Richard Bukos na Issa Mnally
  USIOMBE yakukute!  Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kusikia kisa cha aliyewahi kuwa mpenzi  wa mwanamuziki wa TAKEU, Nice Lucas Mkenda ‘Mr. Nice’, Lulu John  (mwenye blauzi nyekundu) anayedai kumfumania mumewe (siyo Mr. Nice),  Risasi Mchanganyiko linafunguka.
  Lulu alidai kumfumania bwana’ke  Abdulatif Salum na mwanamke ambaye jina halikupatika kwenye gesti moja  iliyopo Kinondoni B jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.
  SINEMA ILIKUWA HIVI 
  Kwa mujibu wa Lulu, akiwa kwenye mihangahiko  ya kusaka bingo, alitonywa na mtu wake wa karibu kuwa mumewe Abdulatif  yupo kwenye nyumba hiyo ya wageni akiigagadua amri ya sita nje ya  mkataba.
  Lulu, baada ya kuthibitishiwa kuwa mumewe anacheza ‘nje  kapu’ ndipo akakodi bodaboda fasta na kuwahi eneo la tukio kwani naye  siyo mgeni wa uwanja huo wa mechi za kitandani. 
  Alidai kuwa ilimchukua dakika 12 tu kutoka Kijitonyama, Dar anakoishi na mumewe hadi eneo la tukio.
  MPAKA CHUMBANI
  Aliendelea kusema kuwa baada ya kutimba mahali  hapo alikwenda moja kwa zote hadi kwenye chumba walichojichimbia wawili  hao na kuanza kubamiza mlango huku akipiga mayowe ya kuomba msaada.
  WENGINE WADHANI WAMEFUMANIWA
  Huku akizidisha kupiga kelele  akitaka kuvunja mlango, ndipo akakatiza stimu za watu wengine waliokuwa  wakilimega tunda tamtam kwenye vyumba vingine ambao walitoka kwa kihoro  wakidhani wamefumaniwa wao.
  MUME ATIMKA NA NGUO YA NDANI
  Aliendelea kusimulia mkasa kuwa watu  walianza kujaa nje ya chumba hicho ndipo Abdulatif akafungua mlango kwa  kasi na kutimka kama mkizi akiwa na nguo ya ndani pekee kisha akaruka  fensi.
  WATU WEWEEE!
  Alisema kuwa wakati anachomoka nduki alimgonga  kikumbo Lulu na kumwangusha chini huku akimwacha akigaragara ambapo watu  walikuwa wakimkimbiza wakisema: “Weweee.”
  VITA
  Baada ya kunyanyuka na Abdulatif kumchomoka hivihivi ndipo vita kuu ikaanza dhidi ya mgoni wake.
  ANG’ATWA PUA
  Alisema kuwa ngumi za uhakika zilipigwa hadi yeye  (Lulu) akang’atwa pua ambapo alitokwa na damu chapachapa usoni huku  aliyefumaniwa akitafuta njia ya kujisitiri baada ya kuchaniwa nguo na  kubaki mtupu.
  Baada ya hali kuwa mbaya, Lulu alisema walitokea  wasamaria wema na kuwatuliza ambapo yeye alikimbilia Kituo cha Polisi  cha Oysterbay, Kinondoni na kumfungulia mgoni wake shitaka la shambulio  la kudhuru mwili lenye jalada la kesi namba OB/RB/12675/2012.
  Kwa  mujibu wa Lulu, kitendo cha kumfumania mwanaume huyo kimemuumiza kwani  amekuwa akimtunza kwa hali na mali na hakuweza kuamini kama angeweza  kumsaliti. 
  Juhudi za kumpata Abdulatif hazikuzaa matunda hadi gazeti hili linakwenda mitamboni hata hivyo zinaendelea.
  KWA NINI USIOMBE YAKUKUTE?
  Lilikuwa ni tukio la aina yake ambalo  halikuishia pale gesti tu bali liliingia mtaani ambapo vitendo vya  Abdulatif kukimbia akiwa mtupu na Lulu kung’atwa pua viligeuka gumzo na  kila mtu akimuomba Mungu asikutwe na kasheshe kama hilo.
 





