Septemba, 2012 kuhesabiwa na kamahapana budi basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa Mwenyekiti wako waMtaa au Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku hiyo ili nawe ujumuishwe.

NduguWananchi;
Baadaya kazi ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili kufikia mwisho, itaanza kazi yauchambuzi na kuunganisha takwimu na taarifa zilizokusanywa. Kazi hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitajiumakini na uangalifu wa hali ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la Sensalitaingia dosari. Nafarijikakuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa na Wakuu wa Idara za Takwimu za Serikalizetu mbili, kwamba wanatambua ukweli huo na wajibu wao. Wameniarifu kwamba kama mambo yatakwenda kamailivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watuna jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa nyingine zitafuatabaadaye. Narejea kuwasihi Watanzaniawenzangu kuwapa nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupatematokeo yaliyo sahihi.
Mpakana Malawi
NduguWananchi;
Jambola pili ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu mpaka baina ya Tanzania naMalawi katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwamiaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe. Sisi, Tanzania, tunasema mpaka upo katikatiya ziwa wakati wenzetu wa Malawi wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande waTanzania. Kwa maneno mengine wanasema ziwalote ni mali ya nchi yao.

Utata kuhusu mpaka wetu katika ZiwaNyasa haujaanza leo. Ulikuwepo tanguwakati nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea baadaya Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa. Jambokubwa lililo tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamuakukaa mezani na tunalizungumza suala hilo.
Chimbukola Mzozo
NduguWananchi;
Chimbuko la mzozo wa mpaka ulioposasa, baina ya nchi zetu mbili jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, nimakubaliano baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetuyaliyofanywa tarehe 1 Julai, 1890. Makubalianohayo yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany HeligolandTreaty) yalitiwa saini kule Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza naWajerumani. Wakoloni hao walikubalianakuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wenginewaliopakana nao. Kwetu sisi hayo ndiyomakubaliano yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake. Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza naWajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi yaMalawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpakaulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande waTanzania.

Ndugu Wananchi;
Katika kipengele cha Sita(Article VI) cha Mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho yampaka mahali po pote kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana namazingira na hali halisi ya mahali hapo. Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume yaMipaka iliundwa. Ilianzia kazi katika MtoSongwe kuhakiki mpaka baina ya nchi yetu na Malawi. Tume ilikubaliana kuhamishampaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati yamto. Baada ya uhakiki katika eneo hilokukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.
Tume iliendelea na kazi yake katika ZiwaTanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkatabampya kusainiwa mwaka 1910. Tume iliendeleakatika ziwa Jipe ambapo mpaka ulihamishwa pia hadi katikati ya ziwa.

Ndugu Wananchi;Bahati mbaya Tume hiyohaikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokeakwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 - 1918. Kama tunavyokumbuka, Waingereza na Wajerumaniwaligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini. Baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Barazala Umoja wa Mataifa (The League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika.Hivyo, Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.

Ndugu Wananchi;
Wakati Tume ya Uingereza naUjerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Urenoiliendelea na kazi. Matokeo yake, mwaka1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka waZiwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji,na kuuhamishia katikati ya ziwa.

Ndugu Wananchi;
Jambo la kustaajabisha ni kuwa,Waingereza walioona umuhimu na busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi naMsumbiji, hawakuona umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi. Inashangaza, kwa sababu wakati huo Uingerezailikuwa mtawala wa nchi zetu mbili hivyo kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi,lakini hawakufanya hivyo. Na, baya zaidini kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotakakupatiwa ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa. Watu walitaka ufafanuzi kwa sababuinasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifaziliweka mpaka katikati ya ziwa. Lakini,kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala lampaka wa Malawi lilijitokeza tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakatiule lilijulikana kuwa Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO). Hoja ya Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpakakuwekwa kwenye ufukwe wetu kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kandokando ya ziwa haki yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samakina kupata manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya Serikaliya Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana wakati ule. Hoja iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali yaTanganyika ijadiliane na Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia waUingereza ili ufumbuzi upatikane. Wakolonihawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuruwake tarehe 9 Desemba, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.
Juhudiza Kubadili Mpaka wa Ziwa Nyasa Baada ya Uhuru
NduguWananchi;
Wakatitulipopata Uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu mpaka wa Tanganyika na Malawiuliendelea Bungeni, ambapo ilitolewa hoja kwamba zifanyike juhudi za makusudiza kuanzisha na kuendeleza mazungumzo ya kurekebisha mpaka huo kwa manufaa yawananchi wote wanaoishi pembezoni mwa ziwa. Iliamuliwa kwamba tusubiri mpaka wenzetu wa Malawi wapate uhuru ili yafanyikemazungumzo baina ya nchi mbili huru. Kulijengeka matumaini kuwa mambo yangekuwa rahisi. Bahati mbaya haikuwa hivyo na kwamba mamboyakageuka na kuwa magumu na ya uhasama. Miakamitatu baada ya Malawi kupata Uhuru wake (1964), kunako tarehe 3 Januari 1967,Serikali ya Tanzania iliandika barua kwa Serikali ya Malawi kuelezea tatizo la mpakawa ziwani na kupendekeza nchi zetu mbili zizungumze na kulitafutiaufumbuzi.

Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri tarehe 24 Januari,1967, Serikali ya Malawi ikajibu kukiri kupokea barua hiyo na kuahidi kuwa itatoamajibu baada ya muda si mrefu. Hatahivyo, tarehe 27 Juni, 1967, Rais Kamuzu Banda akilihutubia Bunge la Malawi, alikataamaombi ya Tanzania. Alisema hayanamsingi na alidai kuwa kihistoria Songea, Mbeya na Njombe ni sehemu yaMalawi. Hivyo basi, mazungumzo yakafa.

Tanzania haikukata tamaa. Alipochaguliwa Rais wa Pili wa Malawi, MheshimiwaBakili Muluzi, juhudi zilifanyika lakini nazo hazikufika mbali. Bahati nzuritarehe 9 Juni, 2005, Rais wa Tatu wa Malawi, Mheshimiwa Bingu Wa Mutharika,ambaye sasa ni marehemu, alimuandikia barua aliyekuwa Rais wa nchi yetu wakatiule, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kushauri nchi zetu zifanye mazungumzokuhusu mpaka wa ziwani. Alipendekeza iundweTume ya Pamoja itakayojumuisha Mawaziri na Wataalamu kutoka nchi zetumbili. Tume hiyo itatoa mapendekezo kwaMarais wa nchi zetu mbili ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina yao. Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzisuala hilo.

Ndugu Wananchi;
Kwa kuwa ilikuwa kipindi champito kuelekea kuchaguliwa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Benjamin Mkapahakuwahi kuishughulikia barua hiyo. Nilipoletewa barua hiyo nikaijibu kukubaliushauri na mapendekezo yake. Aidha, nilipendekezaWizara na Idara zipi za Serikali zetu zishirikishwe katika Tume hiyo. Bahati nzuri Rais wa Malawi alikubalimapendekezo yangu pamoja na lile la kwamba Malawi waitishe mkutano wa kwanza waTume hiyo.

Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa mikutano mitatu ya Tumeya Pamoja imeshafanyika, wa kwanza ulifanyika tarehe 8 – 10 Septemba,2010. Mkutano wa pili ukafanyika tarehe27 – 28 Julai, 2012 hapa Dar es Salaam na wa tatu ukafanyika Mzuzu na Lilongwetarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Hatua kadhaa zimepigwa lakini bado muafakahaujapatikana kwa maana ya madai yetu ya kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa namadai yao kuwa mpaka ubaki ufukweni kwetu kama ilivyo kwenye Mkataba wa Heligoland wa Julai1, 1890. Hoja ya wenzetu ni kuwa huondiyo mpaka tuliorithi wakati wa uhuru. Wanataka tuthibitishe hivyo na kwamba tuzingatie kauli ya OAU yakuheshimu mipaka tuliyorithi kwa wakoloni. Wananukuu kauli ya Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere akisisitiza hoja hiyo katika mkutano wa OAU mwaka1963.
Hojaza Msingi za Kutaka Mpaka Uwe Katikati ya Ziwa
NduguWananchi;
Kwa upande wetu tumekuwa na hojakadhaa za kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa. Ya msingi kabisa ni ukweli kwamba Mkataba wa Heligoland umekosewa kwakuamua kuwanyima wananchi wa Tanzania wanaoishi ufukweni mwa ziwa haki yao yamsingi ya kutumia maji na rasilimali zilizomo katika Ziwa Nyasa. Zipo sababu kadhaa kwa upande wetu kudaihivyo. Mojawapo ni sheria ya kimataifa inayoelekezakwamba po pote kwenye maji ya asili kama vile ziwa na mito iliyopo kati ya nchimbili mpaka huwa katikati. Ndiyoutaratibu unaotumika duniani kote, na mifano iko tele. Kwa nini iwe tofauti katika ziwa Nyasa na kwaupande wa Tanzania tu wakati kwa upande wa Msumbiji mpaka upo katikati ya ziwa?

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mto Songwe, mpakabaina ya nchi zetu mbili upo katikati. Iwejehapa kanuni hiyo itambulike na kuheshimiwa lakini isiwe hivyo ziwani? Kama nilivyoeleza awali, mwanzoni Mto Songwe woteulikuwa umewekwa upande wetu, lakini Tume ya Mipaka iliyoundwa mwaka 1898ilifanya marekebisho na kuweka mpaka katikati ya mto. Kama nilivyokwishagusia kwenye ziwa hilo hilola Nyasa kwa upande wa Msumbiji mwaka 1954 mkataba wa mwaka 1891 ulioipa Malawiziwa lote ulirekebishwa na mpaka kuwekwa katikati. Kwa nini isifanyike hivyo hivyo kwa upande waTanzania? Hivi hasa ni kipi ambachowenzetu wa Msumbiji walichotuzidi na kustahili kupata haki yao ya msingi ya kumilikina kutumia maji ya Ziwa Nyasa ambacho sisi Tanzania tumepungukiwa?

Ndugu Wananchi;
Maji ni zawadi ya Mwenyezi Mungukwa wanadamu wake, waitumie kwa uhai na maendeleo yao. Iweje leo, kwa watu wanaoishi pembeni mwaziwa hilo hilo wengine wapewe na wengine wanyimwe haki ya kulimiliki na kulitumia?Kwa nini wanyimwe haki ya kunufaika na zawadi hiyo? Hivi kauli ya wakoloniwaliokaa Berlin ya kusema fulani apate na fulani asipate inatosha? Hivi kweli ni rahisi kiasi hicho?

Mpaka wa kwenye maji ni tofautina ule wa nchi kavu. Huu una rasilimaliambayo huwezi kuamua kumnyima mwanadamu mwingine anayeishi pembeni yake kwavile haina badala yake. Unapowaambiawatu wa Mbamba Bay, Liuli, Lituhi, Manda, Ngonga, Matema, Mwaya, Itungi nawengineo waishio kando ya ziwa kuwa maji hayo si yao bali ni mali ya Malawihawakuelewi na watakushangaa sana. Watadhani umechanganyikiwa kwani tangu waumbwe wamekuwepo hapowanamiliki na kutumia maji ya Ziwa. Unatakawafanyeje? Waende Malawi kuomba kibalicha kuyatumia? Wao watakuuliza swalimoja tu “hivi hao wenzao wanaoishi ng’ambo ya pili wamewazidi nini katikaubinadamu wao hata wapewe maji yote na wao wanyimwe?”

Ndugu Wananchi;
Kwa maana halisi ya Mkataba waHeligoland tangu tarehe 1 Julai, 1890, wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwawanakunywa, kuoga, kuvua samaki na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yaobali ya nchi nyingine. Na kwa kuwa wamekuwawanafanya hivyo bila ya kupata kibali cha Malawi wamekuwa wanaiba maji nasamaki wa Malawi na kusafiri isivyo halali katika nchi ya watu. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo. Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.

Ndugu Wananchi;
Na hiyo pia, ndiyo maana, busara na hekima ya Sheria ya Kimataifa kuhusumpaka wa kwenye maji kuwakatikati. Sheria hii inazingatia halihalisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo imekuwa inalitegemea maishayao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai na maendeleo yao. Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kandoya Ziwa Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake. Hawataelewa wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumiamaji na rasilimali za ziwani kwa hisaniya nchi ya Malawi.

Kwa watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumbawao na wenzao wa ng’ambo ya pili, siyo sawa na siyo haki hata kidogo kuwafanyiahivyo. Kwe kweli ni unyanyasaji wa haliya juu. Ndiyo maana wazee wetu walidaisuala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru. Na ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zaokatika madai haya ya haki.

Ndugu Wananchi;
Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanyatudai haki ya kumiliki na kutumia Ziwa Nyasa. La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya Tanzania nayo inachangiakujaza maji katika ziwa. Iweje leo maji yanayojazaziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani, ziwa hilo si mali yao wenyemito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali ya watu wengine. Hivi kwelindivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza vyanzo vya mito hiyo na kuruhusumaji yake kutiririka na kuingia ziwani?

Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kwamba mpaka waTanzania na Malawi kuwa ufukweni kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikanikwa uhakika. Unategemea mabadiliko kutokanana kujaa na kupungua kwa majiziwani. Kunafanya mpaka wa nchi kuwahautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya safari. Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwawake nalo ni tatizo la aina yake. Ndiyomaana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.

Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishasema, chimbukola mzozo huu ni mkataba wa Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina yanchi zetu. Bahati mbaya sana Tume yaMipaka haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya nchi yetu na majirani zake kufuatiakuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka 1914. Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya yaUingereza. Bahati mbaya kwetu Waingerezawaliotawala nchi zetu mbili tangu 1918 hawakuchukua hatua za kurekebisha mpakakabla ya uhuru wa nchi zetu. Ni maoni yetukuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni– Waingereza na Wajerumani. Tukifanyesisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka1967 hayakufanikiwa. Bahati nzurikufuatia uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi zetu sasa zinazungumza. Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebishampaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka. Jambo linaloleta faraja, hata hivyo, ni kuwasote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu wa kutusuluhisha.

Ndugu Wananchi;
Hayo ndiyo matokeo ya mazungumzoya Tume yetu ya pamoja tangu ngazi ya Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwaMawaziri, katika vikao vya Mzuzu na Lilongwe kati ya tarehe 20 – 27 Agosti,2012. Katika mkutano wao wa tarehe 27Agosti, 2012 Mawaziri husika wa nchi zetu chini ya uongozi wa pamoja wa Waziriwa Mambo ya Nje wa Malawi, Mheshimiwa Ephraim Chiume na mwenzake wa Tanzania,Mheshimiwa Bernard Membe, wameafiki mapendekezo hayo. Aidha, wamekubaliana kuwa pande zote mbiliwakutane tena Dar es Salaam kati ya tarehe 10 – 15 Septemba, 2012 kukubalianajuu ya usuluhishi wa aina gani unafaa.

Ndugu Wananchi;
Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua muhimukuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili. Hata hivyo, bado safari ni ndefu na huendaikawa na magumu mengi. Maombi yangu kwa viongozina wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea kuunga mkono jitihada hizi. Tuwaunge mkono wataalamu na Mawaziri wetu iliwafanikishe vizuri jukumu lao. Tuzingatie na kuheshimu walichokubaliana Lilongwe kuwa viongozi nawananchi wa nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au kufanya vitendo vinavyoweza kuchafuahali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri majadiliano yanayoendelea.
Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatiaushauri na rai hiyo ya Mawaziri na wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuriya mazungumzo na kuwezesha mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napendakusisitiza kuwa si makusudio yangu wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho lasuala hili kwa nguvu ya kijeshi. NawahakikishiaWatanzania wenzangu kuwa hatuko vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vitadhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika Ziwa. Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu zaujenzi wa taifa letu kama kawaida.

Nilimhakikishia hivyo Rais waMalawi, Mheshimiwa Joyce Banda nilipokutana naye Maputo, Msumbiji tarehe 18Agosti, 2012. Tanzania haina mpango wakuingia vitani na Malawi. Mimi nawenzangu Serikalini tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya kukaa nandugu zetu Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu sote sasatumeipata. Hatuna budi kuitumiaipasavyo. Naamini, tukifanya hivyo,inaweza kutufikisha pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa ajili hiyo kwa pande zetumbili, kuipa fursa ya mazungumzo nafasi ya kuendelea bila ya vikwazovisivyokuwa vya lazima.

Ndugu Wananchi;
Kwasababu hiyo basi , napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa vyombo vyahabari na wanasiasa wenzangu tuepuke kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzona kuchochea uhasama kati ya nchi zetu mbili jirani na rafiki. Kuna manufaa makubwa ya kumaliza mzozo wetukwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita. Kufikiria sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, siwakati wake muafaka. Aidha, tukitumianjia ya vita, badala ya kuwa tumepata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wamgogoro mpana zaidi. Tuendelee kuwaungamkono wawakilishi wetu katika Tume yetu ya pamoja. Naahidi, Serikali itakuwa inawapa taarifakadri mazungumzo yetu na wenzetu wa Malawi yatakavyokuwa yanaendelea. Nina hakika tutamaliza salama.
MunguIbariki Tanzania!

MunguIbariki Afrika!

Asantenikwa Kunisikiliza

Monday, August 27, 2012

Rais Jakaya Kikwete na Familia Yake Washiriki Zoezi la Sensa ya Makazi na watu

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete na familia yake akijibu maswali toka kwa karani wa sensa ya wazu na makazi Bw. Clement Ngalaba leo Agosti 26, 2012 wakati alipojiunga na mamilioni ya Watanzania katika zoezi hilo lililofanyika kwa mafanikio makubwa nchi nzima.Picha na IKULU

Sunday, August 26, 2012

HOTUBA YA RAIS WA TANZANIA KUHAMASISHA SENSA YA MAKAZI NA WATU 2012

Ndugu wananchi;
Imekuwa ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi. Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.

Ndugu wananchi;
Katika historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.

Ndugu wananchi;
Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka 2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.

Ndugu Wananchi;
Pamoja na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.

Ndugu wananchi;
Shughuli yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida. Lakini, tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kuwepo. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya jitihada za makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini. Wamekuwa wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo baadhi yake hazina uhusiano wo wote na Sensa. Zipo sababu nyingine ambazo hata haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa hawatashiriki Sensa mpaka mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule Berlin, Ujerumani atakaporudishwa. Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa nchini zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita. Mwaka 1906 wana sayansi wa Kijerumani waliyagundua mabaki hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na kuyapeleka Ujerumani ambako yamehifadhiwa tangu wakati huo.

Ndugu Wananchi;
Kudai mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa kale waliokuwepo wakati huo wanafananaje. Huenda pia kikawa kivutio cha utalii. Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi. Watu wakisusia Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali hata watu wengine nchini na duniani watawashangaa. Lakini, jambo ambalo ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani? Mjerumani au wanajisusia wenyewe? Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata akirejeshwa huna manufaa ya moja kwa moja? Hasara anapata nani sisi au wao? Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza maneno yahusuyo Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa mambo yenye maslahi makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu. Tuachane nao hawatutakii mema na wala hawaitakii mema nchi yetu. Nawaomba tusitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni.

Ndugu Wananchi;
Wapo ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika orodha ya maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu. Wahusika wakuu hasa ni baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu wasikubali kuhesabiwa. Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi Waislamu wawaunge mkono katika msimamo wao huo. Nimesoma baadhi ya nyaraka na vipeperushi vyao kuhusu madai hayo. Nilipata pia bahati ya kukutana na kuzungumza na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati hizo. Nia yangu katika kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani hoja na madai yao. Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki, Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania.

Hawazikubali taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji wa takwimu hizo. Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya kuwa ni asilimia fulani Watanzania. Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu. Kwa maoni yao, taarifa hizo si za kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu wanazozijua watoaji wa taarifa hizo. Ili kuondoa upotoshaji huo, wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.

Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika hayo. Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya watu hutolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha Serikali. Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na wala siyo chanzo cha takwimu zilizotolewa na mashirika hayo. Walikozipata wanajua wenyewe. Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na ndiyo maana zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na wakipenda watoe tamko la kuzikataa.

Ndugu Wananchi;
Niliwaambia pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni kuionea na kutoitendea haki. Vile vile kuibebesha dhima ya kuongeza swali la dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili. Napenda, kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna hiyo kutambua unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea mifarakano isiyokuwa ya lazima kama ilivyo sasa.


Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya kuliingiza swali la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na kiutekelezaji. Wakati wa ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu yaliulizwa katika Sensa. Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika Sensa ya kwanza ya mwaka 1967 kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya kikoloni. Baada ya hapo ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza maswali hayo kwani nia ya wakoloni kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale. Walitoa huduma kwa ubaguzi, sera ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na Mapinduzi. Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, bali kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.

Ndugu Wananchi;
Sera hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa letu na watu wake. Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni wengi na hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa, sera mpya inawataka watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Nionavyo mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima kubwa. Tuendelee kuidumisha na kuienzi. Kufanya vinginevyo, na hasa kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu ni kuliingiza taifa letu ambalo lina sifa ya amani, upendo na utulivu, katika migogoro isiyokuwa ya lazima. Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na kudumisha sera yetu hii nzuri na sahihi.



Ndugu Wananchi;
Sababu ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji. Imechukua miaka kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Isitoshe Sensa ya majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali yaliyopo na marekebisho kufanywa baada ya hapo. Kuingiza mambo au jambo jipya sasa itakuwa viguku kiutekelezaji. Kutachelewesha zoezi zima na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Kwa vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo cha kutoa huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu wanaokereketwa na jambo hili waache kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze kuhesabiwa. Tujitokeze kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya wananchi wa Tanzania.

Ndugu Wananchi;
Sioni ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo na Waislamu. Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi Kuu ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo. Hata ukiamua uiite Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana sababu. Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa msingi wa dini kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na Waislamu. Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.

Ndugu Wananchi;
Katika maelezo yao kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Said na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa walinieleza kwamba kwa kawaida katikati ya Sensa moja na nyingine, hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani Demographic Survey. Huu ni utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya kaya ambapo taarifa za mambo mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa hukusanywa. Mara ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973, yaani baada ya Sensa ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978. Ni makusudio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016 ambapo baadhi ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa. Subira yavuta heri.

Ndugu Wananchi;
Nimehakikishiwa na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri na zoezi liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012. Lakini, mafanikio ya zoezi lenyewe yatategemea sana ushiriki wa watu ambao ndiyo walengwa na wadau wengine. Naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa kisiasa na kiutendaji wa ngazi mbalimbali waendelee kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika maeneo yao ya uongozi. Hawana budi kuhakikisha kuwa zoezi linakuwa na mafanikio makubwa. Wale wote wanaofanya vitendo vya kuvuruga zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
Nawaomba viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na kushirikiana na Makarani wa Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao. Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi wasijitokeze kuhesabiwa. Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema nchi yetu.

Ndugu wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi wa kisiasa, kusimamia na kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Sensa katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Shehia kwa kazi nzuri ya matayarisho na uendeshaji wa Sensa ya mwaka 2012. Nawatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu na adhimu kwa nchi yetu na watu wake.

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu hawa kwa kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza kwetu ndiyo ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Ewe Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa kwa maendeleo yako na ya taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa kunisikiliza

Popular Posts