KATIBU   wa Bunge Dk. Thomas Kashililah ametoa ufafanuzi kuwa mbunge wa Bahi,   Omar Badweli anayetuhumiwa kwa rushwa ataendele kuwa mbunge hata kama   atahukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita jela.
  Dk.   Kashililah alisema hayo jana alipozungumza kwa njia ya simu alisema kuwa mbunge huyo bado ni mtuhumiwa na pia kwa   mujibu wa katiba atakoma kuwa mbunge kama atahukumiwa kifungo cha   kuanzia miezi sita jela.
        Amesema hayo baada ya mbunge huyo Badwel kufunguliwa kesi mahakamani  ya  tuhuma ya kuomba rushwa ya sh. milioni nane toka halmashauri ya  wilaya  ya Mkuranga, Pwani.
         Dk. Kashililah alitoa mfano wa mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi   ambaye hivi karibuni mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kutishia kuua   kwa maneno kwa kukusudia na kumuhukumu kwenda jela miezi 10 au kulipa   faini ya Sh. 500,000.
       Hata hivyo Kilufi alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na mahakama ya Mbeya.
  Alisema   hata kama Badwel atafungwa kifungo cha chini ya miezi sita kwa mujibu   wa katiba ataendelea kuwa mbunge atakapokuwa amemaliza kifungo chake   hicho.
        "Kwa sasa Badwel ni mbunge halali kwani hayo aliyonayo ni tuhuma tu na   hatuwezi sisi kama Bunge kumuondoa mpaka ithibitishwe na vyombo  husika. Ubunge wake utakoma tu endapo atafungwa zaidi ya miezi sita na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
        Kila mtu ana haki mbele ya sheria anaweza akajitetea na akawa huru,   sasa kama umeshamfukuza utafanyaje ni lazima tusubiri," alifafanua Dk.   Kashililah.