Pages

Tuesday, April 9, 2013

Bunge lijadili ripoti za CAG kwa Uwazi


Taarifa kwa Vyombo vya Habari, April 09, 2013

Bunge lijadili ripoti za CAG kwa Uwazi

Sikika inapenda kuamini kwamba taarifa zilizochapishwa kwenye magazeti mbali mbali kuhusu Bunge kutojadili ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mkutano huu wa 11, ama ‘zimenukuliwa vibaya’, au aliyezitoa alikuwa hajawasiliana kikamilifu na viongozi wa juu wa Bunge.

Iwapo habari kwamba Bunge halitajadili ripoti za CAG katika mkutano ni za kweli, basi Bunge limejitenga na wananchi na pia limejipunguzia madaraka yake ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Kwa lugha nyingine, Bunge litakuwa limewaasi wapiga kura wake.

Takribani miaka kadhaa mfululuzo, CAG amekuwa akilalamika kwamba serikali haitekelezi mapendekezo na ushauri wake katika kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma. Matatizo mengi ambayo CAG amekuwa akiibua katika ripoti zake kuhusu matumizi ya fedha za umma yamekuwa yakijirudia. Sikika inaamini kwamba kutojadiliwa kwa ripoti za CAG bungeni kwa uwazi kunalenga kuficha mapungufu haya ya serikali.

Katika mkutano wa 10 wa Bunge, tulishuhudia mabadiliko makubwa ya namna Bunge linavyoisimamia na kuiwajibisha serikali, ambayo hata hivyo hayakutafuta baraka za wananchi. Wananchi wameiajiri serikali na wameliweka Bunge kuisimamia na kuiwajibisha serikali kwa niaba yao. Bunge halina mamlaka ya kujiondolea au kujipunguzia majukumu ambayo linatekeleza kwa niaba ya wananchi bila kupata baraka za wananchi.

Katika mabadiliko hayo, mojawapo ni hili la kutokujadili ripoti za CAG ndani ya Bunge. Kifungu cha 63.3.b cha Katiba ya JMT kinalitaka Bunge kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti. Mkutano huu wa sasa wa Bunge ni wa Bajeti.

Kipengele hicho cha Katiba hakikutaja Kamati za Bunge bali Mkutano wa Bajeti. Hivyo hata kama ripoti hizi zitapitiwa kwenye Kamati za Bunge, ni lazima, kwa mujibu wa Katiba zikajadiliwa kwenye Mkutano wa Bunge. Hapo wabunge wote na wananchi watapata fursa ya kujua nini kilichojiri katika kila ripoti ya CAG. Pia mjadala huo utanukuliwa katika kumbukumbu rasmi za Bunge yaani Hansad ambayo iko wazi kwa wananchi kuipitia muda wowote.

Mabadiliko ya pili yalihusu kubadilisha muundo na majukumu ya Kamati za Kudumu za Bunge. Katika mabadiliko hayo, Kamati ya Mashirika ya Umma ilifutwa na baadhi ya majukumu yake kuunganishwa kwenye kamati Hesabu za Serikali Kuu (PAC)

Majukumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo hayakuhamishiwa kwenye Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ni lile la kushughulikia ubinafsishaji na pia jukumu la kufanya tathmini ya mashirika ya umma. Majukumu haya mawili ni ya msingi kabisa katika kuwezesha wananchi kujua kinachoendelea katika ubinafsishaji ambao umelalamikiwa sana jinsi ulivyoendeshwa, na pia kujua ufanisi wa mashirika ya umma kwa ujumla.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba mabadiliko yote mawili yalikusudia kuongeza usiri kwa namna serikali inavyotumia madaraka na mali za umma, hivyo kulifanya Bunge kukosa

mamlaka yake, na kuwafanya wananchi kushindwa kuiwajibisha serikali. Pia inawezekana Bunge limevunja Katiba kwa kujipunguzia majukumu yake kikatiba. Pia ni wazi kwamba Bunge limeasi wananchi waliolichagua kwa kujivua jukumu la kuisimamia serikali.

Sikika inalitaka Bunge kurejea kwenye misingi ya majukumu yake kwa sababu majukumu hayo limepewa na wananchi. Bunge halina mamlaka ya kujipunguzia majukumu ya msingi lililopewa na wananchi bila ridhaa ya wananchi wenyewe. Iwapo Bunge linaamini lina mamlaka ya kufanya mabadiliko hayo na kwamba ndiyo njia bora ya kuongeza uwajibikaji wa serikali, litafute ridhaa ya wananchi kwanza.

Mwisho, Sikika inashauri mijadala inayohusu ripoti za CAG, mapendekezo ya bajeti ya serikali, mapato na matumizi, utekelezaji wa mipango na bajeti za mwaka uliotangulia lazima zijadiliwe katika mkutano wa Bunge ulio wazi ili wananchi nao waone namna wawakilishi wao wanavyotekeleza wajibu wao wa kusimamia fedha za walipa kodi.

Bw. Irenei Kiria

Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S. L. P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz

Popular Posts