Pages

Tuesday, May 29, 2012

TAMKO LA TAG KUHUSU MATUKIO YANAYOASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI

Monday, May 28, 2012
TAMKO LA ASKOFU MKUU WA TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD, DK.BARNABAS MTOKAMBALI, KUHUSU MATUKIO YANAYOASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI.

Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani, umoja na utengamano wa taifa letu la Tanzania, haya ndiyo yanayonisukuma kutoa tamko hili leo ili kuonya na kushauri.

Katika siku za karibu kiumeibuka makundi mbalimbali ya kidini ambayo yalianza kutoa matamko yenye kuchochea ghasia za kidini Tanzania, na pengine kauli hizo ndizo zinazotimizwa kwa vitendo hivi sasa.

Miongoni mwa matukio hayo ni:
Januari sita mwaka huu, kikundi kimoja kinachoitwa JUAKATA, kiliitisha kongamano la kujadili katiba mpya Tanzania, kwa upande wa Waislam. Katika kongamano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kauli zifuatazo:
1. Lazima Rais ajaye atoke Zanzibar
2. Kukabiliana na ukuaji wa kasi wa dini ya Kikristo
3. Kupinga Muungano ili kuupa nguvu Uislamu
4. Kupigana kufa na kupona kutetea maslahi yao wakati huu wa kuandaa katiba mpya.

Kauli hizo zilitolewa na Sheikh Nasor Mohameed, kutoka Zanzibar, ambaye alikuwa mgeni rasmi. Baadaye zikaandaliwa kanda za CD zilizosambaza ujumbe huo.

Uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa makanisa yaliyochomwa hivi karibuni huko Zanzibar ni ya EAGT, Elimu Pentecost na TAG, Anglikana, Katoliki na FPCT, hivyo kujenga taswira ya ubaguzi wa kidini ambao kama hautapatiwa dawa unaweza kuligawa taifa la Tanzania kama ilivyotokea Nigeria na kwingineko barani Afrika.

Hofu yangu ni kuwa, roho hii ya ubaguzi wa kidini ambayo Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliifananisha na dhambi ya kula nyama ya mtu, imekuwa ikiyatafuna mataifa ya Afrika kama ifuatavyo:

1. Mwaka 2000, vuguvugu la kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu (Sharia), lilianza kwenye majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria, miaka michache baadaye majimbo kadhaa yakajitangazia sheria hizo na tangu wakati huo kumekuwa na mapambano yasiyoisha. Takwimu zinaonesha kuwa katika miaka ya karibuni zaidi ya Wakristo 500 wameuawa kikatili na makanisa kuchomwa moto.

2. Roho hii imekuwa ikienea kwa kasi katika maeneo mbali mbali ya Afrika ambapo imelikumba taifa la Mali, majimbo ya kaskazini tayari yametangaza kujitenga na kuna vuguvugu lenye kuhusisha mapigano ya silaha.

3. Itakumbukwa kuwa wiki chache tu zilizopita vuguvugu hili la kudai utawala wa kidini liliibuka nchini Kenya ambapo watu wanaojiita wanaharakati walianzisha madai ya kutaka eneo la Pwani kujitenga na Jamhuri ya Kenya na kujitangazia taifa la Kiislamu.

4. Ni wakati huu ambao kundi la Uamsho linalopinga kuandikwa kwa katiba mpya kabla ya kuitishwa kwa kura ya maoni ili wanzazibar waamue kuhusu Muungano liliibuka na kuanzisha ghasia Zanzibar ambazo zimepelekea makanisa kadhaa kuchomwa moto na mali kuharibiwa, huku watu wa bara wakitishiwa maisha.

USHAURI WANGU KWA SERIKALI NA VIONGOZI WA DINI

Ni wajibu wa kila Mtanzania kutii sheria na mamlaka kwa kuwa zimewekwa/kuruhusiwa na Mungu, hivyo kuziasi ni Kumuasi Mungu, yaani ni dhambi. Hivyo kila Mtanzania anastahili kukumbuka wajibu wake wa kutii mamlaka.

Viongozi wenzangu wa dini wakumbuke kuwa wana wajibu mkubwa katika jamii, na jamii inawasikiliza hivyo ni vyema wakawa makini katika matamshi na maelekezo yao ili wasiwe chanzo cha kuchochea vurugu za kidini na uvunjaji wa amani.

Ni vyema wakati huu wa kuandikwa kwa katiba mpya, kila kikundi kikafuata utaratibu uliowekwa badala ya kuchochea ghasia ambazo madhara yake yatawakumba watanzania wote ikiwa ni pamoja na wao wenyewe watoto na wajukuu zao.

Pia ningependa kuwashauri viongozi wa serikali kusimama imara katika kusimamia sheria na haki, na kuepuka kauli au vitendo vitakavyofanya baadhi ya watanzania kudhani kuwa hawatendewi haki.

Ni vema ieleweke kuwa matukio kama haya ya uvunjaji wa amani yasipodhibitiwa na kukomeshwa haraka yanaweza kuumba chuki ambayo inaweza kuibua mlipuko mkubwa na machungu kwa wananchi na matokeo yake yakawa mabaya kwa Taifa zima. Hekima na busara inatufundisha kuwa tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

Ni vyema wenye dhamana ya kuongoza wakakumbuka kuwa wanawajibu mbele ya Mungu aliyewaweka au kuwaruhusu kuingia madarakani na siku moja watatoa hesabu mbele zake.

Mwisho, natoa wito kwa watanzania wenzangu tuulinde umoja, amani na utengamano wa taifa letu, tuikimbie dhambi ya ubaguzi kwa kuwa tukiiruhusu itatuangamiza sote. Tuliombee taifa letu na kukiwa na mbegu ya chuki tuimalize kwa njia ya majadiliano na vikao vya pamoja vinavyohusisha viongozi wa dini zote na serikali pia.

Imetolewa leo 28/05/2012
Na Dk. Barnabas Mtokambali
Askofu Mkuu wa TAG

Popular Posts