Pages

Showing posts with label Dini - Religion. Show all posts
Showing posts with label Dini - Religion. Show all posts

Thursday, December 27, 2012

TAMKO LA MAASKOFU WA TANZANIA KUHUSU AMANI YA TANZANIA


TANZANIA CHRISTIAN FORUM (TCF)
MKUTANO MKUU WA NNE WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA (TCF)

TAMKO RASMI 

“ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA”

Utangulizi
Katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, Tanzania Christian Forum – TCF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba, 2012; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na Utume wake wa Kinabii kwa taifa letu.

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini kama ifuatavyo;-
Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania - TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania - PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (observers)

Tafakari
Tafakari yetu ilianza kwa kujiuliza yafuatayo:
1. Ni mwenendo gani uliotusibu hivi karibuni kusababisha kukutana kwetu hapa?
Vikundi vya kihalifu vikiongozwa chini ya mwavuli wa waamini wa Kiislamu vimekuwa vikishambulia kwa ukali na kikatili sana imani, mali, majengo na makanisa ya Wakristo kwa jeuri na kujiamini.

2. Kwa mwenendo huo ni kitu gani kilicho hatarini?

Vitendo na mienendo yote ya namna hiyo inahujumu sana Amani, Mapatano na Uelewano kati ya watu wote nchini mwetu. Tunaelewa kwamba ni waamini wachache tu wenye kutenda maovu hayo, lakini mienendo ya kikatili ya namna hii huchochea shari miongoni mwa walengwa wa ukatili husika na kutaka kulipiza kisasi hata kusababisha uvunjifu wa amani.3. Ni athari gani kwa nchi, katika muda ujao, iwapo mienendo hiyo haitadhibitiwa na kukomeshwa kabisa?

Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chinichini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni. Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa maslahi ya wanyemelezi. Hali tunayoelezea sio ya kufikirika kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa. Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii. Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza maslahi yao.4. Masuala yanayotakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na Dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa:

  • Hali ya mahusiano kuzorota pamoja na kashfa dhidi ya Kanisa.

Huu ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi na makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu, ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vyao vya habari vya kidini (redio na magazeti) mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na hata viongozi wa dini husika (ushahidi wa mambo yote haya tunao) pasipo Serikali kuchukua hatua yeyote huku bali imekuwa ikibakia kimya tu. Ukimya huu unatoa taswira ya Serikali kuunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi linaashiria hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.
  • Hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa.

Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila ubaguzi wowote, akiimarisha umoja wa Kitaifa, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kukipotosha kizazi hiki na hata vizazi vijavyo kwa kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa.
  • Memorandum of Understanding” (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za kijamii zitolewazo na Makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa nchini kote. Ni vema ikaeleweka wazi kwamba makubaliano hayo (M.o.U) yalikuwa ni kati ya Makanisa ya Tanzania na Makanisa ya nchini Ujerumani ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa tu, kwa vile raia wake ndio wangenufaika na misaada hiyo ambayo nchi ya Ujerumani ingeitoa kupitia Makanisa hayo. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi. Ikibidi ni vema kuondoa hali hii, ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa viongozi wake kutokana na huduma hizi kwa jamii yote. Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana yake, makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania wote.


  • Hujuma ya kuchomwa Makanisa na mali za Kanisa, ni tukio la uvamizi na uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa yetu na waamini wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote. Ni muhimu kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.


  • Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo ni potofu na potevu.

Maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waamini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potovu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na Serikali yetu. Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo!. Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo! Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi ngazi za juu Serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya Utawala wa Kisheria na sio vinginevyo.
  • Matumizi hasi ya Vyombo vya Habari vya Kidini:

Vyombo vya habari vya kidini vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislam kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu hadharani kupitia vyombo hivyo wakiwataka wawaue Maaskofu na Wachungaji, iwe kwa siri au hadharani. Japo Serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imendelea kukaa kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti. Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya umakini wa Dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waamini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa Serikali na viongozi waliopo madarakani, endapo waamini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo na waamini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inapelekea kujiuliza kama je,huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waamini wake dhidi ya wenye imani kali?
  • Matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu:

Tumejionea matukio kadhaa ambayo kwayo vikundi vya watu wenye hasira vilisababisha hujuma na uharibifu mkubwa wa mali za watu wengine. Hivyo ni viashiria tosha vya uchovu na unyonge mkubwa katika jamii yetu, ambamo jambo dogo tu na hata la kupuuzwa, likitendwa na afikiriwaye kuwa hasimu wa watu fulani, wahalifu hujipatia fursa ya kuonesha hasira yao kwa vitendo vya hujuma na shari, wakiharibu hata kuteketeza mali na nyenzo za maisha ya jamii. Suala hili lataka uchambuzi yakinifu na wa kiroho ili kupata majibu na maelezo sahihi na wala sio kwa kutumia nguvu za ziada za kijeshi au kwa majibu mepesi ya kisiasa. Hili ni suala lihusulo tunu na maadili ya jamii yote ya Watanzania katika ujumla wao. Kila mmoja wetu ni mhusika na sote tukitakiwa kuwajibikiana katika ujenzi wa amani iletayo mapatano na uelewano kati yetu.

Mapendekezo:
Kutokana na muono wetu huo tunapendekeza yafuatayo:

  • Tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa na badala yake tujengeane heshima/staha tukizingatia utu wa kila mmoja katika utofauti wetu.
  • Tumwendee Mungu wetu na kumwomba atuongoze sote kufuata utashi wake tukitafuta huruma yake iliyo sheheni upendo wake mkuu, ili atujalie umoja wa kuishi pamoja kwa amani nchini mwetu.
  • Tunaitaka Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na Dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji. Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.
  • Lianzishwe Baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza Serikali kuto fungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote havipotoshwi. Baraza hilo liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama itokeapo matatizo makubwa yaashiriayo uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi.
  • Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislam, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya waamini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo. Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada zetu sote tutambue , tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za watu wengine wanazo ziheshimu na kuzitukuza. Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na usalama wa taifa. Stahamala [kustahimiliana] ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana.


Hitimisho: 
Kwa sasa Kanisa liko katika vita vya Kiroho, hivyo ni vyema Waamini wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu mwenyewe, Mwenye enzi yote ndiye mlinzi wa watu wake na Kanisa lake.
JIBU LITAPATIKANA TU, KWA NJIA YA SALA, KUFUNGA NA MAOMBI!
Hivyo siku ya Jumanne tarehe 25 Desemba 2012, inatangazwa rasmi nchini kote kuwa siku ya sala na maombi kwa Wakristo wote na Makanisa yote nchini, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba kwa imani, amani katika nchi yetu, na kumkabidhi Mungu ashughulikie mipango yoyote iliyopo, ya wazi na ya kisirisiri ya kutaka kuondoa amani ya taifa hili na kuyashambulia Makanisa nchini Tanzania ishindwe na kuanguka pamoja na wale wote walio nyuma ya mipango hiyo.

1. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mwenyekiti
2. Askofu Dkt. Israel Mwakyolile (CCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
3. Askofu Daniel Aweti (PCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
4. Askofu Oscar Mnung’a (CCT) - Mjumbe
5. Askofu Elisa Buberwa (CCT) - Mjumbe
6. Askofu Stephen Mang’ana 
(CCT) - Mjumbe
7. Askofu Dkt. Peter Kitula 
(CCT) - Mjumbe
8. Askofu Alinikisa Felick Cheyo 
(CCT) - Mjumbe
9. Askofu Christopher Ndege 
(CCT) - Mjumbe
10. Askofu Michael Hafidh 
(CCT) - Mjumbe
11. Askofu Charles Salala 
(CCT) - Mjumbe
12. Askofu Dismus Mofulu 
(CCT) - Mjumbe
13. Mchg. Conrad Nguvumali 
(CCT) - Mjumbe
14. Mchg. Ernest Sumisumi 
(CCT) - Mjumbe
15. Mchg. William Kopwe 
(CCT) - Mjumbe
16. Askofu Thaddaeus Ruwa’ichi (TEC) - Mjumbe
17. Askofu Paul Ruzoka 
(TEC) - Mjumbe
18. Askofu Norbert Mtega 
(TEC) - Mjumbe
19. Askofu Severine Niwemugizi 
(TEC) - Mjumbe
20. Askofu Michael Msonganzila 
(TEC) - Mjumbe
21. Askofu Castorl Msemwa 
(TEC) - Mjumbe
22. Askofu Eusebius Nzigilwa 
(TEC) - Mjumbe
23. Askofu Renatus Nkwande 
(TEC) - Mjumbe
24. Askofu Bruno Ngonyani 
(TEC) - Mjumbe
25. Fr. Antony Makunde 
(TEC) - Mjumbe
26. Fr. Sieggried Rusimbya 
(TEC) - Mjumbe
27. Fr. Ubaldus Kidavuri 
(TEC) - Mjumbe
28. Askofu Dkt. Paul Shemsanga (PCT) - Mjumbe
29. Askofu Ability Samas Emmanuel 
(PCT) - Mjumbe
30. Askofu Nkumbu Nazareth Mwalyego 
(PCT) - Mjumbe
31. Askofu Batholomew Sheggah 
(PCT) - Mjumbe
32. Askofu Dkt. Mgullu Kilimba 
(PCT) - Mjumbe
33. Askofu Renatus Tondogosso 
(PCT) - Mjumbe
34. Askofu Emmanuel Mhina 
(PCT) - Mjumbe
35. Askofu O.S. Sissy 
(PCT) - Mjumbe
36. Askofu Jackson Kabuga 
(PCT) - Mjumbe

Thursday, October 18, 2012

SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.



Wapendwa Katika Bwana,
Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla.

Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.

Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika eneo hili la Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimissioni vya Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili kufika hapa Mbagala. Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu:
  1. Tumekuja kuwapa pole na kusimama pamoja nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu ni machozi yetu. Machozi yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33).
  2. Tumekuja kuonyesha majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani, kuporomoka kwa umoja na mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa, na wenye msiba ni watanzania wote, wenye dini na wasio na dini.
  3. Tumekuja kushiriki pamoja nanyi kupokea matumaini ya Tanzania mpya. Katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa. Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo na dini.

Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa kufanya haya yafuatayo:
  1. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na ruhusa kutoka mamlaka zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
  2. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu ya dini; wawe wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi wao binafsi ili kupata kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini.
  3. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali za makanisa kwa kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo tunamwachia Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.

Wapendwa wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa Tanzania ya Julius Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni kebehi kwetu sisi wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala baada ya kazi njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania aliyoijenga.

Kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari, yaani mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa matunda machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa. Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
  • Uchochezi wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili.
  • Ubishi usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa nchini na hata kudiriki kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania. Lengo la ubishi huu ni mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya kimbari na mateso ya kanisa.
  • Matumizi mabaya ya baadhi vyombo vya habari, vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini miongoni mwa watanzania
  • Ukimya wa vyombo vya dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya matumizi ya vyombo vya habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari, mateso kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache dhidi ya wengi.
  • Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama:
  •  

  1. Kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala katika mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi?
  2. Madai yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa nchini. Madai haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa nchini.
  3. Madai na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini
  4. Mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria.
  5. Mashinikizo ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma,
  6. Kuhoji na kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini

Wapendwa wana KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama wanaofanya mambo haya ya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana harakati”, tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na watanzania walio wengi, tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao usitumike kuvunja nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.

Kwa macho na masikio yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na waoga, hufika wakati wakasema “sasa basi” pale wanapodhalilishwa kupita kiasi. Hatuombei wakristo wafikishwe hapo.

Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa sababu ya zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu?

Sisi tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana waumini wa dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii na wasiolazimika kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake. Kamwe hawezi kuliacha liangamie.

Kwa Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine.

Katika mateso haya, kanisa litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo wote kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya kuomba na kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa, imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16).

Daima tukumbuke kuwa, “KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO” (Waefeso 6: 12).

Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu,
  1. Askofu Dr. Alex G. Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani
  2. Askofu Dr. Stephen Munga –Mkuu, D/Kaskazini Mashariki
  3. Askofu Dr. Martin Shao – Mkuu, D/Kaskazini
  4. Askofu Dr. Thomas Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati
  5. Askofu Dr. Benson Bagonza- Mkuu, D/Karagwe
  6. Askofu Isaya J. Mengele – Mkuu, D/Kusini
  7. Askofu Levis Sanga – Mkuu- D/Kusini Kati
  8. Askofu Elisa Buberwa – Mkuu –D/Kaskazini Magharibi
  9. Askofu Andrew Gulle – Mkuu, D/Mashariki ya Ziwa Victoria
  10. Askofu Michael Adam –Mkuu, D/Mkoani Mara
  11. Askofu Renard Mtenji – Mkuu, D/Ulanga-Kilombero
  12. Askofu Dr. Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde
  13. Askofu Job Mbwilo – Mkuu, D/Kusini Magharibi
  14. Askofu Dr. Owdenburg Mdegella- Mkuu, D/Iringa
  15. Askofu Jacob Ole Mameo- Mkuu, D/Morogoro
  16. Askofu Zebedayo Daudi – Mkuu, D/Mbulu
  17. Askofu Paulo Akyoo – Mkuu, D/Meru
  18. Askofu Charles Mjema – Mkuu, D/Pare
  19. Askofu Mteule Amon Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma
  20. Askofu Mteule Dr. Alex Mkumbo- Mkuu, D/Kati

Thursday, September 6, 2012

MWILI WA KARDINALI LAUREAN RUGAMBWA KUZIKWA UPYA OKTOBA 6, BUKOBA

Marehemu Kardinal Laurean Rugambwa enzi ya uhai wake.
Kanisa kuu katoliki jimbo la Bukoba ambalo masalia ya marehemu kardinali Rugambwa yatazikwa ndani yake.

*************
MWILI WA KARDINALI LAUREAN RUGAMBWA KUZIKWA UPYA OKTOBA 6, BUKOBA

Kanisa katoliki nchini dayosisi ya Bukoba mkoani Kagera, wanajiandaa kuzika upya masalia ya mwili wa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo Kardinali Laurean Rugambwa, aliyefariki mnamo mwaka 1997 katika kanisa kuu la Bukoba. Maziko ya Kadinali Rugambwa yamepangwa kufanyika siku ya oktoba 6 mwaka huu.

Mwili wa askofu huyo wa kwanza nchini na Kardinali wa kwanza mweusi barani Afrika umezikwa katika kanisa la kwanza mkoani Kagera lililopo Kashozi kutokana na kwamba kanisa kuu la Bukoba ambalo marehemu aliagiza kuzikiwa ndani yake lilikuwa katika matengenezo makubwa.

Akizungumza katika kipindi cha Baragumu Channel ten na baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba Askofu Methodius Kilaini , amesema wanataka kumzika kardinali Rugambwa kwa heshima tena katika kanisa alilopenda kuzikiwa kutokana na kukamilika kwake, lakini kabla ya kuzikwa humo kutatanguliwa na ibada mbalimbali ikiwa sehemu alikozaliwa, alikobatizwa, sherehe zitakazoambatana na kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa kardinali Rugambwa tarehe 7 mwezi Octoba.

"tuna alika watu wengi kuhudhuria kwenye tukio hili..., na pia tunakaribisha michango itakayowezesha kuwa na kitu cha kumkumbuka marehemu kwa mchango wake,alisema askofu Kilaini.

Naye mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo , James Rugemalira, alimwelezea Kardinali Rugambwa kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kwenye jamii ya watanzania, kuanzia kwenye nyanja za elimu, afya na kiroho.

Marehemu Kardinali Rugambwa ana mambo mengi ya kukumbukwa na jamii ya watanzania hususani watu wa mkoa wa Kagera hasa kwa juhudi zake za kupeleka elimu mkoani humo kwa kuagiza ujengwaji wa shule za msingi na sekondari ikiwemo shule ya kwanza ya wasichana ya Rugambwa ambayo ujenzi wake ulikuwa ni mafanikio ya marehemu huyo kuomba msaada wa ujenzi wa shule hiyo alipohutubia bunge la Ujerumani akiwa mwafrika wa kwanza.

Licha ya mambo hayo yote kanisa hilo pia liko mbioni kuanzisha mfuko rasmi wa kumuenzi kardinali huyo mfuko utakaojulikana kwa jina la Kardinali Rugambwa ambao utakuwa maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Padre Laurean Rugambwa aliwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 10 Februari,1952. Alizaliwa julai 22 1912 na kufariki miaka 15 iliyopita.

Monday, August 27, 2012

KWANINI WAISLAMU HAWANA IMANI NA VITENGO VINAVYOHUSIKA NA TAKWIMU?

Hili ni suala muhimu kulipatia jibu na kulifahamu kwa kina sisi kama Waislamu. Wengi wana maoni kuwa kitendo cha Waislamu kuomba kushirikishwa katika Sensa na kuomba kuingizwa kwa swali la Dini ni ukorofi tu wa Waislamu. Ukweli unafichwa na makala hii ina lengo la kuwajuza watu vipengele kadhaa juu ya hila katika sensa zilizopita.

Makala hii itadhihisha "uchakachuaji uliofanyika na ofisi za serikali katika kutangaza mgawanyiko wa watu kwa mujibu wa dini kabla ya serikali ya Mwalimu Nyerere kuamua kulifuta swali la dini katika sensa ya Tanzania iliyofanyika mwaka 1978.

Tanganyika au Tanzania imeshafanya sensa mara 6. Mara mbili za mwanzo sensa ilifanyika kama Tanganyika chini ya mkoloni wa Kiingereza yaani mwaka 1948 na mwaka 1957. Kisha sensa nne zilizobaki zilifanyika Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zikiwa zimeshaungana. Sensa ya mwanzo ya Tanzania huru iliyoungana iifanyika mwaka 1967 na hii ilikuwa ni sensa ya mwisho kuuliza swali la dini. Sensa zilizobaki zilifanyika mwaka 1978, 1988 na 2002. Sensa ya mwaka huu, 2012 itakuwa ni ya saba katika historia ya nchi yetu na ya tano ya Tanzania huru iliyoungana.

Sensa ya mwisho ya Tanganyika chini ya mkoloni wa Kiingereza katika mwaka 1957 ilionyesha kuwa Tanganyika ina Waislamu 58%, Wakristo 32% na Wapagani 10%. Uwiano kati ya Waislamu na Wakristo ilikuwa ni karibu 2:1 yaani kila penye watu watatu, 2 ni Waislamu na 1 ni mkristo, vile vile unaweza kusema waislamu walikuwa ni karibu mara mbili ya wakristo kiidadi Tanzania.

Mwaka 1967 ndio uliotoa matokeo ya ajabu ambayo mpaka leo sio tu Waislamu bali mtu yoyote aliye na akili timamu ana haki ya kuhoji matokeo hayo. Matokeo haya yalionyesha mgawanyiko wa kidini kama ifuatavyo:

WAKRISTO: 33.5% yaani wameongezeka kwa 1.5% kulinganisha na sensa ya 1957.

WAISLAMU: 31.4% yaani wamepungua kwa 26.6% katika kipindi cha miaka 10 tu. Hii haikuwahi kutokea sehemu yoyote Duniani iwapo sehemu hiyo haikukabiliwa na janga kama vile vita au jambo lolote lilisababisha idadi kubwa ya watu kufariki. Hata china ambayo imeweka sheria ya kuzaa mtoto mmoja tu basi haikuwahi kupungikiwa na watu au kundi fulani la watu katika nchi yao.

WAPAGANI: 34.3% yaani wameongezeka kwa 24.3% kwa kipindi cha miaka 10. Haya nayo ni maajabu, yaani unaweza ukadhani labda Tanzania ina tatizo la Waislamu kuwacha dini yao na kuwa wapagani. Hili nalo halina ushahidi wowote kuwa lilitokea katika kipindi hicho.

Athari kubwa ya kimabadiliko iliyotekea katika sensa hii ni kujumuishwa kwa Wazanzibari katika sensa kwa mara ya kwanza. Kwa vile Wazanzibari karibu 98% ni Waislamu tegemeo lilikuwa Waislamu Tanzania wapindukie angalau 65% (kutoka 58% ya mwaka 57 ambayo haikujumuisha Wazanzibari) ya watu wote lakini badala yake wakashuka hadi 31.4%

Tukumbuke kuwa Waislamu ndio watu ambao mara nyingi hulaumiwa kutofuata uzazi wa majira, hulaumiwa kwa kuozesha mabinti zao mapema na ni dini inayoruhusu mume mmoja kuoa wake wanne, haya yote hupelekea ongezeko kubwa la idadi, lakini ajabu ni kuwa Waislamu walipungua, si kwa asilimia 2 - 3% bali kwa 26.6%!

Hivyo ni wazi Takwimu zilizotolewa na serikali ya Mwalimu Nyerere ama zilikuwa ni za uongo wa makusudi ya kupotosha au zina makosa. Lakini cha kushangaza ni kuwa baada ya sensa hiyo Serikali ya Mwalimu Nyerere iliamrisha kipengele cha dini kuenguliwa kwenye sensa bila ya kueleza Watanzania lengo la kukiondoa kipengele hicho. wakati huo tayari Tanzania ilishaanza kugubikwa na wingu la udini baada ya Mwalimu Nyerere kuamua kuivunja Jumuiya adhimu ya Waislamu East Africa Muslim Walfare Society (EAMWS) na serikali kuunda Jumuiya ambayo mpaka leo waislamu wana mashaka nayo ambayo ni BAKWATA. Naomba sana tuzingatie nukta hii kuwa BAKWATA haikuundwa na Waislamu bali iliundwa na Serikali iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere.

Kudhihirishwa kuwa mwaka 1967 udini ndio ulikuwa unaanza kushamiri Tanzania sio tu katika sensa na kuvunjwa kwa EAMWS na kuundwa kwa BAKWATA, mwaka 1967 ndio mwaka wa Azimio la Arusha na mwaka wa kesi ya uhaini iliyojumuisha Waislamu na wengi wakawekwa rumande kwa tuhuma hizo akiwemo wanasiasa maarufu ambao waliiunga mkono EAMWS akina marehemu Bibi Titi Muhammed na Tewa Said Tewa.

Hivyo leo utaweza je kuwalaumu Waislamu kwa kukosa imani na serikali katika hoja ya sensa? Mara nyingi panapotokea badiliko kubwa kama lile ambalo linaaminika kuwa ni la kuchakachuliwa yaani Waislamu kupungua Tanzania kwa 26.6% na wapagani kuongezeka Tanzania kwa 24.3 katika kipindi cha miaka 10 (jambo ambalo mtaalamu yoyote wa sensa au takwimu hawezi kukubaliana nalo) palitegemwa pfanyike utafiti wa sababu za mabadiliko hayo, lakini hakuna aliyeamua kufanya hivyo na sababu kuu ni kuwa watu walijua wazi kuwa takwimu hizo ni za kupika.
Source: Mapara
Na Ndugu Mohamed Said anaandika juu ya KITENDAWILI CHA SENSA TANZANIA na anaelezea kuwa:
Theluthi mbili ya Waislam wote wa Afrika ya Mashariki wanaishi Tanzania mbayo ndiyo nchi yenye watu wengi kuliko zote katika Afrika ya Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni pamoja na nchi ya Kiislam yenye Waislam takriban 90% na kuna wakati ilikuwa ndiyo kitovu cha maarifa ya Kiislam katika Afrika ya Mashariki na Kati. Kutokana na sensa ya mwaka 1957, kwa kila Waislam watatu walikuwepo Wakristo wawili. Kwa wakati ule hii ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na Waislam wengi katika nchi zote Kusini ya Ikweta. Lakini katika sensa ya kwanza mwaka 1967 baada ya uhuru jumla ya Wakristo Tanzania Bara ilikuwa asilimia 32 % na Waislam 30% Wapagani asilimia 37%. Sensa hii inaonyesha kuwa Wapagani ndiyo walio wengi Tanzania. Sensa hii ya mwaka 1967 haikueleza kwa nini katika kipindi cha miaka kumi kwa ghafla Waislam wamepungua nchini au kwa nini ghafla Wapagani wameongozeka katika nchi ya waumini. Hii ndiyo ilikuwa sensa ya mwisho iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa dini. Inaaminika kuwa matokeo ya sensa hii yalifanyiwa mabadiliko kwa ajili ya sababu za kisiasa pale ilipobainika kuwa Waislam Tanzania walikuwa wengi kupita Wakristo. Upo ushahidi kuwa mwaka 1970, ilipobainika kuwa Waislam ni wengi Tanzania serikali iliiamrisha Idara ya Takwimu kuchoma moto matokeo yote ya sensa ya mwaka 1970. Si tabu kwa hivi leo kutambua ni nani walitoa amri hii na kwa sababu zipi. Bahati mbaya mgao wa madaraka katika siasa Tanzania umewatupa nje Waislam, ingawa inafahamika kuwa usalama na utulivu wa nchi yeyote unategemea mizani hii kuwa sawa. Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili limefanywa nyeti na la kutisha sana. Lakini wanaotishwa na hesabu na takwimu za sensa si Waislam bali ni Wakristo na makanisa yao. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria, uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. Tatizo hili lipo Tanzania. D.B. Barret anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo. Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%. Lakini takwimu za Africa South of the Sahara, zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%. Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982. Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe. Mgao wa madaraka na kugawana vyeo haikupashwa kuwa sababu ya migongano na mifarakano katika Afrika huru. Lakini kwa bahati mbaya sana hii imekuja kuwa sababu ya mifarakano katika serikali za wananchi wenyewe. Jambo hili limekuwa ni suala nyeti kwa sababu ukabila, udini na kujuana ni kitu muhimu katika serikali za Afrika. Mgawanyo wa madaraka na wingi wa wafuasi katika dini au kabila havikuwa vitu vilivyokuwa vikiwashughulisha wananchi wakati wa ukoloni kiasi cha kuleta mifarakano katika jamii. Kwa bahati nzuri ukabila hauna nguvu Tanzania lakini dini imekuwa chanzo cha ubaguzi toka zama za ukoloni, tofauti ni kuwa wakati wa ukoloni waliokuwa wakiwabagua Waislam hawakuwa Wakristo weusi bali Wazungu. Ukristo ni dini mpya Tanzania kwa kuwa uliingizwa katika karne ya kumi na nane na wamisionari. Kanisa na Mwafrika Mkristo ni matokeo ya ukoloni. Kwa ajili hii basi historia ya Kanisa katika Afrika ni ile ya kushirikiana na kuwa tiifu kwa serikali ya kikoloni. Chini ya ukoloni, taratibu Kanisa likaweza kujenga uhusiano maalum kati yake na serikali pamoja na Mkristo Mwafrika ambae imemuelimisha katika shule zake za misheni. Mwafrika Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala kuanzia Wajerumani hadi Waingereza. Mwafrika Mkristo akawa mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru akaja kushika madaraka ya serikali. Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani. Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa likajifanyia msingi imara wenye nguvu kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania. Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania. Waingereza walipokuja kuitawala Tanganyika (kama Tanzania inavyojulikana) baada ya kuondoka Wajerumni baada ya Vita Kuu ya Kwanza, Wajeruamani walikuwa wameshafanya kazi ya kutosha ya kuiweka Tanganyika ndani ya mamlaka mbalimbali za Kikristo. Tanganyika ilikuwa imegawanywa katika mamlaka za Kikristo kutoka nchi tofauti za Ulaya. Kanisa Katoliki ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian Fathers walikuwa Iringa. Wamisionari hawa walipotia mguu pwani ya Afrika ya Mashariki, nia yao hasa ilikuwa kuufuta Uislam. Wakazi wa pwani hii iliyokuwa ikijulikana kama Zanj waliuona Ukrsto kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1498 Wareno walipofika sehemu hizo. Mwaka 1567 wamishionari wa Augustinian waliingia Afrika ya Mashariki ili kupambana na Uislam ili Ukristo uwe dini ya dunia nzima. Kadinali Lavigirie alianzisha The White Fathers, taasisi ya Kanisa Katoliki kwa kusudi maalum la kuupiga vita UislamWakati huo huo Church Missionary Society (CMS) ilikuwa imejitwisha kazi ya kuondoa ulimwengu kutokana na Uislam, ujinga na giza. Hadi hii leo White Fathers wapo Tanzania wakiendelea kufanya kazi iliyowaleta Tanganyika zaidi ya miaka mia iliyopita. Wajerumani walipofika Tanganyika waliwakuta Waislam wanafahamu kuandika, kusoma na walikuwa wameelimika katika hesabu. Mmishionari Ludwig Krapf alipofika kwa Chifu Kimweri wa Usambaa mwaka 1848 alimkuta yeye na wanae wote wanajua kusoma. Herufi walizokuwa wakitumia zilikuwa za Kiarabu. Wajerumani kwa ajili hii basi waliwaajiri Waislam kama walimu, wakalimani na makarani serikalini. Wamisionari na wakoloni waliona wivu na nyoyo zao zikaingia hasad kwa maendeleo haya waliyoyakuta kwa Waislam. Kubwa zaidi ni kuwa walikuwa wamekuja kustaarabisha watu “washenzi” badala yake wamewakuta watu waliostaaarabika na wanye utamaduni wa kupendeza. Elimu hii yote na utamaduni huu wa hali ya juu ulikuwa unatokana na Uislam na shule zake zilizojulikana kama madras. Hapo ndipo zilipoaanza mbinu ya kuvunja maendeleo haya yote. Vita vilivyodumu hadi hii leo. Herufi za Kiarabu zikapigwa marufuku kutumika na badala yake watu wakalazimishwa kujifunza herufi za Kirumi. Muislam ambae jana alipoingia kulala alikuwa anaitwa ameelimika akaamka asubuhi yake mjinga, hana elimu, hajui kusoma wala kuandika. Njama hizi zote dhidi ya Uislam ilikuwa sehemu ya makubaliano kama ilivyoandikwa katika kifungu IV cha Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884. Kifungu hicho kilikuwa kinasema kuwa Ukristo ni lazima ulindwe dhidi ya Uislam. Kati ya mwaka 1888-1892 katika kutekeleza kifungu hicho kama ilivyokubalika katia Mkutano wa Berlin, Imperial British East Africa Company ilitumia nguvu za kisiasa na kijeshi kuulinda Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Ombwe lililoachwa na elimu ya Kiislam ikajazwa na elimu ya Kanisa chini ya usimamizi wa Waingereza. Kanisa hivi sasa linaeneza uongo na propaganda kuwa lenyewe ndilo lililoweka msingi wa kwanza wa elimu Tanganyika. Ukweli ni kuwa Wamisionari walifuata nyayo za madras na walimu wa kwanza katika shule za misheni walikuwa Waislam ambao hawakusoma katika shule za kanisa bali katika madras. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mia moja Kanisa likaelekeza nguvu zake katika katika kuwatayarisha raia ambao wengi wao walikuwa Wakristo, watakaokuwa watiifu kwa Kanisa na serikali. Ni katika mtandao huu ndiyo Wakristo wanaimiliki serikali na Chama Cha Mapinduzi na kuiamrisha ifanye linavyopenda Kanisa, wakati Waislam na Uislam ukifanywa kama vitu visivyokuwa na maana yoyote. Hadi kufikia mwaka wa 1960 Kanisa likawa taasisi kubwa inayomiliki mamilioni ya dola ya misaada inayopokelewa kutoka wahisani na wafadhili walioko katika ulimwengu wa Kikristo. Kanisa sasa hivi linahodhi mahospitali, misururu ya ndege binafsi, viwanja vya ndege, makampuni ya uchapaji na mitambo ya kupiga chapa, stesheni za radio, tv na magazeti. Kanisa limekuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kiasi kwamba wakati mwingine watendaji, hasa Wakristo katika serikali na ndani ya chama tawala CCM hawajui utii wao upo kwa nani, serikalini au katika Kanisa? Ni katika kuchanganyikiwa huku kwa watendaji wa serikali kuhusu uhusiano wao na Kanisa na serikali ndiko kulikoamsha kutoaminiana kati ya Waislam na serikali mara tu baada ya uhuru kupatikana. Serikali ikaonekana kama moja ya taasisi za Kanisa na Waislam wakiwa ni watazamaji tu. Mara baada ya uhuru Kanisa likaangalia nafasi yake na serikali mpya iliyokuwa madarakani. Wakati wa kudai uhuru Kanisa lilijiweka mbali na siasa na ikaonekana kuwa Kanisa lilikuwa likiheshima ule mpaka kati ya dini na siasa. Wakati ule mgongano kati ya Kanisa na serikali haukupata kusikika hata kidogo. Baada ya uhuru kupatikana tu na serikali ikawa mikononi mwa wananchi, Kanisa likaanza kusikika likisema kuwa lina haki na wajibu kuwa na ushawishi ndani ya serikali, kuikosoa serikali na kuingooza pale inapoona serikali haifanyi mambo sawa kwa matarajio yake. Katika msimamo huu mpya, Kanisa likajipa fursa ya kuwa msemaji wa watu. Huu ulikuwa ni mwelekeo mpya katika mambo ya siasa na utawala. Katika Uislam siasa na dini ni kitu kimoja. Vitu hivi viwili havitenganishwi. Lakini mwaka wa 1955 wakati wa siku za mwanzo kabisa za TANU, Waislam katika TANU walivyoweza kukiongoza chama katika misingi ya kisekula na utaifa ili kulinda umoja wa wananchi. Kutochanganya dini na siasa ikawa moja ya maadili makuu ya TANU. Kuanzia hapa ndipo sasa tunaweza kuelewa mapambano kati ya Waislam kwa upande mmoja na serikali na Wakristo kwa upande wa pili yalivyokuja kigubika Tanzania mara baada ya uhuru. (Inatoka katika kita bu “Maisha na Nyakati za Abduliwahid Sykes…”na Mohamed Said, Phoenix Publishers, Nairobi 2002)

Source: Trendinface

Popular Posts