Pages

Saturday, September 1, 2012

TGNP YALAANI KAULI ZA DC WA KOROGWE

DC Korogwe awajibishwe kwa udhalilishaji

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), tumesikitishwa sana na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga Ndugu Mrisho Gambo, kwa mwanasheria wa Halmashauri hiyo Bi. Najum Tekka, kuhusu uhalali wa shahada aliyonayo hususan kuihusisha shahada hiyo na vitendo vya ngono! Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari ikiwepo gazeti la Majira Augosti 29,2012 Uk.3

Kauli hii ni udhalilishaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za wanawake na inaenda kinyume na misingi ya kuzingatia usawa sanjari na Katiba ya nchi ; Uwezeshaji wa wanawake na utekelezaji wa Maazimio ya Haki na Usawa katika ngazi za Kimataifa Kikanda na Nchini Tanzania.

Aidha kauli hii, inalenga kupotosha na kukatisha tamaa juhudi kubwa wanazofanya wanawake na wasichana katika kupata elimu na mafanikio mbalimbali nchini Tanzania. Zaidi ya hapo, kauli hii inadhalilisha na kushusha hadhi ya vyuo vya elimu ya juu vinavyofanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa Watanzania.

Kutokana na kauli hiyo DC amekiuka maadili ya uongozi wa umma na kukidhalilisha kiti cha ukuu wa wilaya na kiongozi Mkuu wa nchi aliyemteua kushika wadhifa huo. Aidha kauli ya kiongozi huyo ya kutimia mahakama kutetea hoja yake , kunaashiria ubabe , ujeuri, vitisho, kiburi na dharau ya kutaka kuingilia uhuru wa mahakama na ajenda binafsi isiyokuwa na maslahi kwa wanawake na umma wa Watanzania

Kutokana na kauli hiyo ya udhalilishwaji ,sisi wanaharakati wa ukombozi wa wanawake Kimapinduzi, usawa wa kijinsia, haki za kibinadamu demokrasia tunalaani vikali kauli za DC na kutoa Rai ifuatayo:

1. Mkuu wa Wilaya Ndugu Mrisho: amwombe radhi Mwanasheria Bi. Najum Tekka, kwa kosa la kumdhalilisha kijinsia

2. Tume ya maadili ya utumishi wa umma, na Mamlaka nyingine za kinidhamu zimchukulie hatua za kinidhamu Ndugu Gambo kwa kutumia lugha ya kudhalilisha watumishi kinyume na maadili.

3. Wanawake wote, wanaume, vijana wa kike na kiume kuendelea na mapambano dhidi ya mfumo dume na mifumo yote kandamizi, kushikamana katika kudai misingi ya kisheria, uwajibikaji inayozingatia usawa na haki na kukataa kudhalilishwa katika ngazi binasfi na za umma !.

Imetolewa
Dar es salaam leo 31/08/2012 na:
Usu Mallya
Mkrugenzi Mtendaji TGNP

Popular Posts