Afisa Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Nd. Juma  Kimtu akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali  Iddi Mchango wa Maafa wa Shilingi 10,000,000/- hapo ofisini kwake Mbweni  nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Nyuma yake ni Meneja Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {  ZSSF } Nd. Khamis Phil Phil Than.  
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea mchango  wa Maafa wa shilingi 10,000,000/- kutoka kwa Meneja Msuluhishi wa Mfuko  wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis Phil Phil Than hapo  katika Ofisi yake iliyopo Baraza la Wawakilishi  Mbweni nje kidogo ya  Mji wa Zanzibar.
  ---
    Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi  Wananchi kuendelea kuiamini Serikali katika kupokea Taarifa zake hasa  wakati wa kutokea  Majanga na Maafa.
    Nasaha hizo amezito hapo katika Ofisini yake iliyopo Baraza la  Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akipokewa mkono  wa Pole kutoka kwa Taasisi mbali mbali za Umma na Kijamii. 
   Salamu hizo za mkono wa pole zimetolewa kwa Balozi Seif na Uongozi wa  Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } na ule wa Hifadhi ya Taifa  ya Jamii ya Tanzania { NSSF } ambapo kila moja ilikabidhi mchango wa  Shilingi Milioni kumi { 1,000,000/- }. 
   Balozi Seif alisema Jamii kujenga tabia ya kuiamini  Serikali  hupelekea  kuwepuka kuchanganywa wakati wa kupokea Taarifa hizo kutoka   vyombo  vya Habari vinavyopokea Baadhi ya Taarifa zisizo rasmi. 
   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa mifuko hiyo ya  Hifadhi ya Jamii Bara na Zanzibar kwa kufikiria jambo hilo muhimu la  kutoa mchango ambalo Taifa linahitaji kuungwa mkono katika kukabiliana  nalo.
    Aliuhakikishia Uongozi wa Taasisi hizo kwamba michango hiyo itasimamiwa  vyema kwa ajili ya kuwafika waliohusika kwa kutumia utaratibu  uliotumika wakati wa ajali iliyotokea Mwaka jana. 
   Alisema licha ya zoezi la uokozi kuwa na gharama kubwa lakini Serikali   inaendelea kutoa huduma zote za mazishi na usafirishaji wa maiti   zinazopelekwa Tanzania Bara ambazo zilipatikana kutokana na ajali ya  Meli ya M.V Skagit hapo juzi. 
   Aliongeza kuwa shughuli hiyo ikiwemo gharama za vyombo, mafuta, Chakula  na uokozi zinahitaji kuungwa mkono na taasisi na jumuiya ya kiraia ndani  na nje ya Nchi. “ Serikali imeshachukua jukumu la kuzizika zile Maiti zilizoshindwa  kutambulika hadi sasa, kuzisafirisha maiti tatu hadi Tanzania Bara  pamoja na familia nne wakati maiti moja ya raia wa kigeni bado  haijatambulika”. Alifafanua Balozi Seif. 
   Alisisitiza kwamba katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo wazamiaji  wa Israel walioko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja wameamua kusaidia  kazi ya uokozi kwenya Meli hiyo ili kuendelea kutafuta miili ya Watu  iliyopotea.
   Mapema Meneja Msuluhishi wa Mfuko  wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Ndugu Khamis Phil Phil Than alisema yapo mambo mengi kwenye  tukio hilo la Maafa ambayo yanahitajika kupata msukumo kutoka kwa  Washirika, Taasisi na Jumuiya za Kiraia. Ndugu Phil Phil alisema mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar umekuwa  mstari wa mbele katika  kutekeleza majukumu yake yaliyolenga zaidi  kwenye eneo la Jamii. 
   Naye kwa upande wake Ofisa  Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF }  kutoka Makao Makuu Mjini Dar es salaam Nd. Juma Kimtu alimueleza Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo imeamua kutoa mchango  huo baada ya kuona uzito Maafa yaliyotokea ambayo yameigusa Jamii yote.
    Ndugu Kimtu alisema Serikali kwa  kuwa  ni ya watu haina budi wakati wote kusaidiwa hasa katika masuala  ya Majanga na Maafa ambayo kwa kiasi kikubwa huigusa Jamii yote.
  Na
  Othman Hamisi Ame
  Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Rais Zanzibar