Tanzania imeitaka Malawi kusitisha  shughuli za utafiti katika eneo la ziwa Nyasa lenye mgogoro  na  kusisitiza nia yake ya kuendelea kuzungumza na nchi hiyo kuhusu mgogoro  wa mpaka licha ya nchi hiyo kuendelea na msimamo wake wa kumiliki eneo  lote la ziwa hilo.
  Hayo yamebainishwa katika  mkutano  wa wataalam na viongozi kutoka serikali ya Malawi na Tanzania kushindwa  kufikia muafaka uliokusudiwa kuhusu eneo halali la mpaka unaotenganisha  nchi hizo.
  Akizungumza wakati wa kuhitimisha  kikao cha usuluhishi kilichohusisha  timu za wataalam na viongozi wa  wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika  jana usiku mjini Lilongwe  Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Bernard  Membe amesema Tanzania bado inaamini katika mazungumzo ili kufikia  muafaka wa kudumu wa mgogoro huo.
  Amesema kuwa pamoja na sababu  mbalimbali zilizotolewa na upande wa serikali ya Malawi juu ya umiliki  wa eneo lote la ziwa Nyasa ,msimamo wa Tanzania juu ya mpaka  unaozitenganisha nchi hizo uko wazi  kwa kwa kuzingatia vielelezo vya  historia vilivyoachwa na wakoloni na sheria za kimataifa kuhusu mpaka  kuwa katikati ya ziwa hilo. 
Ameeleza kuwa licha ya serikali ya Malawi kuonyesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika jana usiku wameamua kuunda timu za wataalam
 Ameeleza kuwa licha ya serikali ya Malawi kuonyesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika jana usiku wameamua kuunda timu za wataalam
 “Licha ya kuwasilisha vielelezo  kuonyesha uhalali wa mpaka hatukuweza kufikia muafaka tumefika mahali pa  kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu zitoe mapendekezo ya nini  kifanyike maana kuna kila dalili kwamba sisi wenyewe tutashindwa  kuendelea zaidi “
  Amesema kuwa wataalam kutoka  Malawi na Tanzana watakutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam ili  waweze kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwapata wasuluhishi wa  mgogoro huo pamoja na kutoa mapendekezo ya faida na hasara ya njia  watakazozipendekeza.
  “ Sasa tumefika mahala pa kuhitaji  msaada,tutazituma timu zetu zikae pamoja na kutoa mapendekezo ya nini  kifanyike maana inaonyesha wazi kabisa sisi wenyewe hatutaweza kuendelea  tena sasa timu zitatoa mapendekezo juu ya kesi hii tuwaite wazee wenye  busara barani Afrika tunaowaamini watuamulie” amesema.
  Amefafanua kuwa timu za wataalamu  zitakazoundwa zinatarajia kukutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam  ili kutoa mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa marais wa nchi hizo katika  kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa mgogoro huo ikiwemo kumtafuta  msuluhishi au kwenda kwenye mahakama ya Kimataifa.
    Aidha , Tanzania imeitaka Malawi   kusitisha shughuli za utafiti katika eneo la Tanzania katika ziwa Nyasa  lililo na mgogoro na kukisisitiza kuwa mchakato wote wa kutafuta suluhu  utaendeshwa kwa amani na utulivu huku akiwaomba watanzania kuendelea   kuiombea nchi amani ili suala hilo limalizike kwa amani ,utulivu na  undugu.
  Kwa upande wake waziri wa Mambo ya  Nje na Mahusiano ya kimataifa wa Malawi Bw. Ephraimu Chiume katika  maelezo yake wakati wa kuhitimisha mkutano huo amesisitiza kuwa licha ya  mgogoro huo kuhitaji busara zaidi bado serikali yake inaamini kuwa  mpaka kati yake na Tanzania uko upande wa mashariki mwa ziwa Nyasa na  unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
  Amesema kutokana na unyeti wa  suala lenyewe na eneo hilo pamoja na historia ya nchi yake anapenda  kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili wananchi wa nchi mbili waweze  kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
  “Ni matumaini yangu mkutano wa Dar  es salaam utaofanyika mwezi  Septemba utazaa matunda ili suala hili  lipatiwe ufumbuzi na ikiwezekana tupate msaada wa sheria za kimataifa  kwa sababu suala hili liko kisheria zaidi” alisisitiza Bw. Chiume.
   Ujumbe wa wataalam kutoka Tanzania  uliokuwa ukitafuta suluhu ya mgogoro huo uliwahusisha makatibu wakuu  Patrick Lutabanzibwa (Ardhi),John Haule(Mambo ya nje) na mawaziri wa  wizara ya Ardhi Prof. Anna Tibaijuka  na Bernard Membe wa Mambo ya Nje  na ushirikiano wa Kimataifa, balozi wa Tanzania nchini Malawi Patrick  Tsere pamoja na wataalam wanaotoka eneo la ziwa Nyasa akiwemo  Prof.Hemphrey Kamisama ambao nao walitoa maelezo kueleza hisia za  wananchi wa eneo hilo na uhalisia wa ziwa hilo.
  Na. 
  Aron Msigwa – MAELEZO.  
  Lilongwe, MALAWI.