Tumejaribu  kutafakari   kwa kina juu ya  nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na  kushiriki  mazishi ya  muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru  aliyetelekezwa  na Taifa  lake, Dr. Vedasto Kyaruzi  na bado ki-ukweli  hatujapata  majibu. 
Tunapata   shida kujua dhima ya safari  ya Nape kwa kuwa shughuli mahsusi   alizozifanya akiwa Kagera zina  kinzana kimaadili na kitamaduni na   maombolezo ya misiba ya Kiafrika na  hasa misiba ya Kihaya. Mjumbe   aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka  pole kwenye msiba hategemewi   atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya  siasa, tena katika mazingira   ya ugenini lakini kwenye maeneo yale yale  msiba unapoendelea. Kwa  mpita  njia ambaye amefahamishwa tukio na  akahiari kufika msibani,  akiendelea  na shughuli zake haitakuwa  ajabu  na hakuna mtu mwenye  akili timamu  atamshangaa hata kidogo. 
Nape   aliingia Bukoba tarehe  25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika   Kashai-Matopeni msibani  kutoa salamu za pole.  Lakini baada ya hapo   alielekea Missenyi ambako  tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.   Watanzania mtakumbuka vema  kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa   kauli ya kutokuwa tayari  kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili  Watanzania  muweze kupima vema  uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe  kuwa Missenyi  ndiko iliko Kyaka  na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi  yamefanyika.  Tunashindwa kuelewa, hiyo  mikutano ilikuwa safisha njia  ya mazishi au  inahusiana vipi na mtu  aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?  
Linalochanganya   zaidi ni hili la  Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo  Dr.  Kyaruzi  alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa  Nape  akiwa  Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kufungua matawi na  kutangaza   operation yake mpya ya kisiasa iitwayo “Vua Gamba, vua  Gwanda, Vaa   Uzalendo”. Katika hili, ukiachilia ukinzani wa matukio  kimaadili na   kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi Nape  alikwenda Kyaka kuzika   au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu  kijana anahubiri  uzalendo  upi? Uzalendo usiokuwa na utamaduni,  Uzalendo wa kuwatelekeza  na  kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru  wa nchi hii? Kama huo  ndiyo  uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji  operation wala kampeni  maana  tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri  hii, ujio na matukio ya  Nape  kwenye maeneo ya msiba huu vinanapata  maana halisi. 
Katika   Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa  Arumeru Mashariki,  Chama Tawala   kimearifiwa kuwa moja ya kosa  lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye   mila hazikuwa zinampa fursa na  tafsiri njema kufanya shughuli kama ya   siasa  katika muda mfupi baada  ya msiba wa Baba yake. Ikiwa kosa hili  la  Kitamaduni limechangia Chama  kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe  tayari  kwa makosa ya Nape kupoteza  zaidi ya Kijiji cha Burifani na  Kata nzima  ya Kyaka. Na hatutoshangaa  iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma  ikishindwa  kuomba radhi! 
Mbali   na vioja vya Nape hapo juu, kwa  wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila   mmoja atakubaliana nasi kuwa  Taasisi yoyote (iwe dola au chama)   kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape  ni dharau ya hali ya juu na   ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii  iliyostaharabika tu, bali hata kwa   watu walipendao Taifa lao na kuuenzi  Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini   kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais  alikosa muwakilishi makini wa  hadhi  inayobeba uzito sawia na mchango wa  Dr. Kyaruzi katika Taifa  hili.  Tukio hili linaleta hisia za ubaguzi wa  Taasisi za dola na chama  katika  kutoa uzito kwenye majanga, matatizo  na misiba ya watu wa  Taifa hili. Ni  majuzi tu Taifa lilipotelewa na  Mcheza Sinema nguli  ambaye hapo awali  hakuwahi kupata heshima yoyote ya  Kitaifa. Lakini  tuliona jinsi viongozi  wa Serikali na Chama  walivyohamia msibani na  Serikali kujipa jukumu la  kuubeba msiba na  shughuli za mazishi.  Haikupita muda, Rais akiwa ziarani  Marekani, Rais  wa Malawi alifariki  duniani. Pamoja na uchovu wa safari  tulimwona Rais  akiingia nchini na  kutoka kuwahi mazishi ya Rais wa nchi  jirani.  Kulingana uzito na  umuhimu uliowekwa na Rais katika msiba huu,   hakusubiri hata atatue  matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali   yake kiasi cha  kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa   za Rais  anazoandika katika mitandao ya kijamii (MyKj) kila anapoelekea   kwenye  misiba ya watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali  Jijini  Dar  es Salaam.  Hili linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini  kuwa   misiba ya watu wa maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za  Rais  hata  kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili. Haya    yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa   MKUU  wa Majeshi Mstaafu Jenerali  Ernest Mwita Kyaro. Marehemu Mwita    alifariki siku chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa    sura ya Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj)   na  wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja  kutoa   salamu. Tabia hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili  inaonekana  kumea  kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar  es Salaam   unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es  Salaam. 
Kwa   Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye,  Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli   alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote  katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi   aiombe radhi jamii yetu kwa dharau  kubwa aliyoonyesha katika msiba huu.   Na kama alikuwa mpita njia tu,  basi atujuze ili Jamii na historia ya   Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi  kama muasisi wa TAA na mzalendo   aliyepigania uhuru wa Taifa lake  ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake   na hata mazishi yake  hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa. 
Na   mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya  Muungano Tanzania, yeye kama   Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa  Dar es Salaam na Mikoani. 
Asiye na Utamaduni ni Mtumwa. Tanzania ni Moja
Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha 
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam
                      -