Rais   wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete   ameteua Wakurugenzi wapya tisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano   wa Kimataifa ambao pia watakuwa na hadhi ya Balozi.
Kwa   mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Dar es Salaam leo, Jumatano, Mei   30, 2012 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, uteuzi huo   umeanza Mei 2, mwaka huu, 2012.
Walioteuliwa   ni Ndugu Vincent Kibwana ambaye anakuwa Mkurugenzi, Idara ya Afrika;   Ndugu Naimi Aziz ambaye anakuwa Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa   Kikanda; Ndugu Celestine Mushy ambaye anakuwa Mkurugenzi, Idara ya   Ushirikiano wa Kimataifa; Ndugu Yahya Simba ambaye anakuwa Mkurugenzi,   Idara ya Mashariki ya Kati, na Ndugu Bertha Somi ambaye ameteuliwa kuwa   Mkurugenzi, Idara ya Diaspora.
Wengine   ni Ndugu Irene Kasyanju aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi, Kitengo cha   Sheria; Ndugu Dorah Msechu ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi, Idara ya   Ulaya na Amerika, Ndugu Mbelwa Kairuki ambaye anakuwa Mkurugenzi, Idara   ya Asia na Australia, na Ndugu Silima Haji ambaye ameteuliwa kuwa   Mkurugenzi, Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar.
Kabla   ya uteuzi wake,  Ndugu Kibwana  alikuwa Afisa Mambo ya Nje Mkuu, Ndugu   Naimi Aziz alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ndugu Mushy alikuwa Kaimu  Katibu  wa Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ndugu Simba alikuwa Afisa  Mambo  ya Nje Mkuu, na Ndugu Somi alikuwa Afisa Mambo ya Nje Mkuu.
Naye   Ndugu Kasyanju alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ndugu Msechu alikuwa   Mkurugenzi Msaidizi, Ndugu Kairuki alikuwa Msaidizi wa Rais (Hotuba),   Ofisi ya Rais, Ikulu na Ndugu Haji alikuwa Afisa Mambo ya Nje Mkuu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
DAR ES SALAAM.
30 Mei, 2012