Pages

Showing posts with label CHADEMA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO. Show all posts
Showing posts with label CHADEMA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO. Show all posts

Monday, January 7, 2013

Taarifa ya BAVICHA kwa vyombo vya habari kuhusu kuwavua uanachama wanachama wake


Taarifa kwa Vyombo vya habari juu maamuzi ya kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA)


Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kuwa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (BAVICHA), limefanya kikao cha kawaida cha Kamati Tendaji, juzi 5 Januari 2013, katika Hotel ya Benzi Garden jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala matatu mazito.

Kwanza, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina suala la kuporomoka kwa elimu nchini, ambapo serikali imepunguza alama za viwango vya kufaulu, jambo ambalo limesababisha mamia ya wanafunzi waliochaguliwa kutokuwa na sifa.

Pili, Kamati Tendaji ilijadili jinsi Bavicha itakavyoshiriki katika maandilizi ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema yalioeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.

Tatu, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina “Tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa Chadema na Baraza kwa ujumla.”

Ndugu waandishi wa habari, yapo baadhi ya vyombo vya habari jana na leo vimeripoti kwa upotoshaji mkubwa wa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kikao hicho.

Kwa mfano, gazeti moja la kila siku limemtaja mwanachama wetu mmoja kuwa ndiye aliyekuwa mtoa taarifa wetu muhimu na kusema mbunge mmoja wa CHADEMA alijadiliwa katika kikao hicho kuwa ni miongoni mwa kundi hili la MASALIA na kufika mbali zaidi kwa kusema, “…sasa amekalia kuti kavu.”

Lakini ukweli wa kilichojadiliwa kikaoni ni huu ambao tunaueleza sasa:

Kwanza, kuhusu ajenda ya kuporomoka kwa elimu: Kamati Tendaji imeagiza kuwa utafiti uliofanywa na BAVICHA katika ngazi ya sekondari, ambao umegundua madudu mbalimbali, uongezwe hadi shule za Msingi na taarifa yake ililetwe kwenye kikao kijacho cha Kamati Tendaji.

Kwenye ajenda ya pili: Kamati ya Utendaji BAVICHA, ilipokea na kujadili agizo la Kamati Kuu ya Chama iliyoeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.

Katika ajenda ya tatu juu ya tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa CHADEMA, na Baraza, Kamati ya Utendaji ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji iliyoundwa Septemba mwaka jana kwenye kikao chake kilichofanyika mjini Morogoro. Kamati ilipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hii.

Katika hili, watuhumiwa wakuu walikuwa ni kama ifuatavyo:


  1. Juliana Shonza, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
  2. Habib Mchange, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  3. Mtela Mwampamba, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  4. Gwakisa Burton Mwakasendo, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  5. Joseph Kasambala, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA


Aidha, baada ya Kamati iliyoundwa kuwahoji baadhi ya watuhumiwa na wanachama wengine mbalimbali, ilibaini kwamba wapo baadhi ya wanachama wa BAVICHA ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tuhuma hizi. Hao ni pamoja na Ben Saanane – maarufu kama Eight Oclock.

Katika orodha hiyo, wakatajwa pia Exaud Mamuya lakini kamati ikashindwa kumpata Mamuya kwa kuwa hakukuwa na mawasiliano ya kutosha.

Ndugu waandishi wa habari, hizi sasa ni tuhuma za kila mmoja:

Ndugu Juliana Shonza:

Alituhumiwa akiwa katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya Baraza, Chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko nchini.

Amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM, akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni kwa kutimiza wajibu wao wa kudai haki zao za msingi na uwajibikaji wa serikali na ambao ni wanachama wa CHASO.

Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali kuitisha mkutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe.

Mfano dhahiri hapa ni kikao alichofanya Baa ya Highland iliyoko maeneo ya Makumbusho, majira ya saa 9 hadi saa 11, ambapo aliwaita viongozi wa CHASO, akawashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye, endapo tu watakubali kufanya press conferences na kuisema CHADEMA kuwa inawavuruga vijana walioko vyuoni.

Tarehe 6, Desemba, 2012 Hotel MIC, kuanzia saa 10 hadi saa 12, aliwaita baadhi ya vijana ambapo yeye na wenzake walipanga njama za kukichafua chama na kutukana viongozi, kwa manufaa ya CCM.
Ifuatayo hapa chini ni moja ya sms ambazo Juliana Shonza alikuwa akiwaandikia vijana katika ushawishi wake wa usaliti kwa mapambano haya ambayo chama chetu kinafanya, kuwapigania Watanzania maskini na wanyonge katika nchi yao;

“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu hela yako yakulinda mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko tutalindana tu jembe usijali.”

Huu ni moja tu kati ya ushahidi mwingi, wa meseji, simu, sauti, video, picha na vikao kadhaa katika maeneo mbalimbali, unaomwingiza Shonza na wenzake wengine katika sifa mbaya ya usaliti wa chama, baraza na viongozi wake na wanachama wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Hapo alikuwa akimwandikia mmoja wa viongozi wetu ili ashiriki katika press conference ambayo yeye Makamu Mwenyekiti kwa kushirikiana na wenzake wengine, walikuwa wameiandaa kwa nia ya kuchafua chama, kulichafua baraza, kutukana viongozi waandamizi pamoja na kuvuruga na kuchonganisha wanachama wa CHADEMA.

Matokeo ya kikao hicho cha MIC Hotel, yalionekana siku moja baada ya kikao hicho, ambapo mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Edo Mwamalala, aliyeshiriki kikao hicho cha MIC Hotel, aliitisha mkutano na waandishi wa habari, akijitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA, cheo ambacho hakuwa nacho.

Aidha, Shonza amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake, wakipanga njama za kufanya kazi na majukumu ya CCM kuhujumu BAVICHA pamoja na CHADEMA. Mikakati ya kuvuruga baraza, kuchonganisha wanachama na kutukana chama na viongozi wakuu, kwa siri na hadharani, imekuwa ikipangwa katika vikao hivi.

Amebainika kukiuka kipengele cha 10.1(x) cha Maadili ya Viongozi, cha Katiba toleo la mwaka 2006, kinachomtaka kiongozi yeyote asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali, kwa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.

Ameonesha ubaguzi wa kikabila na kikanda kupitia maandiko yake kwenye mtandao kwa kutumia jina lake, anapungukiwa na sifa muhimu na mahsusi za kuwa kiongozi, kwa mujibu wa kipengele cha 10.1(iv) kinachomtaka kiongozi yeyote asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda vinavyolenga kuleta ubaguzi ndani ya chama.

Kwa kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA, kushiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na wanachama, kukosanisha na kutukana viongozi wa chama, ndugu Shonza amevunja kipengele cha 10.1(i),(viii)(ix) na ibara ya 10.2(iv).

Kwa kushiriki vikundi hivyo hapo juu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya BAVICHA wamejiridhisha pasi na shaka kuwa Shonza haendani na katiba, falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA. Hivyo kwa mujibu wa ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 anakosa sifa za kuwa mwanachama wa Baraza la Chama.

Kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya wanachama na viongozi wenzake, ameendelea kuvunja kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10.1(viii).

Amehusika katika kuanzisha, kujihusisha na kuratibu moja kwa moja kundi la vijana waliokuwa wakizunguka mikoani na kushawishi viongozi wa vijana kutoa matamko kwa kutumia jina la CHADEMA kufanya kazi na majukumu ya CCM ya kukichafua chama, kugombanisha wanachama na kumtukana Katibu Mkuu kwa kutumia propaganda za CCM.

Kamati Ndogo ilimuita Ndugu Shonza ili kumhoji. Lakini aligoma kwa madai kuwa haitambui kamati hiyo na wala hajui kuwa kuna mgogoro, jambo ambalo limetushangaza wengi kwa kuwa Ndugu Shonza alikuwapo katika kikao cha Morogoro kilichounda Kamati hii.

Ndugu Shonza pia hakuhudhuria kikao cha Kamati Tendaji cha juzi kwa madai kuwa amebanwa na shughuli za familia. Baada ya kupitia maelezo yote hayo, Kamati Tendaji iliamua yafuatayo:

Ndugu Juliana Shonza, amepoteza sifa na uhalali wa kuwa mwanachama wa Chadema kwa kukiuka ibara ya 5.3.4 na ibara ya 10.1(ix) ya katiba ya CHADEMA na hivyo imeamua kumuondoa katika nafasi yake ya makamu mwenyekiti na kumfuta uwanachama wake.

Hivyo basi, kwa maamuzi hayo ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya BAVICHA, kuanzia juzi tarehe 5 Januari 2013, Ndugu Juliana Shonza, si mwanachama wa BAVICHA na hivyo moja kwa moja amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa baraza na kwa nafasi yake aliyokuwa nayo ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.

Habib Mchange:

Huyu alituhumiwa kutoa tuhuma za uongo, zikiwemo za mauaji, kinyume na maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); kuunda vikundi vinavyojulikana kwa majina ya MASALIA na PM7 – Pindua Mbowe.

Pia Ndugu Mchange alituhumiwa kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na kuwatukana viongozi, kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha siasa cha CHAUMMA.

Alituhumiwa pia kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na Baraza hivyo kuendelea kukipaka chama matope.

Kamati ilimuita Mchange, na kumhoji juu ya tuhuma zinazomkabili. Hakufika. Badala yake, aliandika barua kueleza kuwa hana imani na kamati:

Aidha, pamoja na Mchange kugoma kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji, Sekretarieti ya Kamati Tendaji Taifa, ilimuita Ndugu Mchange kuhudhudhuria mkutano wa Kamati Tendaji ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mwaliko huu ulifanywa kwa njia ya barua na simu. Njia hizo ndio zilizotumika kualika wahusika wote wakiwamo wajumbe wa Kamati Tendaji,

Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kwamba Ndugu Mchange alikuwa miongoni mwa wanachama wa BAVICHA waliotaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa taifa wa baraza hili. Jina lake liliondolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA, kutokana na kukosa maadili ya uongozi.

Kamati Tendaji baada ya kusikiliza hoja yake hii, ikajiridhisha kuwa mtuhumiwa ameamua kuibuka hoja hiyo ili kutaka Kamati Tendaji isimjadili ili aendeleze mradi wake wa kukichafua chama akiwa ndani ya chama.

Hivyo Kamati Tendaji imefanya yafuatayo: Imempata na hatia ya kuvunja ibara ya 10.3(iii) na kwenda kinyume na kanuni za uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4), kinyume na Maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4) na kwamba mambo yote haya yanadhihirisha kuwa Ndugu Mchange hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama, hivyo kukiuka katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na kuafikiwa uamuzi wa kumfukuza uwanachama wa Bavicha na Chadema.

Mtela Mwampamba:

Huyu ametuhumiwa kutoa tuhuma nzito za uongo hadharani, zikiwemo za mauaji, kinyume kabisa na Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).

Kuvunja katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na Kanuni za Uendeshaji kazi za chama Ibara ya 10.3(4) kwa kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na baraza na kukipaka matope chama pamoja na kudhihirisha kuwa hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama.

3.Amevunja Katiba ya CHADEMA ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 kwa kutoa kauli za kichochezi dhidi ya chama, kuwachonganisha wanachama na kuwatukana viongozi.

4.Kwa kujiunga na vikundi vinavyoitwa MASALIA NA PM7 na baadae kushiriki vikao vya kuanzisha chama cha CHAUMMA, Ndugu Mwampamba amevunja ibara ya 10.3(iii).

5.Kinyume na ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 ya Katiba ya CHADEMA na Ibara ya 4.3(g) na (i) ya kanuni za BAVICHA, zinazopinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Ndugu Mwampamba ameonesha hisia za ubaguzi wa kikabila na kikanda.

Gwakisa Burton Mwakasendo:

Huyu amekuja kwenye kikao na kukiri kutenda makosa yake ambayo takriban yote ni sawa yanayowahusu watuhumiwa waliotangulia hapo juu. Mbele ya kikao cha Kamati ya Utendaji alikiri kushiriki vikao, akisema kuwa ‘lakini’ alilazimika ‘kuikimbia’ dhambi kwa kuondoka katika baadhi ya mikutano na watu hao, wakati mwingine hata nyumbani kwake hakuweza kulala akihisi ‘dhambi’ hiyo anayoikimbia itamfuata nyumbani.

Kamati Tendaji, iliamua kumpa adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka mzima, katika wakati wote huo amezuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya BAVICHA na onyo kali la barua.

Ben Saanane:

Huyu pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa watuhumiwa alipewa adhabu ya onyo kali na uangalizi wa miezi 12, kutokana na makosa yafuatayo. Kutoa tuhuma nzito, zinazomhusu pia Kiongozi wa juu mwandamizi wa chama, Ben amekiuka Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).

Kukiri kuwa mmoja wa waanzilishi wa vikundi vinavyoitwa MASALIA na PM7 na kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha CHAUMMA, amevunja ibara ya 10.3(iii), kwa nia ya kuvuruga chama na kutukana viongozi wake:

Mbele ya Kamati Tendaji, Ben alikiri makosa na akaomba radhi.

Aidha, Ben alitoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati Ndogo jinsi ya kupatikana kwa taarifa na ushahidi wa namna wanachama wa BAVICHA walivyokuwa wanafanya kazi za kundi hili la MASALIA na PM 7 na hasa juu ya majina wanayotumia katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wakifanya juhudi za kuivuruga CHADEMA, kuvuruga BAVICHA, kutukana viongozi na kuwavuruga wanachama, lakini kikubwa wakionesha kila dalili ya tabia ya usaliti.

Exaud Mamuya:


Huyu hajapata nafasi ya kusikilizwa kwenye vikao. Hivyo suala lake litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa BAVICHA.

Aidha, kikao cha Kamati ya Utendaji pia kilipitisha kwa kauli moja, moja ya maazimio ya BAVICHA Mkoa wa Mwanza, waliopendekeza kufukuzwa uanachama kwa aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu, kwa tuhuma za kukiuka Kanuni ya 10.1(xii) kwa kutoa tamko kwenye vyombo vya habari kwa nia ya kumfarakanisha Katibu Mkuu na wanachama wa CHADEMA na umma wa Watanzania, ikiwa ni sehemu ya uratibu wa kundi lililokuwa likiendeshwa na watuhumiwa wengine hapo juu.

Kamati ya Utendaji pia ilimkuta na makosa ya kiuongozi katika tuhuma zilizowasilishwa vikaoni na kufanyiwa kazi na Kamati Ndogo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala na hivyo amepewa adhabu ya onyo kali.

Hitimisho
Tunaomba kuwahakikishia vijana wenzetu wa CHADEMA na wengine wote wapenda mabadiliko nchini, hakuna kijana mwanachama wa BAVICHA, atafanya kazi za kuhujumu baraza na chama kwa ujumla na kusaliti matumaini pekee ya Watanzania, akifanya kazi za mahasimu wetu, kisha akaachwa.

Ni lazima na muhimu tuoneshe kuwa tuna uthubutu kwa kuchukua hatua kadri inavyotakiwa, pale panapotakiwa. Tuliopewa dhamana za uongozi, tutatimiza wajibu kuhakikisha hakuna mtu ataonewa wala kupunjwa haki yake katika kusimamia utendaji na utoaji utumishi bora wa baraza kwa wanachama wake na chama kwa ujumla.

Daima tutasimamia katiba ya chama, maadili, kanuni, taratibu, itifaki na miongozo ya mabaraza. Baraza hili halitakuwa tayari kuwa sehemu ya kuruga matumaini makubwa ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA.

Baraza liko imara. Wanachama wetu wasifadhaishwe na upotoshaji unaofanywa na wasaliti kuwa tumevurugika au ‘kumechafuka’. Hatuwezi kuchafuka wala kuvurugika kwa kuchukua maamuzi dhidi ya watu wabinafsi wanaotaka kukwamisha mapambano ya awamu ya pili, kupigania mabadiliko ya kweli ya kimfumo na kiutawala, kwa ajili ya Watanzania.

Historia inatuonesha kuwa mara zote ambapo mapambano yamefikia hatua ya juu ya kutimiza malengo, ndipo ambapo wasaliti hujitokeza. Hivyo vikwazo hivi vya baadhi yetu kuanza kugeuka nyuma ni dalili za mwisho mwisho kuwa ushindi unakaribia. Ni lazima kama vijana tuendelee kujenga imani na matumaini ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA kutukabidhi dola mwaka 2015.

Mwisho

Imetolewa leo Januari 7, 2013, Dar es Salaam na;
John Heche
Mwenyekiti wa Taifa,
Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)

Monday, October 22, 2012

(CHADEMA)Chaelezea vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala na Zanzibar


 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabele Marando akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam juzi juu ya matukio makubwa yaliyotokea nchini Tanzania yakiwemo yale ya kuchomwa kwa makanisa, maandamano ya wafuasi wa dini ya Kiislamu pamoja na tukio la kutoweka kwa Sheikh Farid wa Zanzibar ambaye kwa sasa amepatikana akiwa hai.
  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
---
IMEELEZWA kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni ni matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la Dar es Salaam wiki hii.
 
Marando alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo kushughulikia matatizo yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha Waislamu wengi wenye msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi kutotawalika.
 
“Kabla ya uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU, kwa ajili ya kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua kuwawekea Waislamu Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue matatizo ya Waislamu wote hayasimamiwi na Bakwata, waitwe Waislamu na waulizwe shida zao,” alisema Marando.
 
Aliongeza kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini walikuwa wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko yoyote, hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa kutoka katika mikono ya wakoloni.
Alisema serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na makundi yote kutafuta muafaka.
 
“Siamini kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo wa serikali unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa, hawasikilizwi hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji Marando.
 
Akizungumzia utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema serikali haiwezi kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa Ikulu kuwa hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.
 
“Sheikh Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu la serikali kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya ulinzi vikisema havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni majibu kama yale yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.
 
Kwa upande wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa serikali imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.
 
“Jeshi la Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka ya Bunge,” alisema Safari.
Aliongeza kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro baina ya Waislamu na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.

Thursday, September 6, 2012

BAVICHA YALAANI MAUAJI YA MWANDISHI WA HABARI MAREHEMU DAVID MWANGOSI.

BARAZA LA VIJANA CHADEMA (BAVICHA) JIMBO LA SEGEREA

TAMKO LA BAVICHA KULAANI MAUAJI YA MWANDISHI WA HABARI MAREHEMU DAVID MWANGOSI.

1.UTANGULIZI
Ndugu wanahabari,BAVICHA jimbo la Segerea limewaita hapa leo 06/09/2012,ili kutoa masikitiko,kulaani na kutoa tamko juu ya vitendo vinavyoendelea kushamiri vya mauaji dhidi ya raia wasio kuwa na hatia.vifo hivi vyenye mashaka vinavyoendelea kutokea mbele ya uwepo wa jeshi la polisi vimeendelea kwa muda mrefu sasa bila ya kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,na vinazidi kuondoa imani ya jeshi hili lenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Matukio ya mauaji ya hivi karibuni yaliyotokea mbele ya jeshi la polisi,mkoani Morogoro (Morogoro mjini) Nyamongo mkoani Mara na tukio la kuuwawa kwa mwandishi wa habari kijiji cha Nyololo mkoani Iringa ni baadhi tu ya matukio mengi yenye mashaka na yanayoleta sintofahamu juu ya utendaji kazi wa jeshi la polisi na kusababisha kutokuaminika tena kwa watanzania.

BAVICHA jimbo la Segerea tunasikitishwa sana na mauaji ya KINYAMA ya mwandishi wa habari,marehemu DAVID MWANGOSI yaliyotokea 02/09/2012
,akitekeleza majukumu yake ya kutafuta habari kwenye tukio la uzinduzi wa tawi la CHADEMA kijiji cha Nyololo,huku akiwa amezungukwa na polisi wengi na wasiweze kumuokoa na kifo hicho.Je kazi yao ilikuwa nini kama siyo kulinda usalama wa raia na kama ni kulinda ilikuwaje DAVID alikufa amemkumbatia moja ya wanausalama hawa?huku wengine wakimshambulia?

Tunashangazwa sana na jeshi la polisi kuzuia mikutano ya ndani iliyokuwa ikifanywa na CHADEMA kwa kisingizio cha kupisha zoezi la sensa ya watu na makazi,wakati likiacha mikutano ya ndani ya CCM wakiendelea na chaguzi za viongozi wa UWT na UVCCM na mikutano ya hadhara wakati zoezi la sensa likiendelea,kwa mfano
Uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa mbunge jimbo la BUBUBU UNGUJA( Uzinduzi huo ulifanywa na Dr Mohamed Ghalib Bilal,UVCCM wilaya ya Temeke na Kinondoni,UWT wilaya ya Temeke-Uchaguzi uliofanyikia PTA hall sabasaba,Mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi uliofanyika jimbo la Mchinga(Mh.Said Mtanda alihutubia),Asha Suleiman Idd(mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Kaskazini B) aliekuwa akifungua mkutano wa UVCCM katika wilaya ya Kindunina mbunge wa Bumbuli mh.January Makamba aliefungua mkutano wa jumuia ya wazazi CCM wilaya ya Lushoto.Wakati matukio haya yote yakifanywa na CCM ni kipindi cha muda wa nyongeza wa sensa ulikuwa ukiendelea.

BAVICHA jimbo la Segerea tunahoji,KATAZO LA POLISI LA KUZUIA MIKUTANO NA SHUGHULI ZOTE ZA SIASA NI KWA CHADEMA TU? Hali hii inatoa picha kwamba jeshi la polisi linatumika kisiasa kwa kuibeba CCM,ni kwa namna gani wataepuka kuitwa POLISISIEMU?hata hivyo kuna dalili tosha kwamba vyombo vya habari navyo vimeanza kujengewa hofu katika kutekeleza majukumu yao,kwa hili la kuuwawa kwa mwandishi akiwa amezungukwa na polisi akitafuta habari kwenye tukio la kisiasa za chadema,tunajiuliza ni kwa vipi walishindwa kulinda usalama wake ili hali wakijua ni mwandishi?ni nani hasa alimuua DAVID MWANGOSI?mbele ya wanausalama waliokuwa na silaha,magari, intelijensia,radio call,kofia za kujikinga,marungu,mabuti na vyote walivyotakiwa kuwa navyo?

Mauaji haya ya KINYAMA katikati ya polisi wengi yanatudhihirishia kwamba wizara hii ya mambo ya ndani inayoongozwa na Emmanuel Nchimbi pamoja na mkuu wa polisi IGP MWEMA wameshindwa kabisa kukomesha tabia ya vifo vya raia vyenye utata na hasa pale vinapotokea mikononi mwa polisi,na kwamba wao ni wadau halali wa kifo cha marehemu DAUD MWANGOSI.


BAVICHA SEGEREA TUNATAMKA KWAMBA

1.TUNAMTAKA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI EMMANUEL NCHIMBI AJIHUZULU KWA KUSHINDWA KUZUIA VIFO VYA RAIA WASIO NA HATIA VINAVYOTOKEA MIKONONI MWA JESHI LA POLISI ,HASA KWA MAUAJI YA MWANDISHI YALIYOTOKEA AKIWA AMEZUNGUKWA NA POLISI WENGI TU.


2.TUNAMTAKA RAIS JK AVUNJE UKIMYA SASA JUU YA TABIA HII YA MAUAJI YA RAIA WASIO NA HATIA KUUWAWA MBELE YA POLISI, KWA KUWAFUKUZA KAZI MARA MOJA IGP SAID MWEMA,MKUU WA OPERATION PAUL CHAGONJA NA RPC WA IRINGA KAMUHANDA ,NAHATA HIVYO RAIS NI MWEPESI SANA KUTOA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA MISIBA INAYOGUSA TAIFA, NI VIPI KWA KIFO CHA DAUD BADO YUKO KIMYA?


3.POLISI KAMA WANAJIFUNZA KUUA RAIA WASIO NA HATIA BASI NASISI TUTAHAMASISHANA KUJIFUNZA KUFA,NA HATUTAOGOPA TENA KUFA KWA KUWA TUNAJUA TUSIPOKUFA LEO,TUTAKUFA KESHO NA TUSIPOKUFA KESHO IPO SIKU TUTAKUFA.


4.SERIKALI YA CCM IACHE KUTUMIA NGUVU YA DOLA KUTISHA ,KULETA HOFU WALA KUDHOOFISHA WANANCHI WASIENDELEE KUKIUNGA MKONO CHAMA CHA CHADEMA,NA TUNA MTAKA KATIBU WA UVCCM TAIFA,MARTIN SHIGELA AACHANE NA PROPAGANDA ZENYE LENGO LA KUPOTOSHA UMMA NA KUTISHA VIJANA WASIKIUNGE MKONO CHADEMA.

5.BAVICHA SEGEREA TUNATANGAZA KUTOKUWA NA IMANI NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA,NA TUNAMTAKA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA JOHN TENDWA AUELEZE UMMA KUNA TOFAUTI GANI KATI YA KAULI YAKE,NA KAULI YA WASIRA NA KAULI YA WAZIRI MKUU BUNGENI(AMBAYO NI YA SERIKALI NA NI YA CCM PIA) ILIYOLENGA KUTISHIA KUIFUTA CHADEMA,ILI HALI WAKIJUA WANAOUA WATU SIO CHADEMA BALI NI JESHI LA POLISI? NA ATUELEZE JE TENDWA NAE ANAKOSA AMANI KUFUATIA CHADEMA KUUNGWA MKONO NA WANANCHI HUKO VIJIJINI? NA MAENEO MENGINE NCHINI.


6.BAVICHA JIMBO LA SEGEREA TUNATOA RAI KWA VIJANA WOTE TANZANIA WANAOHITAJI MABADILIKO NA WENYE MTIZAMO CHANYA WA UKOMBOZI KUTOKA MIKONONI MWA MAFISADI, KUWA TAYARI KUPAMBANA NA NAMNA YOYOTE YA UONEVU,UKANDAMIZAJI,UDHALILISH AJI NA UBAGUZI WA NAMNA YOYOTE ILE.


Imetolewa leo na uongozi wa BAVICHA (J) SEGEREA
Daniel Raymond
M/Kiti

Monday, September 3, 2012

Mkutano wa CHADEMA DMV Marekani


Hussein Kauzera katibu Mwenenzi wa Tawi la Chadema DMV,
Mwenyekiti wa Chadema DMV Cosmas
Katibu wa Chadema DMV Ndg Isidory Lyamuya akihutubia katika Mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chadema DMV Ndg Cosmas Wambura akihutubia katika mkutano wa Chadema Washington DC.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema DMV Ndg Mariam Khamis akiwa katika mkutano wa Chadema DMV.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa Ndg Freeman Mbowe akihutubia Watanzania waishio Washington DC, Marekani.
Mbunge wa Mbeya Mjini Ndg Joseph Mbilinyi akihutubia Watanzania Waishio Washington DC, Marekani.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Chadema DMV Ndg Kalley Pandukizi akitoa Risala ya Historia ya Tawi la Chadema DMV.
MC Sunday Shomari akiongea mawili matatu katika Mkutano wa Chadema DMV.
Katibu wa Baraza la Wanawake Ndg Baby Mgaza akihutubia katika mkutano huo.
Pichani Viongozi wa Chadema DMV wakiwa katika mkutano Washington DC.
Mkatibu Mwenenzi wa Tawi la CCM DMV Benjamin Mwaipaja kiwa na Kada wa chama Chadema Emmanuel Muganda akimkaribisha kwa upendo katika mkutano huo.

Namalizia kwa wana DMV kufikisha ujumbe huu rasmi uliotolewa na Mh. Freeman Mbowe ''Rai yangu kwenu, mlio Chama cha Mapinduzi CCM, mlio Chadema, hivi vyama vya Siasa visitugombanishe''.
Baadhi ya Watanzania waliojitokeza kwenye mkutano wa Chadema DMV.Picha Zote na habari na CHADEMA-SwahiliVilla

Sunday, September 2, 2012

Dk Slaa:Tutaendelea na Mikutano Yetu Kama Tulivyopanga na Tupo Tayari Kwa Lolote

Wakati jeshi la polisi likipinga shughuli hizo za vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara katibu mkuu wa Chadema Taifa Dkt Willbroad Slaa ameibuka na kusema kuwa chama chake kitaendelea na mikutano kama kilivyojipangia na kuwa wapo tayari kwa lolote litakalojitokeza .

Dkt Slaa alisema kuwa walivumilia mara ya kwanza walipozuiwa mikutano hiyo mkoani Iringa na kuvuta subira hadi jumamosi zoezi hilo lilipomalizika sasa anashangazwa kuona jeshi hilo likiendelea kuzuia mikutano hiyo tena.

"Tumemsikiliza kamishina wa sensa Hajati Amina Mrisho Said kuwa hadi sasa watu asilimia 95 wameandikishwa huku akiwata wale ambao bado kuwapigia simu wenyeviti wa mitaaa na vijiji ili wakaandikishwe na makarani wa sensa ....sasa jeshi la polisi linataka kutuambia kuwa hao watu asilimia 5 waliobaki wapo Iringa peke yake hadi wakazuia mikutano yetu? tunasema hatutakubali tutaendelea na mikutano yetu kama kawaida hatupotayari kabisa kusubiri hadi tarehe nane" alisema Dkt Slaa.

Pia alisema kuwa kama ni uzalendo sasa umefika kikomo na kuwa wataendelea na ratiba zao za mikutano kama ilivyopangwa na watapambana kwa lolote .

MWISHO

Vurugu Baina ya Wafuasi wa Chadema na Polisi katika kijiji cha Nyololo, Mufindi

Hapa polisi wakiwataka wafuasi wa Chadema kutawanyika eneo la tukio ofisi za Chadema Nyololo Mufindi
Mmoja wa askari wa kutuliza ghasia ffu akipita mbele ya ofisi za Chadema Nyololomuda mfupi baada ya kupiga bomu la machozi
Daud Mwangosi kulia enzi za uhai dakika 20 kabla ya kuuwawa kwake
Sehemu ya wafuasi wa chadema wakiwa kwenye ofisi za Chadema Nyololo
Mwili wa mwanahabari Daud Mwangosi ukiwa chini
Sehemu ya magari matano ya Chadema yaliyoharibiwa vibaya kwenye vurugu hizo.Picha zote na Habari na Mdau Francis Godwin-Iringa

Friday, August 31, 2012

TAMKO LA CHADEMA KUHUSU MAUAJI MKOANI MOROGORO

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).

Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.

Hivyokutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi wa kina.

Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao eneo la Msamvu, hivyo kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.

CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.

CHADEMA hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.

CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.

Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na kudondoka.

Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.

Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.

Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.

CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.

Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio cha Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.

Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la Polisi liliikubali.

Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia limekataza maandamano.

CHADEMA kikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.

Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu za misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.

Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.

Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.

Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.

Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi yafanyike kwa msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na vyombo vingine vya usafiri.

Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo yasingetokea madhara yoyote.

Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.

CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.

CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.

Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.

Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano yanayoendelea na familia.

CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.

CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio hicho.

Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe hiyo.

Tume hiyo inaendelea na mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.

CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.

CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.

Imetolewa
tarehe 29 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Dkt Slaa akutana na waandishi wa Habari Mkoani Iringa

katibu mkuu wa Chadema Dkt Slaa akionyesha baadhi ya vielelezo kwa wanahabari leo mjini Iringa
Dkt Slaa akiwa katika mkutano wake na wanahabari mkoa wa Iringa katika ukumbi wa Hoteli ya M.R

Katibu mkuu huyo wa Chadema Taifa Dkt Slaa ameibua mambo mazito juu ya waziri Sitta na serikali yake katika mkutano huo na kueleza mikakati mbali mbali ya Chadema .

Monday, August 27, 2012

MKUTANO WA CHADEMA MOROGORO MJINI

Katibu mkuu wa Chama chama cha Demokrasi na Maendeleo Dkt Wilbrord Slaa akihutubia wananchi wa Manispaa ya Morogoro katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ndege mkoani Morogoro.
Katibu mkuu wa Chama chama cha Demokrasi na Maendeleo Dkt Wilbrord Slaa akiongoza umati uliohudhuria mkutano wa hadhara wa Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) baada ya mtu mmoja kudaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia wakati wengine wawili nao wakidaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa na risasi na askari wa jeshi la polisi.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5 asubuhi eneo la Msamvu barabara kuu Dar es Salaam-Morogoro wakati askari hao wakiwatawanya umati mkubwa wa wanachama na wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakisubiri viongozi wa juu wa chama hicho ili waandamane kuelekea katika mkutano wa hadhara uwanja wa Ndege mkoani Morogoro leo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa, akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Morogoro na vitongoji vyake, katika mkutano wa hadhara wa operesheni sanga ,kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Morogoro waliojitokeza katika mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti Chadema Zanzibar Said Issa Mohamed akifafanua jambo kwa wananchi hao.
Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Igunda kupitia Chadema, Joseph Kashinde akizungumza na wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Mbunge wa viti Maalum Chadema Suzan Mungi akimwaga sera za chama hicho.
Mbunge wa jimbo la Ubungo Jijini Dar es Salaam John Mnyika akipanda jukwaani wakati akiwasili katika uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Sehemu ya umati ambao ni wakazi wa Manispaa ya Morogoro na vitongoji vyake katika mkutano huo.Picha Zote na Juma Mtanda

MKUTANO WA CHADEMA KINGORWILA MKOANI MOROGORO

Baadhi ya wananchi wa Kingorwila, mkoani Morogoro, wakimsikiliza mmoja wa viongozi wa Chama cha CHADEMA, wakati akimwaga sera za chama chake katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika juzi mkoani humo. Picha na Mpigapicha Wetu

Popular Posts