![]()  | 
| Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa akizungumza na waandishi wa habari leo | 
YAH; UPOTOSHAJI WA ZIARA ZA CHAMA MIKOANI
Toka tarehe  03/05/2012 nimekuwa na ziara kadhaa za kichama katika mikoa mbalimbali  kwa lengo la kukiimarisha Chama. Baadhi ya mikoa niliyofanikiwa kufika  ni pamoja na Ruvuma, Njombe, Iringa,Mbeya,Kagera,Rukwa na Katavi. Ziara  hizi zimekuwa zikilenga kufanya yafuatayo kati ya mengi niliyofanya:
1.     Kukagua uhai wa Chama
2.     Kukagua maendeleo ya uchaguzi ndani ya Chama
3.     Kukagua miradi mbalimbali ya kiuchumi ya Chama
4.     Kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
Kwa muda  sasa pamekuwa na juhudi za makusudi za kupotosha nia na madhumuni ya  ziara hizi na kujaribu kuonyesha kuwa kinachofanyika hakina baraka za  Chama na hivyo kimesababisha mgogoro ndani ya Chama, hasa kati yangu na  Katibu Mkuu.
Juhudi hizi  zimelenga kukatisha tamaa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Chama za  kuwa karibu na wanachama wake na wananchi. Kwa bahati nzuri vyombo vya  habari vinavyotumika kusambaza uzushi na uongo huu vinajulikana ni vya  nani, hivyo ni rahisi kujua kwanini wanafanya wayafanyayo.
Kwa mfano,  wanadai kuna pesa nyingi ninapewa mimi kama Katibu wa Itikadi na Uenezi  na ninapewa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM bila Baraka za Katibu Mkuu  wangu ambaye ndiye msimamizi wangu mkuu na kwamba hilo limezua  malalamiko na migongano kati yetu.
Huu ni  uzushi wa kitoto sana, kwani wanataka kuwaaminisha wana CCM na wananchi  kwa ujumla kuwa mambo si shwari ndani ya CCM. Huku wakipuuza ukweli kuwa  Katibu Mkuu wa CCM ndo msimamizi wa mapato na matumizi yote ya CCM,  hivyo kama kuna ziara au jambo linalohusu matumizi ya pesa ndani ya  Chama, lazima liwe na baraka zake.
Lakini  wanafumba macho ili wasione kuwa, Katibu Mkuu wa CCM ndio mwenyekiti wa  sekretarite ya Chama Taifa, hivyo sisi wajumbe wote wa sekretarieti  tunafanya kazi chini ya maagizo na usimamizi wake wa karibu. Kama kuna  mafanikio yeyote basi mwasisi wa mafanikio hayo ni Katibu Mkuu wa CCM  Taifa ndugu Wilson Mukama, kwani yeye ndiye kiongozi wa sekretarieti  hii.
Itakumbukwa  kuwa nilipoanza ziara hizi, wapotoshaji hawa walituhumu ziara zangu kuwa  zinalengo la kutisha baadhi ya watu wasigombee nafasi mbalimbali ndani  ya Chama kisa wao na mimi tuna mitazamo tofauti ndani ya chama.  Nilipowataka kulithibitisha hilo na wakashindwa, sasa wamekuja na tuhuma  mpya.
Nawaomba  wana CCM, wapenzi na mashabiki wa CCM na wananchi kwa ujumla kuupuuza  uongo na uzushi huu kwani hauna ukweli wowote. Umetungwa na watu wenye  roho mbaya wasioitakia mema CCM, wanaotamani kuona CCM haitulii na hivyo  mambo yasimame ndio furaha yao. Sasa wakiona mambo yanakwenda viroho  vyao vinawauma.
Nataka  niwathibitishie  sekretarieti ya Taifa ya CCM iko imara, thabiti,  madhubuti na yenye mshikamano tukifanya kazi kwa pamoja na upendo chini  ya uongozi imara wa Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Mukama.Wanao yatunga na  kuyasambaza haya wanapoteza muda wao.
Nawathibitishia  uzushi huu hauta athiri kasi yetu ya kujenga Chama chetu wala ari yangu  binafsi katika kukitumikia Chama changu kwa nguvu zote. Hivi  ninavyoongea tayari maandalizi yamekamilika ya mkutano mkubwa wa hadhara  mjini Kigoma siku ya kesho tarehe 19/07/2012 kwa lengo la kuzungumza na  wana Kigoma juu ya mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoukabili  mkoa  wa Kigoma.
Katika  mikutano hii mingi nina ambatana na baadhi ya mawaziri wa wizara  mbalimbali zenye maeneo ya utekelezaji kwenye mikoa husika. Kwa mfano  Kigoma tutazungumzia hatua iliyofikiwa katika sekta ya Uchukuzi kwa  maana ya reli, bandari na anga. Lakini mkoa huu una kero kubwa ya maji  hasa mjini Kigoma. Kuna changamoto kadhaa kwenye serikali za mitaa, kuna  mengi yanayoendelea ya ujenzi wa miundimbinu kama barabara nk.
Staili hii  tunayotumia kwenye mikutano mingi ya hadhara ambayo kwakweli  inatutofautisha sisi Chama tawala na vyama vingine vya saisa nchini,  tuliizindua pale jangwani kwenye ule mkutano mkubwa wa kihistoria mwezi  Mei mwaka huu! Staili hii imepewa jina la AHADI NI DENI. Hivyo wana  Kigoma na maeneo mengine kaeni mkao wa kula, AHADI NI DENI  inakuja  kwenu.
Itakumbukwa  tuliwaahidi katika mkutano wa Jangwani kuwa tutazunguka nchi nzima,  lakini tofauti na wenzetu wanaotukana na kukashifu kila kinachofanyika  na kilichofanyika sisi tunakwenda kupeleka majawabu ya changamoto  mbalimbali kwenye maeneo yao. Na hii ndio tofauti ya vyama vya upinzani  na Chama tawala. Wakati wao wanabeba matusi na kejeli kwenye mikutano  yao, sisi tunabeba majawabu namtumaini kwa wananchi. Kwahiyo “ahadi ni  deni” imelenga kuzipitia ahadi zetu kwa wananchi na namna spidi ya  utekelezaji wake ilivyo.
Nawataka  sasa, hawa wanaozusha maneno na kujaribu kupotosha ziara nizifanyazo  mikoani kuacha mara moja, kwani kukaa kwangu kimya haina maana kuwa  siwafahamu. Nawaonya wakiendelea nitawasema hadharani bila kumumunya  maneno. Nasema inatosha, upotoshaji mliofanya unatosha, sasa basi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;
Nape Mose Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Itikadi na Uenezi
