Pages

Saturday, June 2, 2012

TAARIFA YA RAIS WA SMZ KUHUSU HALI YA ZANZIBAR

TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,
KWA WAANDISHI WA HABARI, WAHARIRI NA WANANCHI KUHUSU HALI YA NCHI, TAREHE 31 MEI, 2012

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Assalam Aleykum

Namshukuru Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote, kwa kutupa afya njema tukaweza kuzungumzia mambo yenye mustakbal mwema wa hali ya nchi yetu kwa jumla.

Napenda kutanguliza shukurani zangu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza na kudumisha amani hasa tokea kupatikana kwa maridhiano ya kisiasa baina ya vyama viwili vikuu vya siasa hapa Zanzibar, Chama cha Mapinduzi na Chama cha CUF, yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa mnamo Novemba, 2010 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Maridhiano hayo yalidhihirisha silka, ustaarabu na utamaduni wa Wazanzibari kuishi pamoja kwa kuheshimiana , kusikilizana na kushirikiana katika mambo yao ya kiuchumi na ya kijamii na maendeleo yetu.

Kama tunavyoelewa kwamba Zanzibar ina watu wa makabila na dini tofauti. Wazee wetu wa asili walisema “Zanzibar ni njema atakaye na aje”. Ustaarabu huu ulianza kutumika tangu ulipoanza kuingia Uislamu na kuendelea hadi kufika wageni kutoka Uajemi (washirazi), Ureno na Oman walioanzisha utawala wao katika karne mbali mbali hadi ya 18. Uislamu uliingia Zanzibar mara tu baada ya kuwepo katika nchi ya Saudi Arabia. Kadhalika, Ukristo uliingia Afrika Mashariki alipofika Mvumbuzi wa Kireno, Vasco da Gama mwaka 1498 na hatimae kuja Wamishionari wa kwanza wakiongozwa na Ludwig Krapf mwaka 1844. Mfalme wa wakati huo wa Zanzibar aliwaruhusu kujenga Kanisa la Anglikana la Church Missionary Society (CMS) liliopo Mkunazini. Krapf baadae aliruhusiwa kujenga mishionary Mombasa. Madhehebu mengine ya kikristo yaliingia Zanzibar katikati ya karne ya Kumi na Tisa na kuenea sehemu za bara kutokea hapa Zanzibar, na kanisa la pili kubwa la Minara Miwili lilijengwa katika eneo la Shangani Mjini Zanzibar.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Naelezea haya ili nikumbushe sifa ya Zanzibar kuwa ni pahala ambapo watu wa dini mbali mbali walifika na kuweka makazi yao na kuendeleza shughuli zao za maisha pamoja na kidini. Anayeijua Zanzibar vizuri atakumbuka kwamba ilikuwa taabu kumtambua Muislam au Mkristo kwa sababu wafuasi wengi wa dini hizo walikuwa na tamaduni za mavazi ya aina moja, wakicheza na kusoma pamoja. Baadhi ya ndugu zetu hao leo tunaishi nao pamoja.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Hii ndio hali ya dini ya Kiislamu na Ukristo hapa Zanzibar. Kuvumiliana na kuelewana kulikuwa ni chachu ya amani kwa muda mrefu na kulichangia kuondoa ubaguzi. Kwa mara nyingi sherehe zao zilikuwa zinahudhuriwa na watu wa dini zote. Aidha, wafuasi wa dini hizo walikuwa wakihudhuria shughuli za jamii kwa pamoja na kujadili mambo ya maslahi ya nchi kwa pamoja. Katika Afrika Mashariki ukiongelea uvumilivu wa kidini mfano mzuri ni wa hapa Zanzibar. Mnamo mwaka 1953 yalifanyika mashindano ya sanaa ya uchoraji katika eneo la Afrika Mashariki ya kuonesha uvumilivu wa kidini. Mshindi wa mashindano haya alitokea Zanzibar ambae mchoro wake ulionesha msikiti, kanisa na baina yake palikuwa na temple. Mchoro huu uliashiria mfungamano wa kidini wa watu wa Zanzibar tangu enzi .

Zaidi ya maelezo hayo ya kihistoria, Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 19(1) kimeelezea kuwa “kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha dini au imani yake”, ambapo pia, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayo inazungumzia hayo hayo. Aidha, miongoni mwa masuala tunayokwenda nayo vizuri sisi viongozi ni hili suala la kuheshimu imani za dini mbali mbali hapa Zanzibar.

Mfano ni tarehe 16 Septemba, 2011, mimi nikiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi nilikutana na viongozi wa dini mbali mbali waliokuwa wakijihusisha na juhudi za kuendeleza amani nchini. Pia, nilihudhuria kutawazwa kwa Askofu Michael Henry Hafidh wa kanisa la Aglikana tarehe 15 Aprili mwaka huu na nilipewa fursa ya kuhutubia wafuasi na kuwaelezea msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya imani za watu na kutobagua dini.

Kadhalika, mimi na viongozi wenzangu tumekuwa tukikutana na kujadiliana na viongozi kadhaa wa dini ya Kiislamu. Kwa mfano tarehe 25 Aprili, 2012 Kamati maalum ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikutana na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Maimamu na Mashekhe kuzungumzia hali iliyotokea nchini katika kufanya mihadhara ikiashiria kama kwamba kutatokea uvunjwaji wa amani tuliyonayo. Kamati hiyo ilifanya kazi nzuri sana. Tutaendelea na utaratibu huu wa kukutana na viongozi wa dini zote ili kujadiliana hali halisi katika jamii. Hivi majuzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi pamoja na IGP Said Mwema, wamefanya hivyo juzi na mikutano kama hiyo itaendelea kufanywa kwa utaratibu wake.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Tunaelewa vyema kwamba mustakabali wa nchi yetu umo katika mjadala mkubwa wa kisiasa. Msingi mkuu wa hayo ni mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa maridhiano ya viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tulikubaliana kuwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kikao cha pamoja na viongozi wa dini zote Aprili 25, mwaka huu, iliwasihi sana viongozi hao watumie busara na wafuate taratibu zilizowekwa kuhusu marekebisho ya katiba. Walitakiwa kuwaomba wafuasi wao kuepuka matumizi ya lugha na vitendo vinavyoashiria uvunjaji wa amani katika nchi yetu. Wote walitakiwa kushiriki ipasavyo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba utakapoanza.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Wakati huo huo, kabla ya kuanza mchakato wa mabadiliko ya katiba, Serikali zetu mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tangu mwaka 2006 tumekuwa tukifanya mazungumzo ya pamoja kuhusu mambo ya Muungano kupitia Kamati ya pamoja inayozungumzia mambo ya Muungano inayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuzungumzia kero za Muungano. Mimi nilipata nafasi ya kuingonoza Kamati hii kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Hivi sasa Kamati hio inaongozwa na Mheshimiwa Dk. Mohammed Gharib Bilal ili kujadili kero na mapungufu katika mambo mbali mbali ya Muungano wetu.

Vikao mbali mbali vinaendelea kufanyika. Pande zote mbili zimekuwa zikiwasilisha mambo ambayo yanajichomoza na yanayoendelea kuchomoza kama kero kwa Sekretarieti ambayo ina wajumbe sita, watatu kutoka kila upande wa Muungano.

Sekretarieti hii ina jukumu la kuandaa ajenda za mikutano ya ngazi za Wataalamu, Makatibu Wakuu, Mawaziri na hatimae kikao cha juu kabisa kinachowajumuisha Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uwenyekiti wa Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa vikao vilivyofanyika ni:
1. Vikao 4 vya Sekretarieti vilivyofanyika kwa lengo ka kuratibu utekelezaji wa yatokanayo katika kikao cha mambo ya Muungano.
2. Vikao 6 vya ngazi ya watendaji wa sekta mbali mbali husika kujadili utekelezaji na taratibu za kisheria kwa mambo yote ambayo yameainishwa katika kero za Muungano.
3. Vikao 4 vya ngazi ya Makatibu Wakuu kujadili maamuzi ya watendaji.
4. Vikao vitatu vya ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kuandaa mapendekezo ya kikao cha juu cha mambo ya Muungano.
5. Kikao kimoja kati ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Januari mwaka huu.

Wana ratiba ya kuandaa kikao chengine hivi karibuni.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza hadi sasa na yaliyopata nafasi ya kujadiliwa ni haya yafuatayo:
1. Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
3. Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu.
4. Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Nje.
5. Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
6. Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa Ndani na Nje ya Nchi.
7. Kodi ya Mapato.
8. Usajili wa vyombo vya moto.
9. Ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.
10. Uharamia na utekaji nyara wa Meli.
11. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
12. Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Changamoto zipo na zitafanyiwa kazi.

Nimeona haya niyaseme ili wananchi waelewe mambo haya muhuimu yanayofanywa na Serikali zote mbili juu ya suala hili.

Kutokana na jitihada hizi zinazochukuliwa na Serikali zote mbili, pamoja na kuitumia vizuri fursa tuliyopewa ya kuweza kuwasilisha maoni yetu katika marekebisho ya Katiba, matumaini yangu ni kuwa kwa pamoja tutaweza kuondosha kero hizi na kuandaa Katiba mpya itakayotuletea maendeleo makubwa nchi yetu. Haya ni masuala muhimu kwa ustawi wa nchi yetu. Nawasihi wananchi wayakabili wakiwa na subira na busara ili tuijengee mustakbali mzuri nchi yetu katika mambo 12 niliyoyaorodhesha hapo juu mambo mengi tayari yamepatiwa ufumbuzi na yapo baadhi ambayo yanafanyiwa kazi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar alitangaza majina ya Tume ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Jaji Agostino Ramadhani. Naelewa kuwa hadi sasa sio wananchi wengi wanaoijuwa sheria hiyo. Tume inafanya utaratibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hii ili wapate kutoa maoni yao kwa njia bora zaidi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yo yote ile, wako huru kutoa maoni yao kwa njia ya amani na salama kwa Tume hiyo itakapokuja kuanza kazi zake. Aidha, wananchi hawajawekewa vizuizi katika kutoa maoni yao, ila tu ni kuzingatia sheria za nchi na taratibu zake. Tume nayo imepewa uhuru wa kusikiliza maoni ya wananchi kwa kuzingatia sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (Toleo la mwaka 2012).

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Ni jambo la kusikitisha sana na kutia majonzi kuwa katika siku chache zilizopita kumezuka vitendo vya uvunjaji sheria. Tumeshuhudia maandamano na mikutano yenye sura ya dini lakini yenye ujumbe wa siasa, hasa kwa kuuzungumzia Muungano wetu. Vitendo hivyo vilikuwa chachu ya machafuko yaliyojitokeza tarehe 26 Mei, 2012.

Viongozi na wafuasi wao wasiojali sheria, ustaarabu na utamaduni wa kihistoria wa Kizanzibari walichoma moto majengo, mali za watu wasio na hatia na makanisa, wamevunja maduka ya raia na kuiba mali zao na wamekuwa wakitoa matamshi ya vitisho na ubaguzi ambavyo vimejenga khofu kwa wananchi. Nimeshangaa sana uhusiano gani uliopo kati ya kuzungumzia muungano na matukio hayo ambayo hatukuyatarajia kutokea. Haya ni kinyumbe na Katiba na sheria zetu – lakini yametokea.

Mtakumbuka kwamba hivi karibuni, tarehe 21 Machi, 2012 nilikuwa na ziara kwenye mikoa mitano ya Zanzibar. Katika mikutano yangu ya majumuisho wakati wa ziara ya wilaya zetu zote za Unguja na Pemba, nilikuwa nikitahadharisha sana na kueleza kwamba hatutovumilia kwa hali yoyote uvunjaji wa sheria. Nilisema katika Mkutano wangu wa mwisho wa majumuisho, tarehe 9 Mei, 2012 baada ya ziara ya Mkoa wa Kusini Unguja, kwamba Serikali haitomuonea muhali mtu yeyote atayethubutu kuharibu amani yetu. Hilo lilikuwa ni onyo kwa kila mmoja wetu. Maana ishara tuliziona kupitia mihadhara yao na Serikali ilichukua jitihada za kukabiliana nayo kwa kuzungumza nao.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Kutokana na matokeo hayo ya siku ya tarehe 26 Mei, 2012, Jeshi letu la Polisi lilichukua hatua za haraka kuidhibiti hali iliyojitokeza, wengi wenu mliiona hali ilivyokuwa. Kadhalika, Jeshi la Polisi walihakikisha kwamba wale wote waliohusika na vitendo hivyo vya uharibifu na aibu kwa nchi yetu na jamii ya Kizanzibari wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuzingatia sheria za nchi ziliopo hapa Zanzibar. Hakuna atakaeonewa wala kudhulumiwa na kila mmoja atahukumiwa kwa kesi inayomuhusu na kwa mujibu wa sheria ziliopo.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Nachukua fursa hii kwanza kutoa pole kwa ndugu zetu waliotiwa hasara ya mali zao. Pia, nawapa pole wananchi wote kwa usumbufu wote uliojitokeza. Naelewa vyema kuwa wananchi wamepata hasara kubwa ya kiuchumi kwa baadhi ya wananchi kuvunjiwa maduka yao, kuibiwa na pia kukatizwa shughuli zao za kujitafutia riziki na maisha yao. Kwa bahati mbaya, wako pia waliofikwa na matatizo ambayo hawakuyategemea wala kuyazowea wakati polisi wakifanya kazi zao. Serikali inaendelea kufanya tathmini ya hasara zilizotokea na pia inazingatia hatua za kuchukua katika hasara hizo.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Baada ya hayo, napenda kuwaarifu wananchi wote kwamba hatua za Serikali zetu mbili kuidhibiti hali ya usalama zitaendelea, ili amani idumu na usalama wa wananchi, mali na maisha yao uwepo wakati wote. Kwa wale wanao vunja sheria na viongozi wao tunawataka watambue kwamba Serikali hatovumilia vitendo walivyovifanya. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu ye yote atakayevunja sheria na yule mwenye lengo la kuiharibu amani na utulivu wetu. Amani ambayo haikuja kwa bahati tu, bali imehangaikiwa kwa muda mrefu, tutailinda hali hiyo kwa nguvu zetu zote.

Kadhalika, nataka wananchi waelewe kwamba Serikali haitoingilia shughuli za kweli za kidini au vitendo halali vya viongozi na wafuasi wa dini yoyote. Kwa wale wenye maoni juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tungewasihi sana wasubiri utaratibu wa kutoa maoni kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavyotangaza. Wafahamu fika kwamba kwenda kinyume na sheria iliopo ni kosa la jinai, kwa sababu ni sheria iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama ilivyozoeleka, shughuli za ibada za pamoja zifanywe katika nyumba za ibada na ikiwepo haja ya kufanya nje, iwe kwa kufuata taratibu zilizowekwa nchini haya yanajulikana na lazima yazingatiwe. Kwa kutunza amani na utulivu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imetangaza hatua kadhaa, miongoni mwa hatua hizo ni kupiga marufuku mikusanyiko ya aina mbali mbali, maandamano na mihadhara ambayo haijapata kibali cha Serikali hili ni lazima kila mmoja wetu azingatie, huu sio wakati wa kubeza, na kila mtu azingatie sheria. Mikutano ya halali ya kijamii haitaingiliwa hata siku moja na pale pa kutaka ulinzi Jeshi la Polisi litafanya hivyo. Napenda kuwatoa hofu waumini wa dini zote kwamba shughuli za ibada hazitoingiliwa na waumini wa dini hizo wataendelea na ibada zao kama Katiba ya Zanzibar ya 1984 na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Pamoja na kudhibiti amani na kuwahakikishia usalama wananchi, juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea pia kudumisha sifa ya kuendeleza amani ambayo kama itapungua seuze kuondoka kwake kutaathiri utalii ambao ni tegemeo la uchumi wetu, ni jukumu letu kuendeleza amani na ni jukumu letu kuwalinda wageni wetu wanaokuja kututembelea. Kuathirika kwa utalii kutawaathiri wananchi ambao kwa kiasi ya asilimia 60 za shughuli zao zinahusiana na sekta hiyo. Wananchi hawa ni pamoja na wakulima, wavuvi na wafanyabiashara mbali mbali zikiwemo zile biashara za usafiri, mikahawa na hoteli. Nimeshabainisha katika mikutano mbali mbali kuwa sekta ya Utalii inachangia zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni tunazoingiza nchini. Tutambue kwamba hao wanaofanya fujo ni waharibifu wa uchumi wetu na kamwe tusiwape nafasi katika kutimiza malengo yao.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Natoa wito kwa wananchi wote wanaopenda amani washirikiane na Serikali yao katika kudumisha amani hiyo. Wafuasi wa dini wazitumie nyumba za ibada kwa kufanyia ibada na kutumia wakati wa ibada zao kuamrishana mema na kukatazana mabaya. Wazazi wachunguze myenendo ya watoto wao na wachukue dhamana yao ya kuwalea watoto hao katika maadili mema na kila wakati wawatahadharishe juu ya kutokushiriki katika vitendo vya uvunjaji wa sheria. Viongozi wa jamii nao wanajukumu la kuisaidia jamii katika kufikia misingi ya kuwa raia wema na kutojiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria. Ni jukumu letu sote kuilinda na kuitekeleza misingi ya haki za binadamu na utawala bora, hili ni jukumu la kila mmoja wetu si Serikali tu.

Ni jukumu letu sote tuidumishe misingi ya ustarabu na mila zetu, kwa hakika si vizuri kutaka kuiga kila tuliloliona katika nchi za nje. Lakini tuyaige yaliyo mazuri yenye kujenga uadilifu na utamaduni bora, lakini katu mabaya tusiyaige hayana maana kwetu. Aidha, wakati Serikali inaendelea kudhibiti usalama, nawataka viongozi hasa viongozi wa jamii wawache kutoa lawama zisizokuwa na msingi katika hali hii. Viongozi wa dini, siasa na jamii wawe waangalifu wa matamshi yao, kwani Zanzibar na Tanzania ni yetu sote. Linapoharibika ni letu sote na linapotengamaa ni letu sote.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,

Kwa kumalizia, natoa tena pole kwa wananchi wote wa Zanzibar na ndugu zetu wa kikristo walioathirika na vitendo viovu vilivyotokea hivi karibuni. Pia, nawapa pole wale wote walioathirika kwa njia mbali mbali.

Nawasihi sana wananchi tuendelee kuvumiliana, tuheshimiane na tushirikiane katika shughuli hasa zile za kuiletea maendeleo nchi yetu na kila mmoja wetu kupata manufaa. Tuendele kupendana na tudumishe umoja wetu kama ulivyo utamaduni na silka zetu. Jeshi letu la Polisi litaendelea na kutimiza wajibu wao kwa faida yetu na amani ya nchi yetu. Nataka niwahakikishie wananchi wote kwamba tutaendelea kuyalinda Mapinduzi, tutayaendeleza kwa ajili ya maslahi ya kila mmoja wetu na Wazanzibari wote. Nataka niwahakikishie wananchi wote kuwa Mapinduzi yetu tutayalinda kwa maslahi ya wananchi wetu wote.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Popular Posts