Pages

Wednesday, July 18, 2012

TAARIFA YA SMZ JUU YA KUZAMA KWA MV STAR GET ZANZIBAR

MAAFA YA KUZAMA KWA MELI ZANZIBAR


Meli ya Mv. Star Gate imezama karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki hadi muda huu na wengine kadhaa wamejeruhiwa.


Akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa za kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli hiyo ikizama.


“Tulipata taarifa kutoka Boti ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana waliporipoti kuona meli ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri Mwinyihaji.


Waziri huyo alisema Meli hiyo imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin Kusini mwa Kisiwa cha Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya Malindi.



Waziri Mwinyihaji alisema idadi ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6. “Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la tukio kushirikiana na waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.


Alisema maiti zote zitapelekwa viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya ndugu na jamaa kuzitambua maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.


Katika Bandari ya Malindi mwandishi wetu ameshuhudia maiti kadhaa zikiwemo za watoto zikishushwa, Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa mbalimbali ya nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake amepoteza maisha.


Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Mawaziri na baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi walikuwepo kutoa msaada unaohitajika.


Katika eneo la pembezoni mwa bandari ya Malindi, makundi ya wananchi yalikuwa yamekusanyika wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.


Vikosi vya ulinzi na usalama, msalaba mwekundu na watoaji wengine wa misaada ya dharura walifika kwa haraka eneo la tukio.


Hadi sasa kazi ya uokoaji inaendelea karibu na Kisiwa cha Yasin ilikozama meli hiyo.


Meli ya Mv. Star Gate inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd ambayo mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.


Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders kuzama katika bahari ya Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea Kisiwani Pemba ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.


Taarifa zaidi zitatolewa hapo baadea.


Imetolewa na:
Idara ya Habari(MAELEZO) ZanzĂ­bar
Julia 18,2012

Picha ziadi maafa ya meli




Watalii na raia wa kigeni pia walikuwemo katika meli iliyozama hawa ni baadhi ya waliosalimika


Abiria waliookolewa kutoka katika meli iliozama ya Star Gate katika bahari ya Chumbe Zanzibar
Abiria aliyeokoka kutoka katika meli iliyozama

Abiria aliyookoka katika Meli iliozama ya Star Gate akifarijiwa na Jamaa zake Baada ya kuteremka katika Meli iliowaokoa hapo Bandarini




Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad akiwa katika hali ya huzuni Baada ya kushiriki katika uokoaji na kuwaona Majeruhiwaliookolewa katika Meli iliozama ya Star Gate wakiteremka hapo Bandarini Zanzibar.

Askari wa Vikosi mbalimbali wakiwa katika kazi ya Uokozi kwa Abiria waliokuwa katika Meli ya Star Gate ambayo iliozama katika ikiwa imebeba abiria 250 huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar


Picha zoe na Yussuf Simai Maelezo

Popular Posts