Pages

Wednesday, October 17, 2012

SMZ YAWATAKA WANANCHI KUENDELEA NA SHUGULI ZAO


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli  zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali  ya ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu  wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado  ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.

Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri  Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi  wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani,  Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani  na kudhani amekamatwa na vyombo vya Dola na kuwekwa ndani.


Waziri Mohamed Abud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya  Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa,  Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo, Zimamoto na Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza kutoelewa  chochote kuhusu Sheikh Farid.
  Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya  kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea  kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake  na kuchukua hatua zinazofaa.
Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake,  wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi  au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache  kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa  kwa mujibu wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo.
 
Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa  Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto  Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu  miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.

IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
17/10/2012
ZANZIBAR,TANZANIA

Popular Posts