Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Mhe Said Ali  Mbarouk, akizungumza na ujumbe wa Wafanyakazi wa TV Oman ulipofika  ofisini kwake kujitambulisha kwa ujio wao Zanzibar wa kutengeneza  Program ya Utalii wa Zanzibar na  Majumba ya Mji Mkongwe na sehemu za  Historia ya Zanzibar  kuitangaza Kitalii Oman, kushoto kwa Waziri Balozi  wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid na Wafanyakazi wa TV Oman.
   Balozi wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid, akizungumza na Waziri wa  Habari Utamaduni Utalii na Michezo walipofika Ofisini kwake kutambulisha  Ujumbe wa TV Oman uliofika Zanzibar kwa ajili ya kufanya program  mbalimbali za historia na kuitangaza Zanzibar Kitalii Nchini Oman.
   Balozi wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid, akizungumza na Waziri wa  Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe Said Ali Mbarouk,  alipofika  Wizarani kuwatambulisha Wafanyakazi wa Oman kufanya program mbalimbali  za kuitangaza Zanzibar Kitalii nchini Oman.
    Wafanyakazi wa TV Oman wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Habari Ofisini kwake walipofika kujutambulisha. 
   Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe.Bihindi Hamad,  Mkurugenzi Mipango na Uendeshaji Joseph Kilangi na Mtayarishaji wa  Vipindi wa ZBC TV Ahmeid Talibm wakisikiliza Waziri wakati wa mkutano  huo. uliofanyika katika Ofisi ya Wizara ya Habari Kikwajuni.  
  ---
   UONGOZI wa Shirika la Utangazaji nchini Oman, umeahidi kulisaidia  Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – TV) katika nyanja mbali mbali,  ikiwemo za kiufundi na kitaaluma, ili liweze kuharakisha juhudi zake za  kutoka kwenye mfumo wa Teknolojia ya habari wa Analogy na kuelekea ule  wa Digital.
   Ahadi hiyo imetolewa jana na Uongozi wa Shirika hilo, wakati ulipokutana  na kubadilishana mawazo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na  Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk, ofisini kwake Mnazi Mmoja.
   Ujumbe huo wenye timu ya waandaji wa filamu, upo nchini kwa ajili ya  kutayarisha filamu katika maeneo ya kihistoria, hususan Mji Mkongwe,  ambapo pamoja mambo na mengine filamu hiyo itaisaidia kuitangaza  Zanzibar kiutalii.
   Ujumbe huo ambao uliambatana na Balozi mdogo wa Oman nchini, Mansoor Al  Busaid, umeahidi kukutana na Menejment ya ZBC, ili kubadilishana uzoefu  pamoja na kuangalia maeneo yepi ambapo Shirika hilo linaweza kusaidia  kiufundi na kitaaluma.
   Mmoja wa viongozi wa Shirika hilo, Ebrahim Al Yahmad alisema ZBC inaweza  kunufaika sana kuwepo mashirikiano na Shirika hilo na kuharakisha  safari yake ya kuelekea Digital,kwa kuzingatia kuwa tayari Oman  inaondoka katika mfumo huo (Digital ) na kuelekea mfumo wa DH.
   Alisema Shirika la Utangazaji la Oman, (ambalo lina Waziri wake)  limepiga hatua kubwa sana katika nyanja ya mawasiliano ya habari, hivi  sasa likiwa tayari limejenga Studio kubwa ya kisasa, huku likiendelea na  maandalizi ya program za mafunzo kwa mfumo wa DH.
   Alisema katika dhana ya kuendeleza mashirikiano kati ya mashirika hayo  mawili, vijana wa Zanzibar wataweza kupata fursa ya kubadilishana uzoefu  na wenzao wa Oman na kuona vipi wanafanya kazi. 
   Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema hatua ya kuja kwao nchini  na kuandaa filamu katika maeneo ya kihistora kutaisaidia sana kuutangaza  Utalii wa Zanzibar, kwa kujua kuwa Zanzibar ni eneo bora kwa biashara  ya Utalii.
   Aidha alimwomba Waziri Mbarouk kusaidia upatikanaji wa nakala za  magazeti ya zamani ambayo yaliwahi kuchapishwa hapa nchini, au kumpata  mtu ambae anaweza kueleza kwa ufasaha juu ya uwepo wa magazeti hayo.
   Mapema Waziri Mbarouk alisema Serrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko  tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na ndugu zao wa  Oman.
   Alisema hatua ya Oman TV kuja nchini kwa ajili ya kuandaa filamu maalum  katika maeneo ya kihistoria, ni hatua muafaka inayounga mkono juhudi za  Serikali katika kuutangaza utalii wa Zanzibar hadi nje ya mipaka na  kufanikisha ‘dhana ya utalii kwa wote’. 
   Alisema mbali na ujumbe huo kuangalia eneo la Mji Mkongwe, pia wapaswa  kuangalia maeneo zaidi ya kihistoria, ikiwemo msitu wa Jozani, magofu ya  Mtoni, fukwe zenye kupendeza pamoja na magofu ya Mazrui yalioko Chwaka  kijiji cha Tumbe, kisiwani Pemba.
   Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii, na kutoa  mfano wa Hifadhi yam situ wa Jozani, wenye kupatikana Kima Punju,  wanyama ambao hawezi kupatikana mahala popote pale Duniani, isipokuwa  Zanzibar.
   Aidha aliyasifia magofu yalioko Chwaka Tumbe, kwa kusema kuwa ni eneo  kubwa, linalovutia na lenye historia inayosisimua, likielezwa kuwa ni  mji uliopata kuishi watu kutoka Oman kabla ya kuja kwa Wareno.
   Akizungumzia kuwepo kwa magazeti ya zamani, Mbarouk alisema kuna idadi  kubwa ya magazeti yaliokuwa yakichapishwa hapa Zanzibar miaka mingi  iliopita, na kuuahidi ujumbe huo kupata baadhi ya nakala zake pamoja na  watu wanaoelewa historia ya kuwepo kwa magazeti hayo. 
   Na 
  Abdi Shamnah - 
  Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na  Michezo Zanzibar