Pages

Wednesday, October 17, 2012

Maelezo Ya Jeshi La Polisi Kuhusiana Na Hatua Ya Kumkamata Sheikh Ponda


KATIBU WA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU (T) SHEIKH PONDA ISSA PONDA AKAMATWA NA POLISI

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemtia mbaroni Katibu wa Jumuiya tajwa hapo juu maarufu kama PONDA ISSA PONDA kwa makosa mbali mbali ya kuchochea vurugu na uvunjaji wa amani jijini Dar es Salaam.
Aidha hivi karibuni Sheikh Ponda Issa Ponda aliongoza kundi la wafuasi wake na kuvamia kiwanja No. 311/3/4 BLOCK “T” eneo la Chang’ombe katika Manispaa ya Temeke mali ya Kampuni ya AGRITANZA ambayo ipo chini ya Kurugenzi ya Kampuni hiyo. Mnamo tarehe 12/10/2012 Ponda Issa Ponda aliwaongoza wafuasi wake walioteka eneo hilo wakidai kwamba wanakomboa.
Mali za Waislamu, zilizouzwa na BAKWATA, uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba kiwanja hicho kina hati miliki No. 93773 uliotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na mikataba mbali mbali ya kuuziana au kubadilishana kati ya BAKWATA na Kampuni tajwa hapo juu. Pia uongozi wa BAKWATA umeleta mashahidi kuthibitisha uhalali wa kiwanja hicho kumilikiwa na Kampuni tajwa. Hivyo watu wote waliovamia eneo hilo wakiongozwa na Sheikh Ponda wanakabiliwa na shtaka la kuingia kwa jinai pamoja na uharibifu wa mali katika eneo hilo. Sambamba na kukamatwa kwa Sheikh Ponda tarehe 16/10/2012 saa 4.00 usiku karibu na eneo la maficho yake ambapo aliletwa na pikipiki.
WATU 38 WAMEKAMATWA KWA KOSA LA  JINAI NA UHARIBIFU
Wakati huo huo sambamba na kukamatwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda Polisi walifanya operesheni maalumu ya kuwaondoa wavamizi katika kiwanja tajwa hapo juu kinachomilikiwa na Kampuni AGRITANZA. Watu wapatao 38 walikutwa katika eneo la kiwanja hicho ambacho kati ya hao (7) ni wanawake na 31 ni wanaume.
Operesheni hiyo ilifanyika tarehe 17/10/2012 usiku wa manane kuanzia saa tisa hadi saa kumi na nusu usiku kwa muda wa dakika 90. Katika eneo hilo vilikutwa vielelzo mbali mbali vikiwemo visu na mapanga na pia nyenzo mbali mbali za ujenzi, pamoja na vifaa vya ujenzi, vielelezo hivyo vimehifadhiwa katika kituo cha Polisi tayari kwa ajili ya ushahidi mahakamani.
SHEIKH PONDA KUSABABISHA VURUGU NA VITISHO
Katika siku za hivi karibuni Sheikh Ponda Issa Ponda amekuwa akiwaongoza wafuasi wake chini ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kwa kufanya maandamano kinyume cha Taratibu na kuhamasisha umwagaji damu jijini Dar es Salaam na nchini Tanzania kwa ujumla.
Kwa ujumla Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania inayoongozwa na Sheikh Ponda haijasajiliwa kisheria lakini wanatihumiwa kwa uchochezi wa hali ya juu ambapo licha ya kufanya maadamano kinyume na sheria pia siku ya tarehe 12/10/2012 walisababisha kuvunja kwa makanisa zaidi ya manane, uharibifu wa magari na wizi au upotevu wa vifaa katika makanisa, yote hayo yameongozwa na Sheikh Ponda na madhara yake ni makubwa.
Sheikh Ponda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola pamoja na kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai watuhumuwa waliokamatwa kwa uvunjaji wa makanisa na kufikishwa mahakamani waachiwe mara moja kabla siku saba na kadhalika. Uchunguzi wa watuhumiwa wote 39 unaendelea na kufikishwa mahakamani mara baada ya kupitishwa na wakili wa Serikali kuthibitisha mashitaka.
S.H. KOVA – DCP
KAMANDA WA POLISI
KANDA MAALUMU YA POLISI
DAR ES SALAAM
————————
Nukuu za matamshi ya Kamanda Kova alipokuwa akitoa taarifa:
  • “Sheikh ponda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola na kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai watuhumiwa waliokamatwa kwa uvunjaji wa makanisa na kufikishwa Mahakamani waachiwe mara moja kabla ya siku saba”
  • “Ponda alikamatwa juzi majira ya saa 4:30 usiku akiwa kwenye pikipiki kuelekea katika maficho yake maeneo ya Temeke”
  • “Juzi usiku sijalala kabisa kuhakikisha oparesheni ya kumkamata inakwenda salama, Ponda ni mjanja sana ila Serikali ina mkono mrefu kabla ajaingia katika maficho yake Temeke, alijaribu kukimbia ili atoroke lakini akakamatwa”
  • “Ponda akiwa na wafuasi wake walivamia kiwanja hicho cha agritanza na kudai kuwa wanakomboa mali za waislamu zilizouzwa na BAKWATA”
  • “kati ya watu 38 tuliowakamta wanawake ni saba na wanaume ni 31 na tuliwakuta na silaha mbalimbali kama visu, mapanga, sururu na vifaa vya kuvunjia na vya ujenzi, jenereta na kujenga jengo la haraka”
  • “Jeshi la Polisi limemvumilia Ponda kwa muda mrefu… watu wanaoandamana kinyume cha taratibu waache.”
  • “Nawasifu sana Wakristo ni wavumilivu, wana busara kwa tukio la Mbagala la kuchoma Makanisa la sivyo hali ingekuwa ya hatari na hata hivyo Jumuiya ya Taasisi za Kiislam haijasajiliwa kisheria”
  • “Wafuasi wengine wajisalimishe kwani opareheni inaendelea na watawachukulia hatua za kisheria”
  • “Nawaasa Wananchi kutumia akili zao binafsi na kuacha kufuata mkumbo kwa kuwa watashughulikiwa.”

Popular Posts