Pages

Friday, October 19, 2012

WAZANZIBARI WAISHIO UINGEREZA WASIKILISHWA NA VURUGU


Jumuiya ya Wazanzibari waishio UK ZAWA UK inasikitishwa na matukio ambayo yanaendelea kutokea huko nyumbani Zanzibar yaliyoanza kujitokeza jana tarehe 17/10/2012 ambayo yamesababisha vurugu kubwa katika Miji ya Zanzibar na vitongoji vyake.
Matukio hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa maisha ya askari wa jeshi la polisi,mali za Umma, wananchi mmoja mmoja na hata vyama vya siasa. Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuvunjwa Maduka, vyombo vya usafiri, kukatwa miti ovyo na nguzo za umeme, pamoja na kuchomwa moto maskani za CCM
Kutokana na vitendo hivyo, ZAWA UK kinaalaani vikali matukio hayo ambayo yamepelekea uvunjifu wa mkubwa wa amani ya nchi, na kusababisha hofu kubwa kwa raia pamoja na wageni wanaotembelea Zanzibar.
Pamoja na vurugu hizo, ZAWA UK kimepokea kwa mshangao mkubwa taarifa ya Serikali ya Zanzibar pamoja na ile ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia jeshi la Polisi iliyoeleza juu ya kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed katika mazingira ya kutatanisha.
Katika Taarifa hiyo, Serikali zimethibitisha kuwa vyombo vyake vyote vya ulinzi havijamkamata Sheikh Farid, jambo ambalo limezidisha hofu na wasi wasi kwa wananchi juu ya mahali alipo na hali yake kiongozi huyo wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar.
ZAWA UK kinaziomba Serikali zote mbili kuendeleza juhudi zote za kuhakikisha taarifa za ukweli na za uhakika zinapatikana juu ya kadhia ya kutoweka kwa Sheikh huyo kwani Sheikh Farid ni raia wa nchi hii, na Serikali hii ni kwa ajili ya wananchi wote, ili kuondoa hofu na wasi wasi ambao umesababisha baadhi ya wananchi kujengwa na dhana mbaya.
Vile vile ZAWA UK kinawaomba wananchi wote kwa ujumla kutojiingiza na kutofanya vitendo vyovyote vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani ya nchi yetu.
Sote kwa pamoja tukatae kabisa kujihusisha na vitendo vya kuleta vurugu kwa vitendo na kauli zitakazopelekea kuiondolea sifa njema nchi hii ya Zanzibar.
Mwenyekiti ZAWA UK
Hassan Mussa Khamis

Popular Posts